Emorata; Mila inayowazuia watoto wa Kimasai kupata elimu

Vijana wa Kimasai wakiwa katika sherehe ya maandalizi ya kuwapeleka jando (Emorata).Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Emorata ni kipindi ambacho vijana huandaliwa kutoka kundi la Layoni (ambao hawajatahiriwa) kwenda kundi la Morani (waliotahiriwa), ambao kimila ndio askari na walinzi wa jamii.

Kila baada ya kipindi cha miaka 14, jamii ya wafugaji wa Kimasai hutekeleza mila na desturi ya Emorata, ambayo ni kipindi cha jando kinachowatoa vijana wa kiume kutoka kundi la watoto kwenda kundi la watu wazima.

Emorata ni kipindi ambacho vijana huandaliwa kutoka kundi la Layoni (ambao hawajatahiriwa) kwenda kundi la Morani (waliotahiriwa), ambao kimila ndio askari na walinzi wa jamii.

Kipindi hiki kinachodumu kwa miaka saba mfululizo kabla ya kuanza tena baada ya miaka saba mingine, ni kipindi maalumu na chenye hadhi ya juu ambacho hutenganisha rika moja hadi jingine kwa jamii hiyo inayosifika kwa kudumisha na kuendeleza mila na desturi.

Hata hivyo, pamoja na mengi mazuri ya mila hiyo kwa Wamasai, Emorata pia ina madhara, changamoto na vikwazo vingi kwa maendeleo. Kibaya zaidi mojawapo ya sekta inayoathiriwa na mila hiyo ni elimu.

Utoro, kuacha shule na ujeuri kwa Morani
Vijana wanaokwenda Emorata hulazimika kukaa kwenye kambi maalum kwa kipindi cha kati ya mwezi mmoja hadi miezi sita kulingana na uwezo kiuchumi wa wazazi, hali inayosababisha wanafunzi wengi wa jamii hiyo hukatisha masomo na kwenda jandoni.

Katika kipindi hicho cha Emorata, vijana hao hufundishwa stadi mbalimbali za maisha, ikiwemo ulinzi wa jamii, kulea, kuhudumia na kutunza familia pamoja na ujasiri wa kukabiliana wanyama wakali kama Simba, Chui, Nyati, Mbogo, Duma na wengineo.

Vijana hao pia hufundishwa mbinu za kukabiliana na makabila mengine yanayohesabika kuwa ni maadui, hasa makabila yanayojihusisha na wizi wa mifugo ambayo ndiyo rasilimali kubwa kwa jamii ya Kimasai.

Kutokana na mafunzo wanayopata huko, wanafunzi wa kiume wanaofanikiwa kurejea shuleni baada ya Emorata, hukataa kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko katika makalio na walimu (hasa wa kike), kutokana na mafundisho kuwa wao ni watu wazima wasiostahili tena kuchapwa.

“Kama ni lazima kijana aliyetoka Emorata kuchapwa viboko, basi adhabu hiyo itolewe kwa siri ndani ya ofisi za walimu, isitolewe hadharani. Isitekelezwe na mwalimu wa kike au wa kiume aliyehudhiria Emorata ndani ya kipindi cha miaka saba ambaye kimila wako rika sawa,” anasema Tumaini Meshurian.

Meshurian mwenye elimu ya sekondari aliyopata kutoka Shule ya Sekondari Kimnyak wilayani Arumeru, anasema hata kama mwalimu atakuwa anamzidi mwanafunzi kwa miaka 14, lakini wanaangukia kwenye rika moja kwa kwenda jando msimu sawa wa Emorata.

“Wamaasai rika au umri huzingatia kipindi cha jando, siyo tofauti ya miaka. Anayetoka Emorata ni mtu mzima sawa na baba na babu yake,hastahili kuchapwa viboko hadharani mbele ya Malayoni (wasiotahiriwa). Adhabu yake ni kupigwa faini ya mifugo,” anaongeza kusema.

Nini hufanyika kwa wanaopuuza Emorata
Mratibu wa Elimu Kata ya Olkokola wilayani Arumeru, Obedi Keya ambaye pia ni Mmasai, anasema mzazi anayekaidi kumpeleka mtoto wake Emorata hupigwa faini ya dume la ng’ombe anayechinjwa na kuliwa pamoja na adhabu nyingine, ikiwemo nyumba zao (maboma) kuvunjwa na kutembezwa uchi mitaani wakiwa wamevalishwa mabati.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Elikuroti, wilayani Arumeru, Tajiri Skeita anasema madhara ya Emorata yanaweza kuepukwa kwa jamii kuelimishwa kuhusu umuhimu, faida na uzuri wa kuzingatia ya elimu sambamba na mila, desturi na tamaduni zao.

“Muda wa vijana kupelekwa jando uzingatie kipindi cha likizo na upunguzwe kutoka miezi sita hadi wiki tatu au nne ili kutoa fursa kwa wanafunzi kurejea shuleni baada ya Emorata,” anasema Skeita.

Kwa upande wake, Likihoki Saruni anapendekeza vijana wanaotoka Emorata kupewa nyadhifa za ukiranja shuleni, ili kuwaepusha udhalilishaji wa kuongozwa na wadogo zao wasiokwenda jando pamoja na adhabu ya viboko hadharani.

Kaimu Ofisa Elimu wa halmashauri ya wilaya ya Arusha, Frida Moirana na Ofisa Programu wa asasi ya Hakielimu, Elisante Kitulo, kwa pamoja wanakiri kuwa elimu kwa jamii hiyo, ndio njia ya kuepuka madhara ya Emorata.