Josiah anazitaka nne ngumu Tanzania Prisons

Muktasari:
- Ushindi wa pointi nne ambazo zinaonekana kuwa ngumu utakinasua moja kwa moja kikosi hicho na janga la kushuka daraja.
USHINDI katika mechi nne mfululizo umeonekana kuipa nguvu Tanzania Prisons, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah akiamini mechi mbili zilizobaki dhidi ya Yanga na Singida Black Stars atapata pointi nne anazozitaka ili timu iwe salama.
Ushindi wa pointi nne ambazo zinaonekana kuwa ngumu utakinasua moja kwa moja kikosi hicho na janga la kushuka daraja.
Tanzania Prisons iliyoanza msimu kwa kuchechemea, ilikuwa chini ya Kocha Mbwana Makata ambaye alibadilishwa kisha mabosi wa timu hiyo wakampa kazi Josiah ambaye ni mara ya kwanza kuongoza timu ya Ligi Kuu Bara akiwa kocha mkuu.
Juzi ikicheza dhidi ya Coastal Union na kutakata kwa mabao 2-1, imeifanya Tanzania Prisons kushinda mechi nne mfululizo dhidi ya Kagera Sugar (3-1), KenGold (3-2), JKT Tanzania (3-2) na Coastal Union (2-1). Sasa imefikisha pointi 30 baada ya mechi 28, zikibaki mbili kumaliza msimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah alisema ushindi dhidi ya Coastal Union umewapa uhakika wa kutoshuka daraja moja kwa moja, hivyo kwa sasa wanahitaji kupambana kujinasua kwenye nafasi ya play off ili kuwa salama kabisa.
Alisema mechi zilizobaki hawataangalia wanacheza na nani na wapi badala yake mkakati utakuwa ni vita ya pointi tatu, huku akiwapongeza nyota wa kikosi hicho kwa kazi wanayofanya.
“Kikubwa ni kuwapunguzia hofu wachezaji ili watumie akili zao wenyewe, timu inavyocheza ni matokeo ya mazoezi, haya ni mafanio ya wote, kwa pamoja tunashukuru sapoti ya wadau.
“Ratiba ilivyo hakuna anayetaka kusubiri kucheza play off, kati ya mechi mbili tunahitaji japo pointi nne, tunaanza na mechi ijayo Sokoine dhidi ya Yanga,” alisema Josiah.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Biashara United na Tunduru Korosho, anasaka rekodi ya kuibakiza timu Ligi Kuu ili kuandika historia mpya, vinginevyo huenda akachafua wasifu wake.
Naye kipa wa Tanzania Prisons, Mussa Mbisa amesema sasa wamepata ahueni.
Mbisa aliyecheza mechi 22 akiwa na cleansheet tano huku akiruhusu mabao 23, amesema awali walikuwa wanaishi kwa presha kubwa na kuumiza vichwa namna ya kuhakikisha timu inasalia salama, lakini sasa licha ya kutokuwa nafasi nzuri ila anaona wamepata ahueni ya kubaki Ligi Kuu.
“Msimu huu ulikuwa mchungu sana kwetu, lakini hatukuwahi kukata tamaa kupambana, angalau nafasi tuliyopo tunaona mwanga wa kusalia Ligi Kuu,” alisema na kuongeza.
“Ili tuwe na uhakika zaidi tunatakiwa kushinda mechi ngumu mbili zilizosalia mbele yetu dhidi ya Yanga na Singida Black Stars.”
Nyota mwingine wa kikosi hicho aliyefurahishwa na matokeo mazuri ya timu hiyo ni mshambuliaji Jeremiah Juma aliyesema: “Jambo kubwa kwetu ilikuwa ni timu kusalia Ligi Kuu, hilo tunaliona linakwenda kutimia, kikubwa ni kupambana na mechi zilizosalia.”
Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Benjamin Asukile alisema: “Mbele yetu tuna mechi mbili ngumu, ila naamini kwa sasa wachezaji wana morali ya juu wanaweza wakashinda michezo hiyo.”
Maafande hao wa Magereza watarejea uwanjani Juni 18 kuikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kisha kumalizia ligi ugenini Juni 22 dhidi ya Singida Black Stars.