Prime
Kombe la CRDB linaloamuliwa chumba cha siri
HADI naandika safu hii kulikuwa na habari zilizoenea kuwa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho itachezwa kisiwani Pemba, Zanzibar lakini mamlaka zinazohusika na uandaaji wa mechi hiyo zilikuwa hazijaweka bayana.
Mechi za hatua za mwisho za mashindano hayo maarufu kwa jina la Kombe la CRDB zimekuwa zikichezwa mikoa tofauti kutokana na utashi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kuna wakati hadi kulizuka minong’ono kulalamikia mechi nyingi kuchezwa mkoani Tanga na hivyo uamuzi huo kuhusishwa na utashi wa viongozi wa juu wa TFF wanaotoka mkoani humo.
Hili la mechi ya fainali kupangiwa Pemba nalo limeleta malalmiko na mijadala kuwa uamuzi huo unatokana na msukumo wa kisiasa, kwamba kuna viongozi wa soka wanajishusha kwa viongozi wa kisiasa kwa matarajio fulani.
Hilo ni gumu kulithibitisha na huenda fikra za viongozi wa soka ni ule moto wa kusambaza mpira wa miguu kila kona ya nchi ili mradi tu ni ndani ya mipaka ya Tanzania bila ya kujali sheria na katiba inayotenganisha michezo katika masuala ya Muungano.
Lakini ni muhimu sana uamuzi unaohusu michezo yazingatie mgawanyo wa shughuli za Muungano na zaidi ya yote kuzingatia utamaduni wa mpira wa miguu ambao huweka mashabiki mbele kwa kuwa ndio wanaowezesha mpira wa miguu kufuatwa na wengi na hivyo wawekezaji kuutamani.
Kuhamisha mechi hiyo na kuipeleka sehemu ambayo haihusiki kwa mujibu wa mgawanyo wa shughuli za Muungano, ni kutoheshimu mashabiki wa Tanzania Bara ambao timu zao zimecheza kuanzia hatua ya awali halafu fainali ndio waikose.
Hilo la utashi wa viongozi halifai kuendelea kuwepo. Ni muhimu sana kwa suala hilo liwe la ushirikishwaji ili watu wengi zaidi washiriki katika kuamua medhi ichezwe wapi.
Hivi sasa Manispaa ya Barcelona imewasilisha maombi ya kuandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ya mwaka 2029, ikiwa na matarajio kuwa hadi wakati huo ukarabati wa Uwanja wa Nou Camp utakuwa umekamilika na kuanza kuchukua watu zaidi ya 100,000.
Kukaribisha maombi ya miji kuandaa mechi za hatua za mwisho za mashindano ya Kombe la CRDB ni moja ya mbinu za kushirikisha watu wengi zaidi katika kufanya uamuzi na hivyo kuondoa manung’uniko na hisia mbaya dhidi ya viongozi wa mamlaka.
Ni njia pia inayoondoa mwanya kwa viongozi wa soka kufanya uamuzi kwa maslahi yao binafsi, hasa ya kutaka kujinufaisha kisiasa.
Ni muhimu kwa TFF kubuni mbinu nyingine ya kufanya uamuzi ya mashindano yake na njia hiyo ya kukaribisha maombi ya kuandaa mechi za hatua za mwisho za Kombe la CRDB ingekuwa nzuri zaidi.
Hiyo itawezesha serikali za mikoa kujihusisha zaidi na maandalizi na kuangalia ni kwa jinsi gani maeneo yao yanaweza kunufaika na mechi hizo.
Na unahitaji mechi za kuanzia nusu fainali tu ndio ziandaliwe na mikoa itakayofanikiwa kushinda maombi yao.
Ni suala la TFF kuweka viwango inavyovitaka kwa ajili ya mechi hizo na itakuwa ni wajibu wa mikoa inayotaka kuandaa mechi hizo kuhakikisha inafikia viwango hivyo, kama uwanja bora, usalama, usafiri na huduma za afya au matibabu na mambo mengine muhimu.
Hii itasaidia mikoa na wamiliki wa viwanja kupata muda wa kutosha kuandaa viwanja, kuuandaa umma kwa hamasa, kuandaa fursa zitakazoweza kunufaisha wakazi wao na kuonyesha tamaduni za mikoa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuitangaza mikoa yao kwa kutumia mchezo huu maarufu unaopendwa na mamilioni ya Watanzania.
Hatua hiyo pia itasaidia viongozi wa serikali za mikoa kuona una wajibu wa kutumia vizuri fedha zinazotengwa kwa ajili ya michezo na kuboresha huduma za kijamii.
TFF haina budi kufikiria kwa kina kuhusu uamuzi ya uteuzi wa viwanja kwa ajili ya hatua za mwisho za mechi za Kombe la CRDB na ushirikishwaji wa wadau wake utasaidia kuboresha uandaaji wa hatua za mwisho za mashindano hayo.