Dk Mpango anadi fursa za uwekezaji za Tanzania 

Muktasari:

  •  Asema yupo tayari kumsikiliza mwekezaji yeyote endapo atakwama katika ngazi za chini.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaita wawekezaji wa kimataifa kuwekeza Tanzania, akisema kuna utulivu, sera nzuri, jiografia na mazingira wezeshi kuwawezesha kufanya shughuli zao.

Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 27, 2024 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufunga kongamano la uwekezaji kati ya Tanzania na China. Jukwaa hilo linatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na China, pia kukuza ushirikiano.

Dk Mpango amesema Serikali na viongozi wakuu wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili kufikia malengo ya uwekezaji Tanzania.

Amesema yupo tayari kumsikiliza mwekezaji yeyote endapo atakwama katika ngazi za chini.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, Rais Samia ametoa onyo kali kwa watendaji wa Serikali watakaoonekana kutokuwa na kasi katika kukamilisha michakato ya uwekezaji.

“Uongozi wa juu wa nchi uko tayari kumpokea na kumsikiliza mwekezaji yeyote anayekabiliwa na vikwazo serikalini,” amesema.

Dk Mpango amewataka wawekezaji wa China kufanya uwekezaji katika kuelekea matumizi ya teknolojia ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.

“Eneo lingine linalowezekana kwa uwekezaji ni uvunaji wa rasilimali za uchumi wa buluu katika Bahari ya Hindi na maziwa makuu (Victoria, Tanganyika, Nyasa na Rukwa). Fursa zilizopo ni uvuvi na usindikaji unaohusiana, uchunguzi wa madini, utalii wa pwani na baharini na usafirishaji,” amesema.

Kuhusu jukwaa hilo, Dk Mpango amezipongeza kampuni kutoka China kushiriki, akisema kupitia kongamano hilo wafanyabiashara wa Tanzania na Taifa hilo wanapata fursa ya kubadilishana taarifa.

“Kumekuwa na ongezeko la wawekezaji kutoka China kuja nchini, hii inaonyesha Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji, pia utekelezaji wa sera mbalimbali umechangia Taifa hili kuwa sehemu nzuri ya kuwekeza,” amesema na kuongeza:

“Rais Samia amekuwa kinara katika kufungua uwekezaji kupitia 4R, (Falsafa za maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya Taifa) sambamba na mabadiliko ya sheria, sera na uwazi katika kupunguza urasimu. Hali hii imechangia kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.”


Balozi wa China nchini, Chen Mingjian amesema jukwaa la wawekezaji linalowakutanisha wafanyabiashara wa Taifa lake na Tanzania linalenga kukuza biashara miongoni mwa mataifa hayo mawili.

Balozi Mingjian amesema Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Amesema tangu Rais Samia kushika madaraka mwaka 2021, ameonyesha juhudi kubwa katika sekta mbalimbali za nishati na usafirishaji.

“Tuna furaha kuona mradi wa Bwawa la Julius Nyerere umeanza kufanya kazi, hii itasaidia kuleta kasi ya ukuaji wa uchumi. Mabadiliko chanya ya hivi karibuni yamesaidia kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi. Tanzania na China ni marafiki kwa miaka 60 sasa,” amesema.

Gilead Teri, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), walioandaa jukwaa hilo kwa ushirikiano na sekta binafsi za Tanzania na China, amesema kituo hicho kipo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji.


Umuhimu wa jukwaa

Jukwaa hilo linatoa nafasi kwa wafanyabiashara, wawekezaji wa Tanzania na China kujadili fursa za uwekezaji, kubadilishana taarifa na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza uwekezaji, hivyo kukuza uchumi.

Pia, linajenga uelewa bora kuhusu mazingira ya biashara na uwekezaji ya kila nchi, hivyo kuvutia na kurahisisha uwekezaji.

Mbali na hayo, linawasaidia Watanzania kuongeza mbinu na ujuzi katika kuibua fursa mpya, kudumisha biashara baina ya kampuni ndogo na kubwa, kujua namna ya kupata taarifa sahihi za kibiashara kutoka China.

Katika jukwaa hilo imeshuhudiwa utiaji saini wa Makubaliano ya Mashirikiano (MoUs) kati ya China na Tanzania yanayojumuisha mashirikiano, kukuza uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya nchi hizo mbili.

MoU ya kwanza ni kati ya Baraza la China la Kukuza Uwekezaji na Biashara (CCPIT) na TIC, inayolenga kukuza na kurahisisha uwekezaji kati ya Jiji la Jinhua, Zhejiang, na Tanzania.

Makubaliano mengine yanahusisha Kampuni ya Zhejiang Sifang Group Ltd katika ushirikiano unaolenga maendeleo ya kilimo kupitia ushirikiano wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Vijijini IRDP ili kuendeleza mashine za kilimo.

Mengine ni Kampuni ya Zhejiang Sifang Group Ltd na kampuni ya Initiator Eastern Group Company Limited kuanzisha chapa ya pamoja kwa soko la Tanzania.