Haki za binadamu zilizovunjwa zaidi 2023

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2023 haki ya kuishi, uhuru dhidi ya vurugu, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya uhuru na usalama binafsi ndizo haki za binadamu zilizokiukwa zaidi, huku mikoa saba ikiwa vinara kwa ukiukwaji huo



Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema 2023 ni mwaka ambao uzingatiwaji wa haki za binadamu ulidorora ikilinganishwa na mwaka 2022.

Msingi wa tathmini hiyo ya LHRC, ni utafiti wa haki za binadamu wa mwaka 2023 ilioufanya katika mikoa 20 ya Tanzania bara na mikoa yote ya Zanzibar.

Hali hiyo kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo, ilichagizwa na kuendelea kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo ukatili dhidi ya wanaume, wazee, watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2023 haki ya kuishi, uhuru dhidi ya vurugu, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya uhuru na usalama binafsi ndizo haki za binadamu zilizokiukwa zaidi, huku mikoa saba ikiwa vinara kwa ukiukwaji huo.

Mikoa hiyo ni, Dar es Salaam, Njombe, Geita, Arusha, Kilimanjaro, Mara, Kigoma na Dodoma.

Katika ripoti hiyo, vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume vimeongezeka na kufikia asilimia 10 mwaka 2023 kutoka asilimia sita ya mwaka 2022.

Wazee nao walikatiliwa zaidi mwaka jana hadi kufikia asilimia 12, kutoka asilimia 10 ya mwaka 2022 kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Hali imebaki kuwa mbaya kwa ukatili dhidi ya watoto ambao ni asilimia 45, ukipungua kutoka asilimia 47 ya mwaka 2022, huku wanawake wakifikia asilimia 30 kutoka 33 ya mwaka 2022.

Ripoti hiyo inaeleza watu wenye ulemavu waliokumbana na ukatili mwaka 2023 ni asilimia tatu, kutoka asilimia nne ya mwaka 2022.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaweka wazi haki ya kuishi iliendelea kukiukwa mwaka 2023 kutokana na vitendo mbalimbali, ikiwamo mauaji ya watu wasio na hatia, hukumu za vifo, ajali za barabarani, mauaji ya wenza na kutoweka.

“LHRC ilirekodi matukio 42 ya unyanyasaji wa makundi, ambayo ni mawili zaidi ya yale yaliyorekodiwa mwaka 2022,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kadhalika, ripoti hiyo inabainisha hukumu 37 za vifo zilitolewa na Mahakama Kuu nchini, kati ya hizo wanaume ni asilimia 94.

Kwa upande wa mauaji ya wenza, ripoti hiyo imetaja matukio 50 ya waliouana, ikiwa kuna matukio 17 zaidi ya yaliyoripotiwa mwaka 2022.

Katika matukio hayo ya mwaka 2023, kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 90 ya waathirika ni wanawake na wanaume ni asilimia 10.

“Bado mwaka 2023 hakukuwa na majibu kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali juu ya watu waliopotea kwa miaka saba iliyopita, akiwamo mwandishi wa habari, Azory Gwanda,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Licha ya juhudi zilizofanywa katika kupunguza ajali za barabarani, ripoti hiyo inabainisha zaidi ya watu 500 wanaendelea kupoteza maisha kila mwaka kwa ajali hizo.

Mara nyingi matukio hayo huchagizwa na mwendokasi, ulevi wakati wa kuendesha, kufeli kwa breki na mambo mengine.

Uhuru wa kujieleza nao, umeendelea kuwa tatizo kwa mujibu wa ripoti hiyo, ikielezwa matukio mawili yaliripotiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Arusha.

“Pamoja na wanahabari kuwa na furaha na mwenendo wa uongozi wa vyombo vya habari, wamesisitiza kwamba ni vigumu kupata uhuru kamili bila mabadiliko ya kisheria,” inaeleza ripoti hiyo.


Usawa mbele ya sheria

Asilimia 78 ya wananchi waliofikiwa katika utafiti huo, wameeleza rushwa ndicho kikwazo kikubwa cha kupata haki, huku asilimia 49 wakitaja kesi kukaa muda mrefu, asilimia 48 wametaja uelewa mdogo wa sheria na asilimia 39 ni gharama za kupata uwakilishi mahakamani.

Bado mamlaka za haki jinai zimetajwa kutumia nguvu zaidi zinapomhitaji mtuhumiwa, huku rushwa nayo ikiendelea kuwa mwiba.

Matukio ya kujichukulia sheria mkononi yaliongezeka kwa Julai 2022 hadi Mei 2023 na kufikia 45,455.

