Dk Mpango atoa angalizo makusanyo ya kodi

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kodi la Uwekezaji 2024 lililofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 27, 2024

Muktasari:

  • Azungumzia maboresho ya sera, sheria na usimamizi wa mifumo ya kodi.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ni vyema kuwapo mikakati itakayosaidia kukuza ukusanyaji wa kodi hadi kufikia asilimia 15 ya Pato la Taifa kwa mwaka au zaidi.

 Ametaka mikakati hiyo, kwani ndani ya muongo mmoja kati ya mwaka 2010/2011 hadi 2022/2023 makusanyo ya kodi yamekuwa chini ya asilimia 12 ya Pato la Taifa, kiwango ambacho ni chini ya asilimia 15.6 kilichowekwa kwa nchi za Afrika.

Ametoa kauli hiyo jana Jumanne, Februari 27, 2024 katika uzinduzi wa jukwaa la kodi na uwekezaji kwa mwaka 2024 lililolenga kujadili maboresho ya sera katika uwekezaji, ukusanyaji wa mapato ya ndani na ukuaji wa uchumi jumuishi.

"Nchi nyingine ambazo Tanzania iko nazo katika kundi moja ya kipato cha kati cha chini ziko juu ya asilimia 13, mfano Senegal ina asilimia 18.7, Ghana ina asilimia 14.1, Cameroon asilimia 13.3," amesema Dk Mpango.

Amesema katika kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Sita tangu iingie madarakani imeendelea kufanya maboresho ya sera, sheria na usimamizi wa mifumo ya kodi, ili kujibu malalamiko ya wawekezaji.

"Tumemsikia Profesa Kitila Mkumbo amesema katika kipindi kifupi cha utawala wa Rais Samia yamefanyika maboresho 460 ambayo ni sawa na asilimia 80 ya maboresho yaliyofanyika ndani ya muda mfupi,” amesema Dk Mpango.

Miongoni mwa maboresho hayo, amesema ni kurekebisha sheria za kodi ili kutoa vivutio kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa kimkakati chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuweka utulivu wa sera za kodi ambao viwango vya ushuru wa bidhaa hufanyiwa marekebisho kila baada ya miaka mitatu badala ya kila mwaka.

Pia ametaja kuendelea kujenga na kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara ikiwemo vituo 10 vya utoaji huduma kwa pamoja mipakani, sita vinafanya kazi na vilivyobaki vinamalizia ujenzi na uwekaji wa mifumo ya Tehama.

"Pia tumefanya mapitio na kuhuisha sera na sheria, ili kuweka misingi mizuri na imara ya kusimamia mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji," amesema Dk Mpango.

Amesema pia kuainisha majukumu ya kitaasisi, ili kurahisisha utoaji wa huduma na kufanya mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara (TNBC).

Mengine amesema ni kutoa misamaha ya kodi kwa kiwango cha asilimia sifuri cha ushuru wa forodha kwa bidhaa za mtaji na malighafi, zana za kilimo, ufugaji na uvuvi, dawa za binadamu na mifugo, vifaa vinavyotumika kuunganisha mitambo ya magari na malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za dawa.

Baadhi ya viongozi wakishiriki uzinduzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji 2024 lililofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 27, 2024

Amesema kutokana na hayo, mazingira ya ufanyaji biashara nchini yameimarika katika uongozi wa Rais Samia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi inayokuwa kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara, licha ya misukosuko ya uchumi inayoendelea duniani.

Kwa mujibu wa takwimu za TIC, miradi 526 yenye thamani ya Sh14.586 trilioni (Dola 5.72 bilioni) ilisajiliwa mwaka 2023 ikilinganishwa na miradi 256 yenye thamani ya Sh9.559 trilioni (Dola 3.749 bilioni) mwaka 2021.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za TIC, miradi hiyo ilikuwa ya sekta za uzalishaji, ujenzi wa majengo ya biashara, usafirishaji na kilimo.

