Rais Samia kufungua kikao cha haki za binadamu Afrika

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Kikao hicho cha siku 20,kinatarajiwa kufanyika Arusha ambapo pamoja na masuala mengine kitajadili hali ya haki za binadamu barani Afrika,taarifa za wanaharakati wa haki za binadamu,msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki Tanzania na maadhimisho ya siku ya haki za kibinadamu Afrika kwa kuzingatia itifaki ya Maputo.

Arusha. Wadau zaidi ya 700 kutoka mataifa mbalimbali, wanatarajiwa kushiriki kikao cha 77 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu, kitakachofanyika kuanzia Oktoba 20 hadi Novemba 9, 2023 jijini Arusha.

 Kikao hicho cha siku 20 kitakachofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) kitafunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Oktoba 20.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Oktoba 7, 2023 na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana, wakati katika akizungumza katika kikao cha mawaziri kujadili maandalizi ya kikao hicho.

Balozi Chana amesema kikao hicho cha kawaida cha Kamisheni hiyo, kitajadili masuala mbalimbali ikiwemo hali ya haki za binadamu barani Afrika, taarifa za wanaharakati wa haki za binadamu, na msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki Tanzania.

Aidha, kwa mujibu wa Waziri huyo mwenye dhamana ya sheria nchini, pia katika kikao hicho, kutafanyika uzinduzi wa nyaraka mbalimbali za kamisheni hiyo na maadhimisho ya siku ya haki za kibinadamu Afrika kwa kuzingatia itifaki ya Maputo.

"Kikao hicho cha kawaida kinatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 700 kutoka mataifa mbalimbali na kitafunguliwa na Rais Samia ambapo mbali na kujadili masuala ya msingi yanayohusu haki za binadamu na watu, tutapata fursa siyo tu ya kubadilishana uzoefu wa masuala ya haki za binadamu na watu,” amesema Balozi Chana na kuongeza;

“...pia tutatumia fursa ya kikao hicho kuitangaza nchi kwa mataifa mbalimbali juu ya utajiri na rasilimali tulizonazo hapa nchini, kuonesha vivutio na maeneo ya utalii ili kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi kwenye nchi yetu.”

Amesema kuwa awali Januari 31, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Kamishna Remy Ngoy Lumbu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), alimtembelea Rais Samia na kuomba Serikali ya Tanzania iwe mwenyeji wa kikao hicho, ombi ambalo liliridhiwa.

Amesema Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu inapaswa kutekeleza majukumu makuu matatu ambayo ni kulinda na kukuza haki za binadamu na watu, lakini pia kutoa tafsiri ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

“Wizara ya Katiba na Sheria kama Wizara yenye kuratibu na kusimamia masuala ya haki za binadamu na watu nchini, inaendelea na maandalizi ya kikao hicho ambacho kitahusisha sekta mbalimbali zaidi ya masuala ya haki za binadamu na watu,” amesema.

Sekta hivyo ni pamoja zile zinazohusiana na masuala ya ushirikiano wa kimataifa, utamaduni, sanaa na michezo, fedha na uchumi, ulinzi na usalama, afya, lakini pia zile zihusuzo mambo ya habari na mawasiliano.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka wizara hiyo, Dk Khatibu Kazungu, amesema moja ya masuala inajivunia ni pamoja na kampeni ya msaada wa kisheria inayoitwa Mama Samia Legal aid.

Kampeni hiyo ambayo kimsingi imeanza kutekelezwa mwaka huu, imejikita katika kutoa elimu ya kisheria na msaada wa kisheria kwa wananchi katika masuala mbalimbali, na kwamba inatekelezwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na asasi za kiraia na wadau wengine.

“Lengo la kampeni hii ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki wa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini, tunajivunia kwa kuwa imeweza kusaidia watu wengi katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Naibu huyo.