Miaka 10 ya ACT Wazalendo wakijenga imani katika nyakati ngumu

Mwanzo unaendana na tenzi ya “wanakwenu kwa heri”, au hadithi ya wana wa Israel kuondoka Misri, kufuata malisho mema Nchi ya Ahadi. Wanasiasa walioshindwa kuiva chungu kimoja na viongozi wenzao Chadema, wakaanzisha ACT Wazalendo.

Miaka 10 ilishatimia tangu ACT Wazalendo wapewe usajili wa muda. Mei 5, 2024, itatimia miaka 10 tokea walipopata usajili wa kudumu. Hadithi ya siku 3,652 ina simulizi mseto, lakini chama hicho kimeweza kushika nafasi za juu miongoni mwa vyama vitatu vikubwa Tanzania. Zaidi, ACT Wazalendo ni chama mwenza kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Mithili ya hadithi ya wana wa Israel; Novemba 2013, jioni, ilitolewa taarifa kuwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, Tanzania Bara, Zitto Kabwe, alivuliwa nafasi zote za uongozi kwenye chama hicho. Kosa ni kubainika kuandaa waraka wa kimapinduzi.

Pamoja na Zitto, wengine ni Profesa Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, vilevile aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba. Wakati Zitto akivuliwa nafasi za uongozi, Kitila na Mwigamba, walivuliwa uanachama.

Zitto, hakuwa tu Naibu Katibu Mkuu Chadema, bali pia Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni. Nafasi hiyo pia aliipoteza. Alikaribia kupoteza na ubunge wake, jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), akawahi mahakamani kukizuia chama hicho kujadili uanachama wake.

Huo ndio mwanzo wa ACT Wazalendo na riwaya ya kuanzisha chama ndani ya chama. Kilizaliwa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT). Kikaitwa ACT Tanzania. Ilianza kama fununu kuwa Zitto akiwa bado mwanachama wa Chadema, alianzisha ACT Tanzania.


Zitto kujiunga ACT

Machi 10, 2015, Zitto alifukuzwa uanachama Chadema, baada ya kesi aliyofungua kupinga uanachama wake kujadiliwa, kuondolewa mahakamani. Zitto akaaga bungeni, halafu akajiunga ACT Tanzania, usiku, Tegeta, Dar es Salaam.

Aprili 20, 2015, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alitoa tamko la kubadili jina la ACT Tanzania kuwa ACT Wazalendo. Kuingia kwa Zitto, mwanasiasa maarufu na mashuhuri, kulisababisha umaarufu wa chama hicho upae ghafla.

Zikafuata tamthiliya za mgogoro wa kugombea chama, baina ya Kidawi Limbu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa muda wa ACT dhidi ya Zitto. Mgogoro wa Limbu ulianza mwaka 2014, alipopishana na waliokuwa maswahiba wa Zitto, Profesa Kitila na Mwigamba.

Desemba 31, 2014, Limbu aliitisha mkutano aliouita wa Kamati Kuu, kisha kutangaza uamuzi wa kuwafukuza uanachama Kitila na Mwigamba. Halafu, Mwigamba, akiwa Katibu Mkuu wa ACT Tanzania, aliitisha vikao viwili, Kamati Kuu iliyoketi Januari 5, 2015 na Halmashauri Kuu, Januari 12, 2015, uamuzi wa jumla ukawa kumfukuza uanachama Limbu. Ikawezekana kumwondoa Limbu, halafu chama kikafanya uchaguzi. Zitto akachaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama (KC), Anna Mghwira akawa Mwenyekiti, Mwigamba aliendelea kuhudumia nafasi yake ya ukatibu mkuu. Profesa Kitila, aliteuliwa kuwa mshauri mkuu.

Kipindi safu ya ACT Wazalendo inaundwa rasmi, ilikuwa imebaki miezi sita kufanyika Uchaguzi Mkuu 2015. Mchoro maarufu wa katuni, ukimwonesha Zitto anamwagilia mche unaoanza kuota, kwa matumaini ya kukua ili uwe mti mkubwa. Ni uwasilishaji wa mchoraji gwiji, Ally Masoud “Kipanya”, akitafsiri kazi ngumu iliyokuwepo ya kukijenga ACT Wazalendo, kiweze kukua na kitoe ushindani.