Hata hivyo, Dk Mpango amesema mfumo wa kodi umekuwa kikwazo katika uwekezaji na ufanyaji biashara, jambo ambalo linathibitishwa kutokana na kuwapo kwa malalamiko dhidi ya mfumo wa kodi kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa nje na ndani.

Amesema hata kupitia TNBC, wafanyabiashara na wawekezaji wamekuwa wakilalamikia utitiri wa kodi, tozo na ada, sera za kodi zisizotabirika, viwango vya juu vya kodi, rushwa, makadirio ya kodi yasiyoakisi uhalisia, kutosomana kwa mifumo ya kielektroniki hasa taasisi za utoaji vibali, leseni na huduma nyingine, mwingiliano wa majukumu ya kitaasisi.

"Serikali nayo kwa upande wake imekuwa ikilalamikia kutozingatiwa kwa sheria na miongozo ya kodi na ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji,” amesema.

Amesema Serikali imekuwa ikitoza kodi na kutafuta mikopo na misaada kwa ajili ya kugharimia uendeshaji wa Serikali na utekelezaji miradi ya maendeleo, akieleza katika hali hiyo kodi isipolipwa ipasavyo inadhoofisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake kwa umma.

"Hivyo Serikali ina jukumu la kuweka mazingira bora ya kuwezesha uwekezaji na ufanyaji biashara kushamiri na kuwezesha walipakodi kutekeleza wajibu wao kisheria," amesema Dk Mpango.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema uchambuzi wa taarifa ya utekelezaji wa mkakati wa kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa miaka mitano kati ya mwaka 2019 hadi 2023 inaonyesha mabadiliko na maboresho ya kisera, kisheria, kikanuni yanayohusu kodi na yasiyohusu kodi katika maeneo 665.

“Katika maboresho hayo, 416 yalilenga kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini. Pia katika maboresho yote haya 460 kati ya 665 yamefanyika kati ya mwaka 2021 hadi 2023, kama msukumo wa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara kwa uchambuzi tuliofanya, nchi yetu kwa sasa iko katika mazingira mazuri zaidi katika historia ya nchi hii,” amesema Profesa Mkumbo.

Akizungumzia namna wanavyoshughulikia malalamiko ya kodi, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesena kulikuwa na malalamiko juu ya ukadiriaji wa kodi na utaratibu usio rafiki wa kushughulikia migogoro ya kikodi, jambo ambalo sasa limepatiwa ufumbuzi.

"TRA inakamilisha kujenga mfumo wa kodi ya forodha ambao utahusisha mtiririko mzima wa bidhaa na hivyo kujenga ukadiriaji ambao uko rasmi na wanaendelea kujenga mfumo wa kodi za ndani ambao na wenyewe utapunguza matatizo yalikuwa yanalalamikiwa,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu malalamiko ya migogoro ya kikodi, amesema tayari ofisi ya msuluhishi wa migogoro hiyo imeshazinduliwa na kuanza kazi, jambo ambalo litapunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga alipowasilisha maoni ya taasisi yake ametaka wigo wa ulipaji kodi kutanuliwa.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza moja ya changamoto inayoukumba mfumo wa kodi ni sehemu za makusanyo kuwa chache na mara nyingi ndiyo hizohizo zinatolewa macho kuongezwa kodi.

“Mfano asilimia 80 ya mapato ya ndani ya kodi hukusanywa kutoka kwa walipa kodi 400 wakubwa. Sehemu kubwa iliyobaki ya walipakodi huchangia asilimia 20,” amesema Maganga.

Amesema watu wengi walio katika mwanya wa kuchangia kwenye ulipaji kodi ni kundi lisilo rasmi, hivyo ni vyema kuhakikisha kwenye sekta rasmi kunavutia kuliko kubaki kwenye sekta isiyo rasmi.

“Tuangalie jinsi ya kuwapunguzia mahitaji ya wao kuwa rasmi, tuwapunguzie na kodi ili waingie kwenye mfumo rasmi," amesema Maganga.