UBX: Mama wa upatanifu katika sekta ya kibenki Tanzania

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande (katikati) akitoa fedha kupitia ATM ya NMB waka­ti wa uzinduzi wa ushirikiano kati ya kampuni ya UBX na benki hiyo ambao unawezesha wateja kupata huduma kupitia mtandao wa ATM za Benki ya NMB nchini nzima kupitia mfumo wa upatanifu. Wanaoshuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya UBX, Sabasaba Moshingi (kulia).

Miaka ishirini iliyopita, mkazi wa Mufindi alilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta mashine ya ATM inayomilikiwa na benki yake ili aweze kutoa pesa. Leo hii, kama vingi vinavyotuzunguka, teknolojia imeendelea.

Mabenki yametengeneza mifumo inayowawezesha wateja kutoa hela kutoka ATM yoyote bila kujali kama inamilikiwa na benki ambayo mteja ameweka pesa zake au la. Kama unawaza jambo hili limewezekanaje, basi UBX ni jibu lako.

Kampuni hii ilipoanza mwaka 2000 kama Intrinsic Technology Tanzania Ltd (ITT), ilijihusisha na maswala ya software na mifumo mbalimbali ya kompyuta huku ikiwa na wateja pamoja na wafanyakazi wachache tu.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Benki ya NMB, Kampuni ya UBX na Umoja Switch (walioketi) wakati wa hafla ya uzinduzi wa ushirikiano kati ya kampuni ya UBX na Benki ya NMB ambao unawezesha wateja kupata huduma kupitia mtandao wa ATM za benki ya NMB nchini nzima kupitia mfumo wa upatanifu. Waliosimama ni viongozi na wawakilishi wa mabenki nchini.

Mwaka 2004, ilinunuliwa na kampuni kutoka Afrika Kusini na kuitwa Business Connexion Tanzania (BCX). Iliponunuliwa tena na kampuni ya Umoja Switch Company Limited (USC) mwaka 2021, ndipo ilipopata jina ambalo linalo sasa – UBX Tanzania Limited.

Hii imekuwa zaidi ya mlolongo wa majina mapya. Kwa zaidi ya miongo miwili ya kufanya kazi Tanzania, UBX imekuwa katika mstari wa mbele kubadilisha maisha ya watu kupitia teknolojia. Ikiwa imehudumia zaidi ya wateja wa corporate 100, zaidi ya miradi 1000 iliyokamilika, huku huduma zao zikiwa zimewafikia zaidi ya watu milioni 5 nchini Tanzania, Msumbiji na Malawi.


Nguvu ya upatanifu: Mashine za ATM

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UBX Seronga Wangwe amesema kuwa hakuna kampuni iliyowahi kutengeneza mifumo kama hii nchini. Anasema kuwa UBX ni ‘Mama wa Upatanifu’.

Kampuni hii ilipoanza, walifanya kazi na benki tano tu, na ATM 30 katika mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Leo hii, kuna mabenki zaidi ya 18 yaliyounganishwa na zaidi ya ATM 280 za UmojaSwitch pamoja na zaidi ya ATM 800 za benki ya NMB.

Hivyo, wameweza kujenga mtandao wenye zaidi ya ATM 1000 nchini na kuwawezesha Watanzania kufanya miamala ya kibenki ya ada ndogo tu. jambo hili linajulikana kama upatanifu, au interoperability kwa lugha ya Kingereza. Ni hatua kubwa sana kwa Tanzania.

Kuna mambo matatu ambayo hufanyika katika upatanifu wa mashine za ATM. Moja, ni kupunguza gharama kwa mteja na mabenki pia; pili, kufanya huduma zifikike kwa urahisi zaidi; na tatu kufanya huduma zitolewe kwa haraka zaidi. Mambo haya matatu ni matokeo kwa aina zote za upatanifu.

Lakini, huu ni mwanzo tu. UBX inatamani kuona sekta ya fedha ikiwa imeimarika na kuwa na upatanifu zaidi. “Tunatarajia kuwa benki kubwa zitaungana nasi, ili miamala ya kifedha ya ndani kati ya benki tofauti iweze kufanyika hapahapa Tanzania. Hii itapunguza gharama kwa walau asilimia 70 na kuongeza mapato ya mabenki na serikali pia. Hii ndiyo kesho tunayotaka kuiona,” alisema Wangwe.

Nguvu ya upatanifu: Mawakala

Kwa sasa, kila benki huwa na wakala wake ambaye anahudumia wateja wao tu. Hata hivyo, kuna njia mbadala. UBX inatarajia kumwezesha wakala mmoja kuwahudumia wateja wa mabenki mbalimbali.

Huu ndiyo upatanifu wa mabenki, mfumo ambao utapunguza gharama kwa mabenki na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa muda mfupi zaidi.