Katuni hiyo haikuwa mbali na kitovu cha ukweli. Matumaini yote ya ACT Wazalendo, yaliegemea kwa mtu mmoja; Zitto. Mbio za urais hadi mchuano wa wabunge majimboni, chama hicho kilitegemea nguvu ya Zitto ambaye wakati huo alikuwa wamoto kwelikweli.

Bahati mbaya kwa Zitto na ACT, Uchaguzi Mkuu 2015, ulikuwa mgumu zaidi katika historia ya siasa Tanzania. Waziri Mkuu aliyejiuzulu Februari 2008, Edward Lowassa, alicheza karata ngumu kushinda urais. CCM wakati huo ikiwa chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, kilicheza mpira mgumu, kuhakikisha Lowassa hafanikiwi.

Kikwete akiibeba CCM begani na mgombea wake, Dk John Magufuli, Lowassa kwa tiketi ya Chadema, akibeba baraka za vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikasababisha taifa ligawanyike vipande viwili; wa Magufuli (Kikwete na CCM), wa Lowassa (Ukawa). ACT, chama kichanga, kilikutana na dhoruba kali.


ACT si kwa bahati

Yupo mtu anaweza kudhani ACT Wazalendo ni chama chenye bahati ya mtende kuotea jangwani, kisa wimbi la wanachama wa Civic United Front (Cuf), waliohamia ACT mwaka 2019, la hasha! Sifa nyingi ziende kwa viongozi, hasa Zitto, kwa uvumilivu na kusimama imara licha ya majaribu na mitihani mingi.

Oktoba 15, 2015, aliyekuwa mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, alifariki dunia kwa ajali ya helikopta, iliyotokea kwenye pori la Selous, kijiji cha Mtende, Morogoro. Baada ya kifo hicho, Zitto alieleza jinsi ambavyo alishirikiana na Deo katika kuasisi ACT.

Kumbe, Deo akiwa CCM, kutokana na uswahiba wake na Zitto, alihakikisha anatoa kila mchango kuhakikisha ACT Wazalendo siyo tu kinapata usajili, bali pia kinakuwa taasisi kubwa ya kisiasa. Siku 10 kabla ya Uchaguzi Mkuu, Deo alifariki dunia. Unaweza kutafakari iliumiza kiasi gani.

Kabla ya hapo, Zitto alipokuwa anaasisi ACT, alikuwa na matumaini makubwa ya kiushirikiano na aliyekuwa mshirika wake wa karibu, David Kafulila, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kusini 2010 – 2015. Kafulila hakuhamia ACT. Naye alikuwa silaha tegemeo ya Zitto katika kuiimarisha ACT. Hivi sasa Kafulila ni Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Uchaguzi Mkuu 2015, ACT walionesha hamu kubwa kwenye majimbo. Walisimamisha wagombea ubunge wengi, wakishika nafasi ya pili nyuma ya CCM. Hata hivyo, matokeo hayakuwa mema kwao. Mbunge mmoja tu, Zitto, ambaye alifanikiwa kushinda ubunge jimbo la Kigoma Mjini na akawezesha ACT kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mgombea urais wa ACT, Mghwira, alipata kura 98,763 katika kura 15.2 milioni, zilizopigwa kuchagua rais. Magufuli na Lowassa, peke yao walikusanya kura 14.95 milioni, katika jumla ya kura 15.2 milioni. Huo ni uthibitisho kuwa mchuano wa uchaguzi ulikuwa wa pande mbili. Hakukuwa na fursa ya mgombea wa tatu kuleta changamoto ya matokeo (kingmaker scenario).

Machi 28, 2015, Zitto alichaguliwa kuwa Kiongozi wa ACT. Oktoba 25, 2015, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu. Hivyo, Zitto alikiongoza chama hicho kwa miezi saba kasoro siku tatu, uchaguzi ukawadia. Baada ya uchaguzi, kilikuwa kipindi cha kuuguza majeraha ya kushindwa. ACT haikufikisha japo asilimia tano ya kura za wabunge, iweze kupata fursa ya kuteua wabunge wa viti maalumu pamoja na ruzuku.

Ulipowadia mwaka 2016, Dk Magufuli akiwa Rais wa Tanzania, alipiga marufuku shughuli za kisiasa. Zikageuka nyakati za vuta nikuvute baina ya viongozi wa upinzani na dola.

Zitto alikuwa mmoja wa viongozi waliolala mahabusu mara nyingi. Halafu, wabunge na madiwani wa upinzani walihamia CCM kwa hoja kumuunga mkono Magufuli. ACT ilipoteza madiwani wengi katika hamahama hiyo.

