Uchaguzi wa Serikali za Mtaa kutoa taswira uchaguzi mkuu

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Singida Magharibi eneo la Puma katika muendelezo wa ziara yake mkoani Singida jana Oktoba 15, 2023.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ametaka uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 utoe taswira ya Uchaguzi Mkuu 2025.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaka uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, utoe taswira ya uchaguzi utakaofuata wa mwaka 2025.

 Ametaka kudumishwa kwa amani na mshikamano miongoni mwa wananchi katika uchaguzi huo, ili kujenga taswira njema ya uchaguzi Mkuu wa 2025.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 16, 2023 alipohutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida baada ya kuzindua Daraja la Msingi katika eneo hilo.

Mbali na kuwataka wananchi wachague viongozi watakaowatumikia, ametumia jukwaa hilo kusisitiza watakaokosa nafasi wasiwe chanzo cha kuunda makundi.

“Unapokosa tusianze sasa kutengeneza makundi tukaanza kubomoa chama chetu, tukaanza kupambana maendeleo yasipatikane, tukaanza chuki, hapana huko tusifike,” amesema.

Amewataka wadumishe amani, upendo na mshikamano ili uchaguzi huo utoe taswira ya uchaguzi unaofuata wa 2025.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa nchi amewataka wakulima kuongeza juhudi katika shughuli za kilimo kwa kuwa Serikali inahangaika kusaka masoko.

“Limeni masoko yapo, kama soko la nje halipo kwa wakati huo, Serikali nitanunua badala yake, itayahifadhi na baadaye itatafuta masoko,” amesema.

Kuhusu mradi wa daraja hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohammed Besta amesema Sh11.1 bilioni zimetumika kufanikisha shughuli hiyo.

Ameeleza fedha hizo zimetolewa na Serikali na hata rasilimali watu iliyotumika katika ujenzi huo inatoka nchini.

Kulingana na Besta, daraja hilo lipo katika barabara ya Mkoa na linaunganisha kati ya Singida, Simiyu, Mara na Arusha.

“Ujenzi wa mradi huu, ulisimamiwa na taasisi ya usimamizi wa ujenzi wa madaraja na barabara kutoka Tanroads inaitwa TECU,” amesema Besta.