Ngoja tuone! Rekodi zinazosubiriwa kuvunjwa Ligi Kuu England msimu huu
Muktasari:
- Kwa mfano, Arsenal inashika usukani wa Ligi Kuu England kwa sasa na kwenye mchakamchaka huo wa kusaka taji hilo kwa msimu huu kuna rekodi kibao zinatarajiwa kwenda kuzivunja.
LONDON, ENGLAND: REKODI zinawekwa ili zivunjwe. Hata za Ligi Kuu England, hadithi ni hiyo hiyo zimewekwa ili zivunjwe.
Kwa mfano, Arsenal inashika usukani wa Ligi Kuu England kwa sasa na kwenye mchakamchaka huo wa kusaka taji hilo kwa msimu huu kuna rekodi kibao zinatarajiwa kwenda kuzivunja.
Msimu wa 2025-26 umeanza kunoga kwenye Ligi Kuu England na kinachoelezwa ni kwamba kuna rekodi kibao zitakwenda kuvunjwa.
Je, ni rekodi gani zinaweza kuvunjwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu? Mambo ni moto.
1. Kufungwa mabao machache – 15 (Chelsea, 2004/05)
Hii ilikuwa rekodi kwenye Ligi Kuu England ambayo ni ngumu kuvunjwa. Timu iliyokaribia kufikia rekodi hiyo ilifungwa mabao 22 na ilikuwa Chelsea tena msimu wa 2005/06, sambamba na Manchester United (2007/08) na Liverpool (2018/19).
Rekodi hiyo inaweza kuvunjwa msimu huu na vinara Arsenal, ambapo hadi sasa kwenye mechi 10 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England imeruhusu mabao matatu tu. Ngome yake ya mabeki ni ngumu kufungika.
2. Mechi nyingi bila kuruhusu bao – 11 (Liverpool, 2005)
Katika miaka ya 2000 mechi ilizokutanisha Liverpool na Chelsea ilikuwa ni vita vya makocha Rafa Benitez na Jose Mourinho.
Chelsea na Liverpool mechi zao zilikuwa vita kali ikiwamo ile ya sare ya 0-0, ambapo ilikuwa na matukio mengi ya kibabe uwanjani ikiwamo ya kiungo Michael Essien kumchapa rafu mbaya Dietmar Hamann.
Sare hiyo ya bila kufungana ilikuwa ya tisa kati ya mechi 11, ambapo Liverpool ilicheza bila kuruhusu nyavu kuguswa. Kwenye michuano yote, Liverpool ilifikisha mechi 11 bila kuruhusu bao kitu ambacho Arsenal inaweza kukifikia msimu huu, ambapo hadi sasa imeshuhudia mechi nane katika michuano yote bila kuruhusu bao golini kwake.
3. Mchezaji kufunga mabao mengi – 36 (Erling Haaland, 2022/23)
Kwenye suala la kutumbukiza mipira kwenye nyavu za wapinzani hilo halijawahi kuwa tatizo kabisa kwa straika wa Manchester City, Erling Haaland. Katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England alimaliza akifunga mabao 36, rekodi ambayo bado haijafikiwa katika msimu wa mechi 38 katika ligi hiyo.
Kwa msimu huu hadi sasa zikiwa zimechezwa mechi 10 kwenye Ligi Kuu England, Haaland amefunga mara 13, hivyo kama ataendelea kuweka rekodi yake hiyo ya kufunga mara 13 kwenye kila mechi 10, hiyo inaweza kumweka kwenye wakati mzuri wa uwezekano wa kuvunja rekodi yake mwenyewe ya kufunga mabao 36 katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England.
4. Kucheza mechi nyingi kwenye ligi – 653 (Gareth Barry)
Kwenye Ligi Kuu England mchezaji anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi kwa sasa ni kiungo wa zamani, Gareth Barry, ambaye amecheza mechi 653.
Na katika msimu huu, James Milner amebakiza mechi tisa tu kufikia rekodi hiyo na kuweka alama zake kwenye Ligi Kuu England kama mchezaji aliyetumika kwenye mechi nyingi kuliko wengine.
Milner kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Brighton na tayari ameshatumika kwenye mechi 645 za Ligi Kuu England, akifunga mabao 56 na kuasisti mara 90. Kwa maana hiyo, mechi tisakutoka sasa, Milner atakuwa amevunja rekodi hiyo ya Barry.
5. Sare chache kwa msimu kwenye ligi – 2 (Man City, 2018/19)
Kwenye kipengele hiki, Manchester City haipo pekee yake katika orodha ya timu zilizopata sare chache kwa msimu mmoja katika Ligi Kuu England, ilipotoka sare mbili msimu wa 2018/19, Tottenham Hotspur na yenyewe ilitoka sare mbili msimu huo wa 2018/19 na Sheffield United ilitoka sare mbili 2020/21.
Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, sare ni chache, kwenye mechi 10 zilizochezwa, timu zilizotoka sare nyingi ni sare tatu, huku nyingi zikiwa mbili na moja, lakini Liverpool ikibakia kuwa timu pekee kwenye ligi hiyo hadi sasa ambayo haijatoka sare yoyote na ndiyo inayokimbizia rekodi hiyo ya kutoka sare chache kwa msimu mmoja wa Ligi Kuu England.
6. Pointi chache kwenye msimu mzima – 11 (Derby, 2007/08)
Hii si rekodi nzuri ambayo timu itatamani kuivunja, lakini Wolves kwa sasa kwenye Ligi Kuu England msimu huu kwenye kuivunja, baada ya kukusanya pointi mbili tu kwenye mechi 10 ilizocheza hadi sasa.
Kwa hali ilivyo, Wolves ipo kwenye nafasi kubwa ya kwenda kuvunja rekodi ya kuvuna pointi chache kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu England kama ambayo ilifanya Derby kwenye msimu wa 2007/08.
Kitu kinachotishia zaidi kwa Wolves, hata Derby wakati inaweka rekodi hiyo ya kuvuna pointi chache ilikuwa imekusanya pointi sita kwenye mechi 10, wakati Wolves yenyewe hadi sasa, imevuna pointi mbili tu.
7. Pointi chache nyumbani – 6 (Southampton, 2024/25)
Southampton ilikuwa na wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, wakati iliposhindwa kabisa kutumia vyema faida ya uwanja wake wa nyumbani wa St Mary’s.
Katika uwanja huo, Southampton ilishuhudia ikishinda mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu England kwa msimu mzima, iliposhinda 1-0 dhidi ya Everton, shukrani kwa bao la dakika 85 katika mechi iliyofanyika karibia Novemba na baada ya hapo ilitoka sare tatu uwanjani hapo.
Nottingham Forest, West Ham nap engine Tottenham Hotspur zinaweza kwenda kuvunja rekodi hiyo kutokana na mwenendo wao wa msimu huu, huku Wolves ikiwa nafasi kubwa zaidi baada ya kuvuna pointi moja tu katika mechi tano ilizocheza Molineux hadi sasa.
8. Pointi chache mechi za ugenini – 3 (Derby, 2007/08)
Kushinda ugenini na kunyakua pointi tatu si kitu rahisi na ukitaka kufahamu hilo nenda kawaulize Derby kilichowakuta kwenye msimu wa 2007/08.
Derby ilinyakua pointi moja Craven Cottage, St James’ Park na St Andrew’s na hivyo kuvuna pointi tatu kwenye mechi za ugenini katika ligi ndani ya msimu mzima. Kwa msimu huu,
Nottingham Forest hadi sasa kwenye mechi 10 ilizocheza, imevuna pointi mbili ugenini, hivyo kocha Sean Dyche anapaswa kulitazama hilo kama ilivyo kwa Marco Silva huko Fulham.
Rekodi hiyo ya kuvuna pointi chache kwenye mechi za ugenini, inaweza kuwashindanisha pia Wolves, ambayo hadi sasa ina pointi moja tu iliyopata kwenye mechi za ugenini.
9. Mechi nyingi bila kushinda – 32 (Derby, 2007/08)
Pengine ni rekodi ngumu zaidi kuvunjwa kwenye Ligi Kuu England. Kwa sasa inashikiliwa na Derby, ambayo haipo kwenye ligi tangu iliposhuka katika msimu ambao ilishindwa kupata ushindi kwenye mechi 32. Hata hivyo, kwa msimu huu, rekodi yao hiyo ipo kwenye hatari ya kuvunjwa na Wolves, endapo kama itaendelea na mwenendo wake wa sasa.
Mechi nne bila ya kushinda mwishoni mwa msimu uliopita, zimefanya Wolves hadi sasa kufikisha mechi 10 bila ya ushindi, hiyo ina maana, timu hiyo inaweza kuandikisha rekodi mpya kwenye Ligi Kuu England, endapo kama itaendelea kutoshinda mechi hadi kufikia Machi 4 mwakani itakapokabiliana na Liverpool nyumbani.
10. Kadi nyingi za njano msimu mmoja – 14
Kiungo Joao Palhinha alionyeshwa kadi tano za njano kwenye mechi 10 za kwanza alizocheza Fulham msimu wa 2022/23, wakati Etienne Capoue alionyeshwa kadi nne za njano katika mechi 10 katika kikosi cha Watford msimu wa 2018/19.
Kwa msimu huu kwenye Ligi Kuu England, kuna wachezaji wanane walionyeshwa kadi nne za njano baada ya mechi 10 zilizocheza kwenye ligi.
Lakini, Kiernan Dewsbury-Hall anashika usukani hadi sasa kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuonyeshwa kadi tano za njano katika mechi 10 zilizochezwa, jambo linalotishia kwamba huenda akaenda kuvunja rekodi ya kuonyeshwa kadi nyingi zaidi kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu England, ambapo rekodi kwa sasa ndani ya msimu mmoja ni kadi za njano ni 14.