Dk Salmin alivyoiacha Zanzibar na Dira ya 2020

Dk Salmin Amour Juma ‘Komandoo’.

Dodoma. Jana tuliangalia namna Dk Salmin Amour Juma ‘Komandoo’ alivyo onja shubiri baada ya kuibuka hoja ya kuondoa ukomo wa kugombea kwenye Katiba ya Zanzibar, ili aweze kugombea urais kwa mara ya tatu.

Leo katika makala ya mwisho kuhusukiongozi huyo na uongozi wake, tunaangalia namna alivyowaachia Wanzanzibari Dira ya Maendeleo ya Zanzibar mwaka 2020.

Dk Salmin Amour pamoja na misukosuko ya kisiasa ndiye Rais wa kwanza wa Zanzibar aliyeweka dira ya maendeleo aliyoiita ‘Gari la matumaini katika safari ya maendeleo.’

Dk Salmin hakutaka kuiacha Zanzibar ikiwa haina mipango ya maendeleo ya muda mrefu na Januari 2000, miezi michache kabla ya kipindi chake cha pili cha uongozi kumalizika, alizindua Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020.

“Serikali ya Zanzibar imepanga Dira ya 2020 kama gari la matumaini litakalotubeba salama katika safari hii ya maendeleo,” ilikuwa ni kauli ya Dk Salmin wakati wa uzinduzi wa dira hiyo, Januari mwaka 2000.

Wakati huo Dk Salmin alieleza sababu za kuandaa dira hiyo, kuwa ni kwa sababu dunia imebadilika katika mambo mengi yakiwamo ya kiuchumi, kijamii, uhusiano wa kimataifa na maendeleo ya teknolojia.

Utabiri wa kiuchumi na kisayansi kwa wakati huo ulionyesha dunia itakuwa kijiji kidogo kinachoendeshwa kwa msingi wa ushindani kwa ajili ya kuimarisha ufanisi wa kiuchumi, biashara na maendeleo ya kiteknolojia.

Kwa mujibu wa Dk Salmin, mataifa madogo yanayoendelea kama ya Zanzibar yalikuwa yanahitaji kuwa macho na ufanisi zaidi ikibidi yanufaike na mkokoteni mrefu wa maendeleo ya kimataifa.

Alisema kwa utambuzi huo, Serikali ya Zanzibar imepanga Dira ya 2020 kama gari la matumaini litakalowabeba Wazanzibari salama katika safari hii ya maendeleo.
 

Uchumi baada ya Mapinduzi

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, hali iliyokuwepo iliruhusu vyombo vya dola kukuza uchumi kwa mafanikio, hata hivyo kushuka kwa kasi kwa bei ya karafuu duniani kulifanya lengo hilo lishindwe kuendelezwa na kuanzia hapo Serikali haikuweza kutoa huduma za kijamii kwa kiwango cha kutosha.

Uwezo wa Serikali wa kuagiza chakula na mahitaji muhimu ya kijamii kutoka nje ulipunguza. Matumaini ya watu yalianza kupoteza mwelekeo.

 

Dira ya Maendeleo 2020

Dira iliyoachwa na Dk Salmin ililenga kuondoa upungufu wa mapato kati ya vikundi vya kijamii na kanda za kijiografia na kuongeza uwezo wa mtu binafsi kupata mahitaji muhimu ya maisha.

Pia, dira hiyo ililenga kujenga mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia unaoheshimu maoni mbalimbali, uwazi, uwajibikaji na hiyo yote ni dhidi ya mafisadi tabia, kutafuta kodi na kuondoa uonevu.

Mambo mengine yaliyoelezwa kwenye dira hiyo ni kujenga umoja wa kitaifa usio na tofauti zinazotokana na itikadi, dini, rangi au jinsia ili kuhakikisha watu wote wanajiamini, kujiheshimu na kuheshimiana.
Falsafa ya dira hiyo ya Dk Salmin ni gari ambalo lingeipeleka Zanzibar kwenye maendeleo na kwamba ili gari liende vizuri, inabidi limilikiwe na wananchi kupitia demokrasia na taasisi ya uwakilishi.

