Wahadhiri waonyeshwa njia ya kuzoa tuzo za tafiti

Mtaalam wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Hispania (ICREA) Profesa David Brickington. Picha na Sharon Sauwa

Muktasari:

Imeelezwa kuwa, ushirikiano wa kimataifa kati ya watafiti na wachapishaji  wa kimataifa ndio utakaoweza kurahisisha kazi

Dodoma. Mtaalamu wa utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Hispania, (ICREA) Profesa David Brockington amesema ushirikiano wa kimataifa utarahisisha kazi za utafiti nchini kuchapishwa kwenye majarida ya juu yanayokubalika kimataifa.

Machi mwaka jana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alizindua tuzo kwa wahadhiri wa elimu ya juu na  katika mwaka wa bajeti wa 2022/23 ilitengewa Sh3 bilioni.

Katika tuzo hizo, mhadhiri Mtanzania atakayefanikiwa kufanya vizuri atapatiwa Sh50 milioni, lengo likiwa ni kuwawezesha wanasayansi wengi kuchapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa.

Akizungumza leo Jumatatu Machi 25, 2024 wakati wa mafunzo kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Brockington  amesema jambo muhimu ni ushirikiano wa kimataifa kati ya watafiti na wachapishaji  wa kimataifa ndio utakaoweza kurahisisha kazi zao.

Amesema wataalamu wengi waliopo Udom, bado ni vijana, wana nguvu, hivyo wana uwezo na wigo mpana wa kuongeza uzuri wa kazi zao.

Profesa Brockington amesema katika mafunzo hayo, watajadili kazi zote zilizochapishwa na wataalamu duniani kote kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka juzi na kuangalia mabadiliko yaliyojitokeza kutokana na kazi walizofanya watafiti hao.

Amesema iwapo tafiti hizo hazikuleta mafanikio mazuri kwa jamii za watafiti na vyuo vikuu kwa jumla, watatakiwa kuwa makini kwa kutafuta njia nzuri itakayowezesha tafiti hizo kuleta mafanikio.

Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lughano Kusiluka amesema mafunzo hayo yanalenga katika kujenga uwezo wa wanataaluma na watafiti katika kuandika miradi mikubwa na mizuri ya utafiti pamoja na kuandaa machapisho mazuri yatakayotumika kutoa taarifa kwa watu duniani kuhusu tafiti.

Amesema kazi kubwa ya vyuo vikuu ni kutoa taaluma, kufanya tafiti na kutoa huduma za jamii za aina mbalimbali.

Amewataka wanataaluma na wanafunzi hasa wanaosoma shahada ya uzamivu kujiongeza katika kutafuta fursa za utafiti.

Mkuu wa Idara ya Jiografia na Mazingira kutoka Ndaki ya Jinsia na Sayansi ya Jamii Udom, Dk Augustine Mwakipesile amesema lengo la Udom ni kuhakikisha wahadhiri wanapewa mafunzo ya maeneo gani wanatakiwa kupeleka machapisho yao.

Amesema hiyo inatokana na eneo la mahali pa kupeleka machapisho ya wanataaluma kuingiliwa na watu wasio na sifa.

“Kuna machapisho ambayo wakati mwingine yanakwenda katika maeneo yasiyo sahihi. Hivyo yanakuwa na viwango vya chini na ikitokea yamechapishwa katika vyanzo kama hivyo yanapokuja ndani ya vyuo yanakataliwa,” amesema Mwakipesile.

Hivyo,  amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha kujua wapi pa kupeleka machapisho hasa nje ya nchi ambako ndipo chuo hicho kinapigia chapuo zaidi.