Aliyekuwa Mshauri Mkuu wa ACT, Profesa Kitila, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, kisha aliyekuwa Mwenyekiti Mghwira, akawa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Mwaka 2017, aliyekuwa Mshauri wa ACT, Albert Msando, ambaye alimpokea kijiti Kitila, alikumbwa na kashfa ya mambo binafsi ya kijamii, akalazimika kujiuzulu.

Halafu, Mwigamba, Msando, Mghwira na Kitila, wakahamia CCM. ACT ilibaki na upweke mkubwa. Watu muhimu kwenye chama, waliondoka. Wapo waliosajiliwa na Dk Magufuli, aliyeamua kuwatumia kwenye Serikali yake, wengine walihamia CCM katika mkumbo maarufu mwaka 2016-2020, ulioitwa “kuunga mkono juhudi za Magufuli.”


Mwanga mpya ACT

Machi 18, 2019, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, aliongoza kundi kubwa kuhama kutoka Cuf na kuhamia ACT. Ni kutoka hapo, angalau ACT ikapata nguvu Zanzibar. Ikajenga matarajio ya wabunge wengi au hata kushinda urais visiwani. Uchaguzi Mkuu 2020, dunia ilishuhudia uharibifu mkubwa. Vyama vyote vya upinzani vililia. ACT haikuwa na nafuu.

Kulekea Uchaguzi Mkuu 2020, ACT walimpokea mwanasiasa na mwanadiplomasia nguli, Bernard Membe. Matumaini yaliongezeka. Membe akateuliwa kuwa mgombea urais wa ACT. Hata hivyo, kadiri siku zilivyosogea, mazingira yalimtafsiri Membe kuwa mmoja wa wagombea dhaifu, kwani hakuonyesha makeke.

Uchaguzi Mkuu 2020 ulipomalizika, Membe alitangaza kujivua uanachama wa ACT. Miezi mitatu baada ya kumalizika uchaguzi, Seif “Maalim” alifariki dunia. Othman Masoud ameingia kama mrithi wake ndani ya ACT. Awali, ilionekana Seif angeibeba ACT Zanzibar na Zitto, Tanzania Bara. Alipoongezeka Membe, matumaini yakawa makubwa.

Kwa mantiki hiyo, kuondoka kwa Membe na kifo cha Seif, mambo hayo mawili yaliiumiza mno ACT. Halafu mpaka wakati huo, hakukuwa na fursa ya kufanya shughuli za kisiasa. Vyama vya upinzani vilijitutumua kwa vipimo vidogo. Vivyo hivyo kwa ACT.

Januari 3, 2023, ruhusa ya kufanya siasa ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Vyama vya siasa vikaanza kufanya mikutano ya hadhara na shughuli nyingine za kisiasa bila bughudha. Machi 2024, Zitto alikabidhi uongozi wa chama kwa Kiongozi mpya, Dorothy Semu.

Kikokotoo kitakuonesha kuwa ACT, walifanya siasa za kujijenga kwa muda mfupi mwaka 2014, kisha chama kikakumbwa na mgogoro wa uongozi. Februari 2015, mgogoro uliisha, halafu chama hicho kikajielekeza kwenye uchaguzi wa ndani. Baada ya kupata safu ya uongozi, chama hicho kilikuwa na miezi saba ya kufanya siasa kwa nafasi, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.

Pamoja na changamoto lukuki, ACT kiliweza kujenga ahadi njema kwa Seif na viongozi wengine wa Cuf, wakiwemo waliokuwa wabunge wa Bunge la Tanzania 2015-2020, wakahamia. ACT wamekuwa mahiri wa kutumia mitandao ya kijamii kujenga ushawishi, kufanya siasa za kijamii, kuwafuata wananchi walipo na kuzungumzia matatizo yao.

Miaka 10 ya ACT Wazalendo ina tafsiri ya kujenga ahadi njema kisiasa katika nyakati ngumu. ACT ilianzishwa kama kimbilio salama kwa kila aliyekosa oksijeni ya kisiasa mahali alipokuwa, ikawa ahadi njema. Vifo, kukimbiwa na watu muhimu, kudhibitiwa kufanya siasa, bado chama hicho kilijenga ahadi njema kidemokrasia, hivyo kukimbiliwa na Seif pamoja na timu yake.