Kinana awaonya wanaojipitisha kabla ya 2025

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, awaonya wana-CCM wanaosaka nafasi za uongozi kupitia chama hicho, kusubiri mpaka muda wa uchaguzi utakapofika.

Hai. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, awaonya wana-CCM wanaosaka nafasi za uongozi kupitia chama hicho, kusubiri mpaka muda wa uchaguzi utakapofika.

Kufuatia kauli hiyo, Kinana ameziagiza kamati za siasa zikisaidiwa na zile za kanuni za maadili kufuatilia na kuchukua hatua kwa wote walioanza kuzunguka, wakitafuta uungwaji mkono kwenye nafasi za ubunge, udiwani, mwenyekiti wa mtaa na kitongoji.

Kinana ameyasema hayo jana, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa miaka miwili katika jimbo la Hai, ambayo imewasilishwa na Mbunge jimbo hilo, Saashisha Mafuwe.

"Nampongeza sana Mbunge kwa kazi nzuri sana anazozifanya, mbunge mnaye na anafanya kazi nzuri sana ya ubunge, ameanza ubunge na umri mdogo, shikamaneni naye mtaenda mbali sana,"

"Nitumie nafasi hii kuzungumzia wale wanaotafuta ubunge Mkoa wa Kilimanjaro lakini kwenye majimbo yote na kata zote chama chetu kina utaratibu mzuri sana,

"...wale wana-CCM wanaotaka kugombea kuanzia urais, ubunge, udiwani uwenyekiti wa kijiji na Serikali za mitaa...kuna kanuni inaitwa kanuni ya maadili ya Chama Cha Mapinduzi, kanuni zote hizi zinasimamia uchaguzi ndani ya CCM na ndani ya Serikali,"

"Huruhusiwi kutafuta uongozi ndani ya CCM na Serikali wakati waliochaguliwa wapo na wanafanya kazi, mwana-CCM yoyote anayetafuta uongozi wakati huu anavunja kanuni hizi nne, "amesema Kinana na kuongeza kuwa;

"Nataka nitumie fursa hii kuiagiza kamati za siasa zikisaidiwa na kamati za maadili nchi nzima, kuwafuatilia wale ambao wameanza kuzunguka zunguka na kutafuta ubunge, udiwani, uwenyekiti wa mtaa au kitongoji kuanzia sasa nawaonya."

Kinana ameziagiza kamati za maadili za mkoa na wilaya na zile za siasa kuwachukulia hatua kwa kadri inavyotakiwa na kanuni za maadili za uchaguzi ndani ya vyombo vya serikali.

Amesema ili mwanachama ateuliwe kuna vigezo vingi vinatizamwa, kura anazopata mgombea ni mojawapo, huku mambo mengine yanayoangaziwa ni pamoja na utoaji rushwa, kuanza kampeni kabla ya muda, na kama mgombea aliwachafua wenzake.

"Kwa hiyo unaweza kuwa wa kwanza lakini wakati wa uteuzi ukawa wa mwisho, sasa niwatahadharishe wale wenye kutafuta uongozi, subirini mpaka wakati utakapofika...nadhani mmenielewa vizuri kwa niaba ya wana-CCM wengine," amesistiza.

"Tunaishukuru Serikali yetu chini ya mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za kutekeleza miradi mbalimbali katika jimbo letu la Hai, ambapo kwa kipindi cha mwaka 2020/21 na  mwaka 2022/23 ambapo tumeweza kupata zaidi ya Sh39.4 bilioni," amesema Mbunge Mafuwe.