Jaji Warioba: Ukipewa nafasi ukaona inakuzidi sema atafutwe mwingine

Muktasari:

  • Jaji Warioba amesema yeye aliomba kuachia baada ya kutumikia nafasi ya uwaziri mkuu kwa kipindi cha miaka mitano ya utawala wa awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema viongozi wanaopewa fursa za kuongoza kwenye nafasi mbalimbali pindi wanapoona hawaziwezi wawe tayari kuziachia kwa manufaa ya taifa.

Jaji Warioba amesema yeye alifanya hivyo baada ya kutumikia nafasi ya uwaziri mkuu kwa kipindi cha miaka mitano ya utawala wa awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Amesema alifanya hivyo baada ya kuona amechoka na anahitaji kupumzika. Pia, uamuzi kama huo anasema uliwahi kufanywa na Edward Sokoine, akiwa waziri mkuu katika utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere.

Jaji Warioba: Ukipewa nafasi ukaona inakuzidi sema atafutwe mwingine

Jaji Warioba anatoa simulizi ikiwa sehemu ya safari ya uongozi wa uwaziri mkuu wa miaka mitano kuanzia Novemba 5, 1985 hadi Novemba 9, 1990 katika mahojiano maalum na gazeti hili, aliyoyafanya Aprili 5 mwaka huu ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Anasema katika kipindi chake cha uwaziri mkuu, baada ya miaka mitano kumalizika alimwomba Rais Mwinyi amruhusu kupumzika, asiendelee naye tena kwenye Baraza lake la Mawaziri kama waziri mkuu.

"Huwa nawaambia watu niliomba kupumzika lakini hawaamini, uzuri Mzee Mwinyi kwenye kitabu chake naye aliandika," amesema Jaji Warioba huku akitabasamu kwenye mahojiano hayo.

Kuhusu uamuzi huo, Jaji Warioba anasema hakutaka kuendelea na uwaziri mkuu baada ya kumaliza miaka mitano kutokana na ugumu aliopitia.

"Baada ya miaka mitano nilimwambia Rais, mimi tena basi tafuta mtu mwingine awe waziri mkuu. Nilikwenda kwa Rais nikamwambia Mzee, mimi nadhani sasa nipumzike pamoja na kwamba yeye (Rais) alitaka niendelee," anasema.

Anasema wakati ule ilikuwa ukipewa kazi kama unaiona unaiweza unafanya, huiwezi unakaa pembeni.

Jaji Warioba anatolea mfano mwingine wa Sokoine kuwa aliteuliwa kuwa waziri mkuu Februari 13, 1977 ilipofika Novemba 1980 yeye mwenyewe aliomba asiendelee.

"Mwalimu (Nyerere) alitaka aendelee naye, lakini yeye akaomba asiendelee apumzike. Baada ya miaka miwili Mwalimu akamrudia tena Sokoine,” anasema Jaji Warioba.

Sokoine alikuwa waziri mkuu kwa awamu mbili, Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 kisha akaingia Cleopa Msuya. Baadaye Sokoine akarejeshwa tena Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari.

Mzee Mwinyi aliyefariki dunia Februari 29 mwaka huu, katika kitabu chake ‘Mzee Rukhsa- Safari ya Maisha Yangu’ kinachoelezea masuala mbalimbali, amegusia suala la Jaji Warioba akieleza namna alivyotaka kuendelea naye kama waziri mkuu huku yeye akiomba kuachia.

Katika sura ya 13 ukurasa wa 157 wa kitabu chake, Mzee Mwinyi anamshukuru Jaji Warioba aliyekuwa waziri mkuu wake wa kwanza baada ya kuingia madarakani 1985. Mwinyi anakanusha kile alichosema maneno ya watu kwamba ‘alimteua Jaji Warioba kuwa waziri mkuu kwa kulazimishwa na Mwalimu Nyerere.’

“Si, kweli, na waliosema hivyo ni wazi hawakumjua Mwalimu vizuri. Ni kweli kuna mambo nilikuwa nashauriana na Mwalimu; lakini Mwalimu hakuwa aina ya mtu wa kukulazimisha au hata kukuingilia kwenye kuunda timu yako ya uongozi.