Dira hiyo pia ilieleza changamoto zilizokuwepo kwa wananchi ambazo Serikali ililenga kuziondoa, yaani kutokomeza umaskini uliokithiri na kuweka malengo ya Wazanzibari walio huru kutokana na umaskini ili waweze kushiriki kikamilifu mkondo wa maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Pia, dira hiyo iliweka malengo ya kuanzisha mfumo wa hifadhi ya jamii na vyandarua vingine vya usalama vinavyowalinda maskini, wenye ulemavu, wazee na makundi mengine yaliyo hatarini, ikiwamo kutoa fursa za ajira, elimu na mafunzo yatakayokuza maisha endelevu.

Dira pia iliweka mambo mengine makuu ya mkakati wa kuondoa umaskini ikiwamo kuanzisha sera zinazolenga kupunguza kukosekana wa usawa, kuongeza fursa za kuboresha na kutoa ufikiaji wa rasilimali na kuboresha hali ya mazingira maeneo ya vijijini Zanzibar.

Dira iliyoachwa na Dk Salmin pia iliweka misingi ya kutoa ulinzi wa kijamii kwa wale ambao hawawezi kujisaidia wenyewe; kutambua mahitaji na ujuzi wa wanawake, kuendeleza rasilimali watu, kuboresha miundombinu, ikiwa ni pamoja na mawasiliano vifaa na kuifanya ipatikane zaidi na kukuza sera za ndani kwa ajili ya kukidhi mahitaji muhimu ya watu wote wa Zanzibar.

Dira 2020 ilitokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali waliojumuisha wanaume na wanawake, wataalamu na wanasiasa na viongozi wa dini.

Dira ilikuwa ikisisitiza ustawi wa kiuchumi kwa watu wote. “Ni matumaini yetu kwamba itaangazia penye giza, ityaleta tumaini jipya palipokatishwa tamaa, itaongeza ushirikiano palipo na migawanyiko na kuwa kichocheo cha utulivu, usalama na upendo miongoni mwetu sote,” alisema Komandoo.

Kwa mujibu wa Dk Salmin, Dira ya 2020 vilevile iliweka lengo la kuipeleka Zanzibar katikati ya soko kama muuzaji na mnunuzi, huku ikiwa kama kituo muhimu cha biashara ya usafirishaji kati ya majirani zake wa kikanda.

Pia, Serikali ya Zanzibar iliongoza uundaji wa Dira ya 2020 kama njia ya kuondoa umaskini, janga ambalo limezikumba nchi kadhaa zinazoendelea duniani.

Dira ya 2020 ilieleza kuwa umaskini kwa kiasi kikubwa unachangiwa na kutojua kusoma na kuandika, ukosefu wa huduma bora za afya, maji safi na salama, nishati ya uhakika na ukosefu wa makazi bora.

Mwongozo uliokuwemo kwenye Dira ya 2020 ni kufanya kazi kwa bidii, amani na utulivu pamoja na mipango yenye malengo, kuwa hiyo ndiyo njia ya suluhisho sahihi kwa matatizo makubwa yanayowasumbua watu wengi katika nchi zinazoendelea.

Hayo ndiyo yalikuwa maono ya utawala wa Dk Salmin, suala la kujiuliza ni kwa kiasi gani malengo hayo yamefikiwa na matunda yake ni yapi.

Zanzibar kwa sasa ina Dira ya 2050 yenye la kuifanya Zanzibar iendelee zaidi na kufikia nchi ya kipato cha kati katika ngazi ya juu, na kwamba ifikapo mwaka 2050 kipato cha mwananchi kinatakiwa kufikia dola 4,400 (Sh11,022,000) kwa mwaka.