Haki tano za binadamu zinazoongozwa kuvunjwa Tanzania

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga

Muktasari:

  • Ripoti ya haki za binadamu 2022 imezinduliwa huku ikionyesha matukio ya ukatili dhidi ya watoto yakizidi kuongezeka nchini kwa asilimia 47.

Dar es Salaam. Ripoti ya hali ya haki za binadamu inaonyesha kwa mwaka 2022 haki tano zimeongoza kwa kuvunjwa zaidi nchini ikilinganishwa na haki zingine.

Kulingana na ripoti hiyo iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) haki zilizovunjwa zaidi ni haki ya kuishi, uhuru dhidi ya ukatili, haki ya usawa mbele ya sheria, haki ya kuwa huru na salama, na haki ya elimu.

Akizungumza leo Aprili 12, 2023 wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesema tathmini inaonyesha watoto walikuwa ni wahanga wakuu wa vitendo vya ukatili kwa asilimia 47, wakifuatiwa na wanawake kwa asilimia 33 na wazee asilimia 10.

Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yameendelea kuwa mwiba kwa haki ya kuishi, ambapo kwa mwaka huu LHRC imekusanya matukio 40, ambayo ni 18 zaidi ukilinganisha na mwaka 2021.

Kulingana na ripoti hiyo matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina yamepungua, lakini bado ni changamoto, hasa kwa wanawake, ambao walikuwa ni 52% ya wahanga.

Ripoti pia inaonyesha kuibuka upya kwa mashambulio na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (ualbino) na mwaka 2022 lilitokea tukio jingine la mauaji ya mtu mwenye ulemavu huo mkoani Mwanza, ambaye alifariki baada ya kukatwa mkono.

Kwa upande wa uhuru wa kujieleza, bado kuna sheria mbalimbali ambazo zina vifungu vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

“Wadau mbalimbali wamekuwa wakipiga kelele sheria hizi kurekebishwa ili kulinda uhuru wa kujieleza. Hata hivyo, tunaipongeza Serikali kwa kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, ikiwemo kwa kuvifungulia vyombo vinne vya habari vilivyokuwa vimefungiwa.

“Tunafurahi pia kuondolewa kwa katazo la mikutano ya kisaisa ya hadhara hivi karibuni, ambalo lilikuwa linakiuka uhuru wa kujumuika na kukuanyika kwa muda mrefu, ikiwemo mwaka 2022,” amesema Anna.

Mtafiti mkuu katika rpoti hiyo Fundikira Wazambi amesema haki ya usawa mbele ya sheria imeandelea kuwa mojawapo ya haki zinazokiukwa zaidi kwa sababu ya vikwazo mbalimbali vya upatikanaji haki na changamoto katika mfumo wa haki jinai.

“Mojawapo ya vikwazo vikubwa vya upatikanaji haki kwa mtazamo wa wanajamii ni rushwa (82%), ikifuatiwa na kesi kuchukua muda mrefu na uelewa mdogo kuhusu sheria (54%).” Amesema Wazambi.