Dawa za Serikali zanaswa zikiuzwa maduka binafsi

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Edgar Mahundi, akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Chato,  Said Nkumba boksi lenye dawa za binadamu.

Muktasari:

Kukamatwa kwa dawa hizo kumetokana na ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)  kanda ya Ziwa Magharibi.

Geita. Maduka muhimu ya dawa 78 katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera yamebainika kuwa na dawa na vifaatiba visivyoruhusiwa kuuzwa kwenye maduka hayo.

Maduka hayo pia yamekutwa yakiuza dawa za Serikali kinyume na sheria zote zikiwa na thamani ya Sh12.7 milioni.

Kukamatwa kwa dawa hizo kumetokana na ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)  kanda ya ziwa magharibi kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 ambapo maduka 600 yalikaguliwa na 78 kati yake yalibainika kuwa na dawa zisizostahili kuuzwa kwenye maduka muhimu ya dawa.

Meneja wa TMDA kanda ya Ziwa Magharibi,  Edga Mahundi ameyasema hayo wakati alipokuwa akikabidhi dawa hizo kwenye Magereza ya wafungwa na mahabusu ya Wilaya ya Chato.

Mahundi amesema miongoni mwa majukumu ya TMDA, ni kulinda afya ya umma kwa kudhibiti ubora usalama na ufanisi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi.

“Ukaguzi tuliofanya tumebaini uwepo wa dawa na vifaa tiba vilivyopo madukani kinyume na sheria ya dawa na vifaa tiba sura namba 219 na tumezipima   bado zinafaa kwa  matumizi ya binadamu lakini pia tulibaini dawa za Serikali zikiwa kwenye maduka binafsi.

“Kwa mujibu wa sheria tulitakiwa kuzitoa na kuzimiliki sisi sio watumiaji na ndio maana tumezileta Magereza ziwasaidie wafungwa na mahabusu na wagonjwa wanaohudumiwa kwenye zahanati hii, ”amesema Mahundi.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya dawa na vifaa tiba sura namba 219 na sheria ya  baraza la famasi sura 311, inaelekeza baadhi ya dawa zisizoruhusiwa kuuzwa kwenye maduka muhimu na badala yake zinapaswa kuuzwa kwenye maduka makubwa yenye wataalamu .

 Amesema wananchi wanalalamika kukosa dawa wanapofika kwenye hospitali za umma lakini wapo watumishi wasio waaminifu wanaoiba dawa hizo na kuziuza kwenye maduka ya dawa muhimu kinyume na sheria.

“Tulikamata dawa hizo na wahusika wamepigwa faini huku wale waliokutwa na dawa za Serikali walichukulkiwa hatua za kisheria ikiwemo kupandishwa mahakamani Mahundi amewataka  wamiliki wa duka muhimu kuzingatia taratibu na sheria huku akiwataka watumishi wa idara ya afya kuacha wizi wa dawa kwani wanaisababishia Serikali hasana na kuwakosesha wannachi huduma kwenye vituo vya afya vya umma .

Akipokea dawa hizo Mkuu wa Wilaya ya Chato Said Nkumba,  amesema kupatikana kwa dawa sio tu faraja kwa wafungwa bali itawasaidia pia wananchi wanaoishi karibu na magereza wanaohitaji huduma za afya katika zahanati iliyopo eneo la Magereza.

Amesema zahanati hiyo hupokea wateja kutoka maeneo tofauti na kuutaka uongozi wa Magereza  kuhakikisha dawa hizo zinatumiwa na walengwa na sio vinginevyo.