Vijana sita mbaroni Z’bar tuhuma za wizi, kushambulia

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Richard Thadei Mchonvu akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja visiwani Zanzibar, linawashikilia vijana sita wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 15-18 kwa tuhuma tofauti zikiwemo kushambulia wananchi kwa kutumia silaha za jadi.

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja visiwani Zanzibar, limesema halitoacha kufanya msako wa vijana waliotekeleza matukio ya wizi na kushambulia wananchi ili liwakamate na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Januari 2, 2024 na  Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Richard Thadei Mchonvu wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema msako walioufanya katika maeneo mbalimbali umesaidia kuwakamata vijana sita na wataendelea nao ili kukomesha vitendo vya kihalifu.

Mchomvu amesema usiku wa Desemba 30, 2023 vijana wanaokadiriwa kuwa 15 walivamia makazi ya watu eneo la Dole na Mwanyanya na kuvunja nyumba kisha  kuwashambulia watu kwa mapanga na kuwajeruhi huku wengine wakilazwa hospitali.

Kamanda huyo amesema watu hao waliiba simu 18 za aina tofauti na Sh85,000 walizozikuta kwenye nyumbani walizovamia.

Katika hatua nyingine, kamanda huyo amesema wanaendelea na msako zaidi kuwabaini wengine ambao wamehusika na tukio hilo akiamini bado wapo.

“Nataka niseme kila aliyehusika kwenye tukio hili atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili achukuliwe hatua za kisheria,’’ amesema.