“Wivu, imani za kishirikina, mirathi hasa ya ardhi ndizo sababu za hatua hizo,” inaeleza ripoti hiyo.

Matukio ya vitisho pia, yaliongezeka mwaka 2023 na kufikia 57, kutoka 44 ya mwaka 2022.

Ripoti hiyo, nimebaini upungufu wa asilimia 50 ya wafanyakazi katika sekta ya afya na hata bajeti katika sekta hiyo bado haijafikia viwango stahiki, licha ya kuongezeka kwa asilimia 15.

Katika utafiti huo, asilimia 39 ya wazee wamelalamikia hatua ya watoto wao kuwaachia mzigo wa kuwalea wajukuu.

Utafiti huo wa LHRC kuhusu rushwa unashabihiana na kile alichokisema hivi karibuni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kuwa licha ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuonesha mafanikio kwa mwaka 2022/23, lakini hali ya rushwa ni mbaya.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, mapema mwezi huu, Jaji Warioba alisema anaamini hali ya rushwa sasa ni mbaya, akisisitiza hakuna haja ya kwenda mbali zaidi katika maeneo yenye rushwa, kwani ukiwauliza wananchi wa kawaida hivi siku hizi kwenye huduma za afya, polisi, Mahakama hakuna rushwa, au Tanesco, ardhi, hakuna rushwa? (akimaanisha utapata majibu) pamoja na taarifa ya CAG, tunaona upotevu wa fedha katika Serikali ni mkubwa, mimi nadhani tusiwe tunasema Tanzania rushwa imepungua, hapana, ukienda kwa wananchi matatizo yao ni makubwa, nafikiri bado Takukuru hawajafanya kazi ya kutosha kuelimisha wananchi kwenye hili.”

Jaji Warioba alikuwa akijenga hoja juu ya ripoti ya Takukuru iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Salum Hamduni kuonesha mafanikio makubwa waliyoyapata kwa mwaka 2022/23.


Mapendekezo

Kutokana na yote yaliyobainika, LHRC inapendekeza maboresho ya kisera na kisheria katika mifumo ya haki jinai na mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, mapendekezo ya LHRC yanashabihiana na kile kilichopendekezwa na Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Othman Chande.

Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuangalia na kupendekeza marekebisho ya mifumo na taasisi za haki jinai, ilipendekeza mabadiliko ya kisheria kuwa hatua madhubuti ya kufanikisha hilo.

Msisitizo wa mapendekezo ya tume hiyo, ulijikita kwenye maboresho ya kisera na kisheria, kama hatua ya kukabiliana na changamoto katika mifumo ya haki jinai.


Alichokisema Henga

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema jambo zuri ndani ya utafiti huo kwa mwaka 2023 hakuna tukio la mauaji ya albino lililobainika.

Pamoja na hali hiyo, alisema ni muhimu elimu ikaendelea kutolewa kwa kuwa matukio hayo mara nyingi hutokea katika kipindi ambacho uchaguzi unakaribia.

“Kwa sababu tunakaribia uchaguzi hatuna budi kutoa elimu, maana kipindi kama hiki ndipo matukio ya mauaji ya albino hutokea, wapo watu wanaodhani ushindi wa uchaguzi unatokana na uhai wa mtu,” alisisitiza.

Mtafiti Mwandamizi wa LHRC aliyesimamia utafiti huo, Fundikira Wazambi alisema matukio yaliyobainishwa yana athari kwa watu binafsi na uchumi wa nchi.

Alisema kuendelea kutokea kwa matukio hayo, kunasababishwa na kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote.

"Wapo wanaoshuhudia matukio lakini hawataki au wanaogopa kuripoti katika Mamlaka zinazohusika, mimi nimewahi kushuhudia kiongozi anaogopa kuripoti," alisema.

Rushwa nayo ni sababu nyingine ya kuendelea kwa vitendo hivyo, kwa mujibu wa Fundikira.

Alisema wapo wanaofanya matukio hayo kisha wakawahonga wazazi wa mwathirika ili akafute kesi mahakamani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe alipozungumza na gazeti hili kuhusu ripoti hiyo alisema kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo ya kisheria ndiyo suluhu ya changamoto zote zilizobainishwa katika ripoti hiyo.

Alisema mabadiliko hayo, yataimarisha taasisi zitakazosimamia uwajibikaji na ufanisi. Alieleza mabadiliko hayo yanapaswa kuwa ya Katiba kwa kuwa ndiyo sheria mama itakayofanikisha hayo.

“Mifumo yetu ni rotten na hamna uwajibikaji, ndiyo maana haki za binadamu haziachi kukanyagwa kila leo,” alisema Wangwe.