Junguni yaweka rekodi kufungwa
Muktasari:
- Hiyo ni idadi kubwa ya mabao ya kufungwa kwa timu ndani ya msimu mmoja wa ligi hiyo tangu kuanzishwa kwake.
LIGI Kuu ya Zanzibar msimu wa 2025-2026 imemalizika Juni 12, 2026 kwa timu ya KVZ kutwaa ubingwa huo huku Junguni ikiweka rekodi ya kufungwa mabao 106 kwenye michezo 30.
Hiyo ni idadi kubwa ya mabao ya kufungwa kwa timu ndani ya msimu mmoja wa ligi hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Timu hiyo ni miongoni mwa nne zilizoshuka daraja na msimu ujao itacheza Ligi Daraja la Kwanza sambamba na New Stone Town, New King na Malindi.
Junguni kuruhusu idadi hiyo ya mabao imechangiwa na kupoteza mechi kumi kati ya 30 kwa vipigo vikubwa ndani ya Ligi Kuu Zanzibar.
Matokeo ya mechi hizo yalikuwa kama hivi: Junguni 1-9 Polisi, Fufuni 8-0 Junguni, KMKM 9-0 Junguni, JKU 6-1 Junguni, Muembe Makumbi 6-1 Junguni, Mlandege 6-1 Junguni, KMKM 6- 1 Junguni, Kipanga 6-1 Junguni, Uhamiaji 5-1 Junguni na Mlandege 5-1 Junguni.
Katika mechi hizo kumi pekee, imeshuhudiwa Junguni ikifungwa mabao 66.
Kati ya mechi 30 ilizocheza Junguni United, imeshinda mbili, sare nne na kupoteza 24 huku ikifunga mabao 23 na kukusanya pointi 10.
Timu hiyo ilianza vibaya msimu kwani ilikuwa ya kwanza kutozwa faini ya Sh200,000 kwa kufika uwanjani bila ya kuvaa jezi jambo ambalo lilisababisha kuvunjwa kwa mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 dhidi ya Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba.
Mbali na Junguni, timu ya New Stone Town inafuatia kwa kufungwa mabao mengi (81), Malindi (50) na New King (46) ambazo zote zimeshuka daraja.