“Mimi mwenyewe nilitaka kiongozi wa aina ya Warioba, na isingekuwa yeye mwenyewe kuomba kupumzika ningeweza kuendelea naye katika kipindi change cha pili,” anasema Mzee Mwinyi kwenye kitabu chake na kuongeza:

“Alipoomba kuondoka ilibidi nimuulize anitajie nafasi nyingine anayoweza kulisaidia Taifa. Hadi leo, naendelea kumshukuru kwa alivyonisaidia katika miaka mitano ya kwanza ya uongozi wangu wa Taifa letu.”


Kila siku ilikuwa ngumu

Jaji Warioba anaeleza kuwa kipindi chote cha miaka mitano ya mwanzo akiwa waziri mkuu nchi ilivyopita kwenye hali ngumu. Walipokea utawala kutoka kwa Mwalimu Nyerere aliyeamua kung’atuka madarakani na Mzee Mwinyi kushika uongozi.

"Tumeingia hatukuwa na uwezo, hatukuwa na fedha za kigeni, baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika, ilibidi tuanzishe mashirika mapya, yalitumia fedha nyingi," anasema Jaji Warioba aliyezaliwa wa Bunda, Mkoa wa Mara, Septemba 3, 1940.

"Kisha vikaja vita vya Uganda mwaka 1978, tukatumia akiba yetu yote kwenye vita, mwaka 1979 bei ya mafuta ikapanda.

Tumeingia hali ikiwa ni mbaya, hatuna mafuta ya kutosha, hatuna bidhaa madukani sababu hatukuwa na uwezo wa kununua, tuna njaa, ilikuwa ni kuhangaika, kurekebisha hayo kipindi chote kile nilipoingia kuwa waziri mkuu,” anasema

Jaji Warioba anasema, si kwenye uwaziri mkuu pekee, hata akiwa kwenye utumushi wa umma, matukio yalikuwa ni mengi.

"Kuanzia nilipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika, ikabidi tuanzishe mashirika mapya, badaye nikawa waziri wa sheria. Hata Katiba hii tunayoizungumzia ya mwaka 1977 nikiwa mwanasheria mkuu tulipewa mwezi mmoja wa kuiandika,” anasema.

Anasema ni jambo ambalo lilizungumzwa kisiasa, mpaka chama kikaamua tunakuwa na Katiba mpya, wakati huo ilikuwa ni Tanu na ASP.

"Iliandikwa kwa mwezi mmoja, tena kwa Kiswahili, tuliyokuwa nayo kabla ilikuwa ni ya Kiingereza

Jaji Warioba anasema:"Hata nilipokuwa waziri mkuu, kulikuwa na matukio mengi tu, juzi juzi nilikuwa naangalia mafuriko ya Hanang, yalinikumbusha yaliyotokea Lindi na Mtwara mwaka 1990 nikiwa waziri mkuu."

Anasema alikwenda kuona madhara ambayo ukiacha miundombinu na madaraja makubwa vilivyosombwa na maji, alipofika Hospitali ya Ndanda, Padri wa pale akawa anamtembeza kwenye eneo ambalo lilibaki wazi.

"Aliniambia, pale kulikuwa na nyumba, nyingine ya bruda wao zimesombwa, na hata huyo bruda naye yuko humohumo kwenye maji, yapo hawajui ni wapi amenasa, tulipoteza watu zaidi ya 50,” anasimuliza Jaji Warioba

Anasema katika kipindi chake cha uwaziri mkuu kila siku ilikuwa ni ngumu.

"Ninachoshukuru tulikuwa na ushirikiano mzuri na timu ya washauri wa Rais ambaye pia alituamini tukaweza kusimamia mabadiliko. Kipindi chote cha Mwinyi kilikuwa cha mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa, kilikuwa kipindi kigumu, wakati ule itikadi zetu na sera zilikuwa ni ujamaa, hivyo kubadili kutoka comand economy (uchumi hodhi) kuja free market (soko huru) haikuwa rahisi,” anasema.


Mwalimu Nyerere awakingia kifua

Katika mahojiano hayo ya zaidi ya dakika 120,Jaji Warioba anasema wakati fulani mwaka 1967, yeye na wenzake vijana wasomi ndani ya Tanu walianzisha kitu kinaitwa study group.

Anasema vijana wa wakati ule akiwamo pia Kingunge Ngombale Mwiru kazi yao ilikuwani kuwa na mijadala kwenye suala fulani, kisha wanawasilisha mawazo yao kwenye chama.

"Ilifika mahali baadhi ya wazee wakawa wanaona hawa ni vijana wakorofi na wasaliti, wengine wakasema wanadhani tuadhibiwe au tufukuzwe kwenye chama.

