Rais Ruto amteua Kahariri kuwa CDF Kenya

Muktasari:

  • Kahariri anateuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya baada ya kifo cha Jenerali Ogolla aliyekuwa akishikilia wadhifa huo kabla ya kufariki dunia katika ajali ya helikopta.

Kenya. Rais wa Kenya, William Ruto amempandisha cheo Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri kuwa Jenerali na kisha kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi (CDF) leo Alhamisi Mei 2, 2024 kuchukua nafasi ya Francis Ogolla, CDF aliyekufa kwenye ajali ya helikopta.

Kwa mujibu wa tovuti ya Taifa Leo ya nchini Kenya, mbali na uteuzi huo, mabadiliko mbalimbali mengine yamefanyika ikiwamo; Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed amepandishwa cheo kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga na kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza kamandi jeshini.

Jenerali Kahariri anajaza nafasi ya Ogolla ambaye pamoja na wanajeshi wengine tisa, waliofariki dunia ajali ya helikopta katika eneo la Sindar, Kaunti ya Elgeyo Marakwet Aprili 18, 2024.

Machi 2024, Rais Ruto alimpandisha cheo Kahariri, wakati huo akiwa Meja Jenerali kuwa Luteni Jenerali na Naibu Mkuu wa Majeshi (VCDF).

Hii ilifuatia kustaafu kwa aliyekuwa VCDF wakati huo, Jenerali Jonah Mwangi na Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu, Luteni Jenerali Peter Mbogo baada ya wawili hao kustaafu.

Pia katika mabadiliko hayo, Meja Jenerali David Kimaiyo Tarus amekuwa Mkuu wa Kamandi ya Nchi Kavu.

Kwa mujibu sheria ya ulinzi ya Kenya, mabadiliko hayo na uteuzi huo wa CDF umeidhinishwa kwenye mkutano wa Baraza la Idara ya Ulinzi chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ulinzi Aden Duale.