Usiku wa Ulaya unavyozichonganisha Chelsea, Spurs

London,England. Matokeo ya mchezo kati ya Chelsea na Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Stamford Bridge yatakuwa na athari hasi ama chanya kwa timu nyingine tano tofauti na hizo mbili zinazoumana leo kuanzia saa 3:30 usiku ukiwa ni muendelezo wa Ligi Kuu England (EPL).

Ukiondoa Chelsea na Spurs zenyewe, Liverpool, Aston Villa, Manchester United, Newcastle United na West Ham United kila moja inayasubiria kwa namna tofauti kulingana na nafasi iliyopo kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Vita ya kuwania kushiriki mashindano ya klabu Ulaya msimu ujao kuanzia yale ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hadi yale ya Europa Conference ndio inayofanya timu hizo saba kutegemea zaidi matokeo ya mechi baina ya timu hizo mbili za jiji la London leo kuona yataziweka katika nafasi gani wakati msimu ukielekea ukingoni.

Liverpool iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa EPL, inaiombea mabaya Tottenham Hotspur katika mechi ya leo ili yenyewe ijihakikishie rasmi kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, baada ya kutofanya hivyo msimu huu.

Kama Spurs itapoteza mechi ya leo, haitoweza kufikisha pointi 75 kwani itabakia na pointi zake 60 hivyo hata ikipata ushindi katika mechi nne itakazobakia, itavuna pointi 12 na hivyo kumaliza ikiwa na pointi 72, jambo ambalo litaifanya Liverpool iwe na uhakika wa kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi zake 75.

Timu nyingine ambayo itanufaika na kichapo cha Spurs leo ni Aston Villa iliyopo katika nafasi ya nne ikiwa imekusanya pointi 67.

Kupoteza kwa Tottenham Hotspur leo kutaifanya Aston Villa iihitajike kuvuna pointi tano tu katika mechi tatu ilizobakiza ili nayo ijihakikishie kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Lakini kama Spurs itapata ushindi, itaiweka Aston Villa katika presha kubwa kwa vile itafikisha pointi 63 na huku ikiwa na faida ya kuwa na mechi mmoja mkononi ambayo ikipata ushindi itakuwa nyuma ya timu hiyo inayoshika nafasi ya nne kwa sasa kwa tofauti ya pointi moja.

Manchester United iliyo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi nayo inaiombea Spurs ipoteze mechi ya leo ili iweke hai matumaini yake ya kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Ligi ya Europa msimu ujao.

Kwa pointi 54 ilizonazo, Manchester United haitoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani hata ikipata ushindi katika mechi zake nne ilizobakiza, itamaliza ikiwa na pointi 66 ambazo hazitofikia zile ambazo Aston Villa iliyo nafasi ya nne imezikusanya hadi sasa.

Timu nyingine ambazo zinasubiria kwa hamu Spurs iangushe pointi leo ni Newcastle United iliyo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 53 na West Hamu United iliyopo nafasi ya saba ikikusanya pointi 49.

Ushindi wa Spurs leo utazika rasmi ndoto za West Ham kushiriki Kombe la Europa msimu huu ujao huku ukiweka rehani matumaini ya Newcastle United kuwepo katika mashindano hayo ambayo yanashika nafasi ya pili kwa thamani na ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.

Wenyeji Chelsea wanategemea ushindi katika mechi ya leo ili uweke hai ndoto zao za kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Europa msimu ujao lakini kama itashindikana basi kuweka matumaini ya kuwepo kwenye Kombe la Europa Confrence msimu wa 2024/2025.

Mechi hiyo ya leo itachezeshwa na refa Robert Jones ambaye atasaidiwa na Ian Hussin na Wade Smith huku refa wa nne akiwa ni Tim Robinson.

Kwa upande wa waamuzi watakaokuwa katika chumba cha teknolojia ya vide ya usaidizi kwa marefa ni Michael Salisbury na James Mainwaring.

Chelsea inaingia uwanjani huku ikiwa na historia nzuri ya ubabe mbele ya Spurs ambapo katika mechi 63 zilizokutanisha timu hizo, imeibuka na ushindi mara 34 na kupoteza mechi nane tu huku michezo 21 baina yao ikimalizika kwa sare.

Katika mechi tano zilizopita baina yao kwenye EPL, Chelsea imepata ushindi mara tatu, Spurs imeshinda moja na mechi moja ilimalizika kwa sare.