ACT Wazalendo yajiimarisha Kigoma

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu leo ameanza ziara yake ya siku mbili mkoani wa Tabora baada ya jana kuhitimisha katika Mkoa wa Kigoma.

Akiwa mkoani Kigoma, bosi huyo wa ACT Wazalendo amefanya ziara yake katika majimbo nane akiwa na viongozi wa kata 139, lengo likiwa ni kuimarisha uongozi ngazi ya matawi, kata, majimbo na mkoa, hivyo kuwa ta timu madhubuti.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa katika Mkoa wa Kigoma, chama chetu kinakuwa na mtandao na muundo imara kwa uongozi kuliko chama chochote cha siasa ikiwemo CCM,” anasema Shaibu.

Chama hicho kimeamua kujipanga mapema na kina malengo ya kuongoza kwa wingi wa viti vya uwakilishi katika chaguzi zijazo za serikali za mtaa zitakazofanyika 2024 na kuamini kuwa chaguzi hizo zitathibitisha Kigoma ni ya zambarau.

Pia amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa na wadau wa demokrasia kuhakikisha Tanzania inapata tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.

Kwa kuwa serikali imeshaahidi mara kadhaa kuanza kwa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya na sheria mpya ya uchaguzi ni muhimu serikali ije na kalenda ya utekelezaji.

“Hili la tume huru ni lazima likamilike mwaka 2023 ili uchaguzi ujao wa serikali za mitaa usimamiwe na tume huru badala ya Tamisemi,” anasema Shaibu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo amesema chama chao kitakuwa mstari wa mbele katika kuwasemea watanzania kupitia baraza kivuli la mawaziri, vyombo vya habari na mikutano ya hadhara, huku akidai kuwa Kigoma inautajiri wa maliasili lakini bado upo nyuma kiuchumi.

Amedai wananchi wa kigoma wanaongoza kupata changamoto zitokanazo utambuzi wa uraia wao huku akidai kuwa watu wa mkoa huo wana wana haki sawa na wananchi wengine katika mikoa mbalimbali Tanzania.

Kwa upande mwingine, Shaibu amewapokea madiwani na wagombea udiwani 11 kutoka vyama vya CCM, Chadema na NCCR Mageuzi na viongozi 62 wa ngazi mbalimbali kutoka vyama hivyo.

Baada ya kuwapokea wanachama hao wapya amesema chama kinapata faraja na kudai kwamba ACT Wazalendo kimekuwa ni kimbilio la wanasiasa kutoka vyama vingine.

“Tunawakaribisha wapambanaji wote waliochoshwa na vyama vyao vya siasa, na wote wanaotaka uendeshwaji wa siasa za hoja kwa maslahi ya wananchi, waifanye ACT Wazalendo kuwa chaguo lao,” amejinadi Katibu Mkuu huyo.