Vilevile, mawakala hutumia kifaa maalumu, yaani mashine ya POS, katika kutekeleza kazi zao. Wakala hutumia mashine moja kwa kila benki. Hata hivyo, mashine hizi zina gharama kubwa za manunuzi, matumizi na muda wa kumuelimisha wakala kuhusu jinsi ya kutumia mashine hiyo.

Kuwa na wakala anayetumia mashine moja kwa mabenki mengi itasaidia kutatua tatizo hili. Mbali na kupunguza gharama, pia mwananchi wa kawaida hatohitaji kusafiri umbali mrefu kutafuta mashine ya ATM au kutafuta wakala maalumu wa benki yake. Ikiwa mawakala hawa wako ndani ya jamii wanayoishi wateja, itasaidia kurahisisha upatikaji wa huduma tena iliyo bora.

Wangwe anasema, huduma zao zimewafikia wateja walio katika vikundi vya fedha kama SACCOS, ambapo wanachama wao huweza kupata huduma za ATM na Wakala nchini kote.


Kuwezesha ustawi wa sekta ya kifedha

Wangwe anafafanua kwamba kampuni aina ya startup na mabenki kutoka nje, zinazotaka kuanza shughuli zao Tanzania, hupaswa kufuata taratibu mbalimbali zilizowekwa na BoT pamoja na TCRA ambazo huwataka waweke taarifa zao katika mifumo ya ndani.

Hapo ndipo UBX inapoingia. UBX ndio kampuni pekee nchini inayoweza kuwasaidia kuanza kazi kwa wepesi, ikiwapa huduma za kutunza data zao na kuhakikisha kuwa wanafuata kanuni mbalimbali zilizowekwa. UBX ina data centre za kisasa jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Mikocheni na Kibaha.

Vilevile, UBX ndio kampuni pekee nchini Tanzania inayoweza kuchakata miamala ya Visa. Kwa sasa, UBX inafadhili benki sita katika kutumia huduma za Visa na inawezesha zaidi ya benki 15 kutoa kadi za Visa kwenye ATM zao. Huduma hii ingekuwa na gharama kubwa zaidi iwapo kila benki ingelazimika kujisimamia yenyewe katika hili. Huu ni mfano mzuri wa upatanifu wa benki za ndani na za nje ya nchi.

UBX imekuwa katika mstari wa mbele kuiwezesha jumuiya ya makampuni ya startup pale wanapohitajika. “Tunayo mifumo inayowezesha kazi zinazofanyika na makampuni ya startup. Tunatoa huduma za kuhifadhi data za application zao pamoja na suluhisho za kiteknolojia. Tunayo miundombinu ya kisasa na tuko tayari kufanya kazi kwa kushirikiana na wengine,” alisema Wangwe.

Hivi karibuni, Serikali ya Zanzibar iliipa kazi UBX ya kutengeneza mfumo wa kukusanya mapato ya ndani. “Ni mfumo wa kisasa zaidi kwa Afrika Mashariki na Kati. Mfumo huu umechangia ongezeko la mapato kwa kiwango kikubwa. Tunatiwa moyo kuona kuwa tuna nafasi katika kujenga uchumi wa nchi kama taasisi, na kuona jinsi serikali inavyotuamini,” Wangwe alisema.


Kubadilisha utamaduni

Bado kuna nafasi kubwa kwa makampuni ya kifedha kubadilisha utamaduni wa watu, anasema Wangwe. “Bado watu wamezoea kutumia hela wanazoweza kuzishika. Lakini jiulize, kwa nini mtu aende kwenye ATM kwanza akatoe hela, kabla hajaingia kwenye supermarket wakati anayo kadi ya visa? Kwetu sisi kwenye sekta ya fedha, pesa inayoshikika ni adui mkubwa,” alisema.

Alishauri kwamba kuna haja ya kuanza kuwafundisha watoto kuacha kutumia fedha ya mkononi na kuanza kutumia teknolojia zaidi. “UBX iko tayari kufanya kazi na serikali ili kuwapa wanafunzi ufahamu wa maswala ya ubunifu na teknolojia. UBX iko tayari kutoa huduma za elimu, na kuchangia katika maendeleo ya wabunifu wa kizazi kijacho nchini.

Watu wakikosa elimu ya fedha wanakuwa wagumu sana kubadilika utu uzimani. Haijawa rahisi kwa UBX kuleta mabadiliko chanya. Mbali na kufanya taasisi za kifedha, wamejihusisha pia na taasisi za usafirishaji kwa kutengeneza mifumo inayowawezesha wateja kufanya malipo kielekroniki.

Miaka michache iliyopita, UBX ilitengeneza mfumo wa mtandaoni kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam, ambapo wateja waliweza kununua tiketi mtandaoni. Haya yalikuwa mafanikio makubwa. Hata hivyo, makondakta hawakufurahia jinsi ambayo mfumo ulikuwa wa wazi; jambo lililoleta ugumu katika kutekeleza zoezi hilo.