Dar, Lindi na Simiyu vinara uchepushaji dawa za Serikali

Muktasari:

  • Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Baraza la Famasi, Tamisemi na Jeshi la Polisi iliandaa na kufanya operesheni kati ya Novemba 20 hadi 24,2023.

Dar es Salaam. Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Simiyu imetajwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) kuwa vinara wa uchepushaji dawa za Serikali.

TMDA imesema operesheni iliyofanyika katika mikoa 13, imekamata dawa kadhaa zikiwemo zenye asili ya kulevya na za nusu kaputi zilizokutwa kwenye maduka ya dawa ambazo haziruhusiwi kuuzwa nje ya hospitali.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Desemba 20, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo alipotoa matokeo ya operesheni hiyo maalumu ya kukamata dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya Serikali, dawa bandia, duni, zisizo na usajili na dawa za kulevya.

"Vifaa tiba vya Serikali vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh11,297,500 vilikamatwa katika vituo na maduka binafsi.

"Baadhi ya vifaa tiba hivyo ni IV Cannula G21, G20, G22, vifaa vya kupima malaria na virusi vya Ukimwi, Hemocue Glocose201, Microcuvettes na Hemocue Hb2021 ambavyo vilikamatwa Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kati," amesema Fimbo.

Amesema lengo lilikuwa kubaini na kukamata bidhaa za Serikali zinazouzwa kwenye mnyororo wa ugavi, ambazo walizikuta zinauzwa maduka ya watu jambo ambalo haliruhusiwi.

Amesema katika operesheni hiyo ambayo jumla ya bidhaa zenye thamani ya Sh172 milioni zilikamatwa walibaini wachepushaji hao walikuwa wakifuta nembo za Serikali.

“Maboksi mengi yamefutwa maandishi yaliyosomeka GOT, hizi wamezitoa kwenye mnyororo wa Serikali zinauzwa maduka binafsi na nyingine tumezikuta zina nembo za Bohari ya Dawa (MSD),” amesema Fimbo.

Pia wamekamata dawa za Kifua Kikuu zikiuzwa nje ya mfumo wakati haziruhusiwi kuuzwa, dawa za uzazi za kutibu fangasi na dawa za operesheni zinazotumika kama nusu kaputi.

Amesema dawa bandia za mifugo na za binadamu zimekamatwa zikiuzwa mitaani. Dawa hizo zimechukuliwa kwa ajili ya vielelezo.

“Pia tumekamata dawa zenye ubora hafifu, bandeji ambazo ukibandika hazishiki, gozi zinazopukutika na bidhaa ambazo hazijasajiliwa,” amesema.

Fimbo amesema jumla ya Sh100 milioni zimekusanywa zikiwa faini walizotozwa wakosaji na wengine wamepelekwa Polisi.

Msajili wa baraza la famasia, Elizabeth Shekalaghe amesema wamekamata wauzaji wa dawa katika famasi na maduka ya dawa za binadamu na mifugo wasio na utaalamu.

“Kumekuwa na dhana potofu, wananchi wengi wakidhani biashara ya dawa ni nyepesi kufanya kwa lengo la kujipatia kipato, hizi dawa zilizokamatwa inawezekana katika maeneo mengine ambayo hatujafika zipo. Nitoe wito kwa wataalamu wote wa dawa tutumie weledi kufanya kazi zetu,” amesema.

Shekalaghe amesema kwa waliobainika taarifa itaenda kufanyiwa kazi na iwapo kuna mwanataaluma wa famasia amejihusisha na uuzaji wa dawa za Serikali, duni, bandia hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kufutiwa leseni.

“Tabia za wamiliki wa maduka kununua dawa za mikononi iachwe, natoa wito kwa wananchi kutupatia taarifa. Kila mtu anatakiwa kuhakikisha analinda afya ya mwingine,” amesema.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wamekamata watoa dawa 3,000 ambao waliuza bila kuwa na sifa.

Kwa upande wa Naibu Kamishna wa Polisi, Daniel Nyambabe amesema katika operesheni hiyo wamefungua majalada 13 kwa ajili ya kushughulikia kesi za uuzaji dawa za Serikali, bandia, duni na dawa za binadamu zenye asili ya kulevya kinyume cha sheria.

“Majalada 13 yamefunguliwa na yapo katika hatua za upepelezi chini ya ofisi ya Mkuu wa Mashtaka,” amesema.

Amewataka wauzaji kuhakikisha biashara zao hazikinzani na sheria.