Makonda ajizuia kuzungumza akihofia ‘kulikoroga’ mbele ya Dk Mpango

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amepunguza maneno kati ya aliyokuwa nayo, akihofu kuzungumza zaidi kunakoweza kumsababishia kile alichokiita ‘kuyakoroga.’

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameonyesha hofu ya kuzungumza mambo mengi mbele ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwa kuhofia kile alichokiita  ‘kuyakoroga.

Hofu yake hiyo inatokana na kile alichoeleza, yupo katika furaha na katika nyakati kama hizo akizungumza zaidi atayakoroga.

Kauli yake hiyo inakuja wakati ambao, Makonda amekuwa na historia ya kutoa kauli mbalimbali zinazoibua mijadala na hata kusababisha mashaka ndani ya Serikali.

Mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, Makonda aliahidi kuwataja mawaziri wanaoshiriki kulipa na kutuma watu wanaomtukana Rais Samia Suluhu Hassan mitandaoni.

Makonda pia  aliitwa na Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumuhoji kwa takriban saa tatu.

Makonda ameonyesha hofu hiyo leo Jumatano, Mei 1, 2024 alipotoa salamu za Mkoa wa Arusha katika sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi kitaifa.

Katika hotuba yake hiyo Makonda amemwomba Dk Mpango amruhusu kuzungumza maneno machache kati ya mengi aliyonayo kwa hofu kuwa, furaha aliyonayo itamfanya akoroge mambo.

“Hapa nitayakoroga mambo Mheshimiwa Makamu wa Rais uniruhusu niseme matatu, ukiwa na furaha sana unaweza ukajikuta unasema mambo mengi,” amesema.

Mambo hayo matatu aliyoyasema ni pongezi kwa Rais Samia kwa mchango wake katika sekta ya utalii unaosababisha matarajio ya ujio wa watalii wengi watakaofaidisha wananchi.

Jambo la pili, amesema ni ombi kwa Serikali kuu kuwezesha maboresho ya barabara katika Jiji hilo, kwa kuwa zilizopo hazipitiki kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Makonda, jambo la tatu ni kuwa  sherehe hizo zinafanyika katika wakati ambao Tanzania inadumisha umoja na kwamba hatatokea yeyote wa kuligawanya Taifa.