"Aliyetuponya ni Mwalimu, alisema msishangae vijana kuwa na mawazo haya, akasema ukifika mahali ukute mawazo ya vijana yanafanana na ya wazee, ujue jamii ile imedumaa," anasema Jaji Warioba.

Anasema, Mwalimu aliwambia wale wazee kwamba, mabadiliko huwa yanaletwa na mawazo mapya na mawazo hayo yanatoka kwa vijana kwa kuwa wazee wanafanya vitu kwa mazoea.

"Hatukuwa tunatafuta vyeo, bali kutoa mawazo, tulijengwa vile kwa kutoweka tamaa ya cheo bali kupewa mafunzo ili uje uwe kiongozi mzuri, japo siku hizi wengi ni kama wanakazania vyeo," anasema.

Anasema, kwenye uongozi ni lazima vijana wapate uzoefu na mafunzo ili wakitoa mawazo yawe ni kwa nia ya kujenga.

"Siku hizi naona kama vijana wengi wanachotaka ni kuingia kule ili wapate nafasi," alisema Jaji Warioba akigusia mwelekeo wa vijana kupewa nafasi hivi sasa.

Anasema, hata wakati wao, Mwalimu Nyerere alitoa nafasi kwa vijana wengi.

"Mimi ni miongoni mwao, niliingia Baraza la Mawaziri mwaka 1976 nikiwa bado kijana wa miaka 35 nakwenda kufikisha 36.

"Baada ya uchaguzi wa 1975, Rais aliwapa nafasi vijana, alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri akaingiza vijana wengi, mmoja wetu alikuwa na miaka 24 au 25, wale wazee alioanza nao Mwalimu walibaki wachache, baadaye ndipo akawaleta vijana wengine kina (Benjamini) Mkapa na (Dk Salim Ahmed) Salim," anasema.

Anasema wakati Mwalimu Nyerere anakaribia kutoka madarakani alikuwa amebaki na wazee kama wanne alioanza nao.

“Alipokuwa anajiandaa kuondoka madarakani, Mwalimu akamteua Sokoine kuwa Waziri Mkuu, yeye naye alikuwa ni rika la vijana na hata utendaji kazi baada ya uteuzi huo ulibadilika,” anasema Jaji Warioba.

Maboksi mawili

Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba anafananisha makundi mawili yanayopongeza viongozi na linalowapinga kama maboksi ambayo hayana afya kwa mustakabali wa Taifa.

“Siku hizi kuna maboksi, moja kazi yake ni kusifu na jingine ni la kupinga tu. Sio kila kitu ni kusifu tu, hasa ili la kuwasifu viongozi, inafikia mahali unajiuliza hizi ni sifa kweli au kujipendekeza! Kuna boksi jingine nalo ni kupinga, kupinga kila kitu,” anasema akionyesha kuchukizwa.

Anasema kuna mambo kama Taifa ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo, mnaweza kutofautiana lakini kama taifa mnakaa na kukubaliana jinsi ya kulitekeleza kwa manufaa ya nchi.

Alitolea mfano, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kuwa ni mradi mzuri wenye tija kwa Taifa ambao kila mmoja angeweza kushiriki kwa mawazo ili kufikia lengo kama nchi.

"Tunajua ni muhimu tuwe na nishati ya kutosha, Bwawa la Nyerere ni jambo la kitaifa, japo tunaweza kuhitilafiana namna ya kulitekeleza, lakini ni la kitaifa, au reli ya kisasa kuna vitu vya kitaifa vinahitaji majadiliano ya pamoja sio kupinga tu," anasema.

Anasema, siku hizi siasa imekuwa kama ni watu, akitolea mfano miaka ya nyuma nchi ilikuwa inafanya mambo yake na kupongezwa na wengine.

"Tanzania ilikuwa inasifika sana kwa kuwa ilifanya mambo yake kwa msingi wa kitaifa, haikuwa ikijitangaza. Siku hizi tunajisifu sana, lakini huoni hizo sifa zinatoka nje, tunabaki tunajisifu wenyewe.

Mimi nadhani ama ni kusifu au ni kupinga, ikifika kwenye mambo ya kitaifa tuwe na mijadala ya pamoja, lazima tujue sisi ni Watanzania hata kama tuna mawazo tofauti tuzungumze tukubaliane masuala ya kitaifa," anasema.