Dk Mpango kuiwakilisha Tanzania Jukwaa la Uchumi

Vice President Dr Phillip Mpango speaks at the launch of the Tanzania International Cashew Conference in Dar es Salaam on October 11, 2023.

Muktasari:

  • Tanzania inatarajia kushiriki mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unalolenga kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo uchumi, uwekezaji na mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajia kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) utakaofanyika kuanzia kesho hadi Januari 19, mwaka huu.

Katika mkutano huo utakaofanyika nchini Uswisi, Dk Mpango atashiriki akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Taarifa ya safari ya Dk Mpango imetolewa leo, Jumapili Januari 14, 2024 na kutiwa saini na msaidizi wake wa habari, Franco Singaile.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk Mpango anatarajiwa kuhudhuria mikutano mbalimbali katika jukwaa hilo, ikiwemo inayohusu uchumi, uwekezaji na utawala bora.

Mikutano mingine atakayohudhuria katika jukwaa hilo ni kilimo, usalama wa chakula na mabadiliko ya tabianchi. Kadhalika kiongozi huyo atafanya mazungumzo na viongozi wa mataifa na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Wengine atakaofanya nao mazungumzo ni watendaji wakuu wa mashirika ya kimataifa, wakuu wa taasisi na kampuni, na wafanyabiashara.

Jukwaa la Uchumi Duniani ni shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma na hufanyika karibu kila mwishoni mwa Januari.

Mikutano hiyo inawakutanisha wakuu wa mataifa mbalimbali duniani, wanauchumi na wafanyabiashara.

Kaulimbiu ya jukwaa hilo mwaka huu ni ‘Kujenga upya uaminifu’ ikilenga kurejesha imani kwa wakati ujao, ndani ya jamii na miongoni mwa mataifa.

Tanzania inakwenda kushiriki jukwaa hilo, ikiwa na rekodi ya kuimarika kiuchumi , ikiwa pato lake limekua na kufikia Sh200 trilioni mwaka 2023, kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Ongezeko hilo ni kutoka Sh163.5 trilioni mwaka 2021 na upo uwezekano wa pato hilo kuongezeka na kufikia Sh276 trilioni mwaka 2028.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, tayari Tanzania ilishaweka msimamo wa mambo manne katika mkutano wa jukwaa la mabadiliko ya tabianchi uliofanyika Misri mwishoni mwa mwaka jana.

Msimamo huo ni kupatikana kwa fedha za ufadhili kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi, kuanzishwa mfuko wa pamoja wa majanga na maafa kufidia waathirika wa mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya nishati safi na jumuishi, na mjadala wa jinsia unaompa mwanamke kipaumbele.

Katika eneo la uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeweka wazi kuwa, Tanzania imesajili miradi 504 yenye thamani ya Sh10 trilioni kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 100 ikilinganishwa na miradi 132 iliyosajiliwa mwaka 2022