CWT yawafedhehesha walimu Songwe

Picha ya walimu ambao ni wananchama wa Chama cha Walimu Tanzania  (CWT) Mkoa wa Songwe wakiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani (Mei Mosi) bila sare kama ilivyozoeleka.

Muktasari:

Walimu hao wamesema licha ya kukatwa asilimia mbili ya mshahara kila mwezi lakini wamekosa sare.

Songwe. Zaidi ya walimu 5,000 ambao ni wanachama wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Songwe, wameulalamikia uongozi wa chama hicho Taifa kwa kushindwa kuwanunulia fulana kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya  Wafanyakazi duniani (Mei Mosi) ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Ileje.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Mei Mosi, 2024 wakati wa maadhimisho hayo, baadhi ya wanachama wa CWT wameeleza kutofurahishwa kushiriki sherehe hizo bila kuwa sare kama walivyovaa wenzao kutoka vyama vingine.

Akizungumzia jambo hilo, mwalimu wa Shule ya Msingi Isansa iliyopo wilaya ya Mbozi, Basilyusi Ngonela amesema hawakutegemea chama hicho kikubwa nchini kitashindwa kuwanunulia sare kwa ajili ya sherehe hizo kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma.

“Sisi kama walimu tunakatwa asilimia mbili kwenye mishahara yetu ambayo tulipaswa tununuliwe na fulana za sare ya sikukuu hii, na tukiwauliza viongozi wa mkoa, wanasema tatizo ni makao makuu,” amesema Ngonela huku akiwataka viongozi wa CWT kujitathmini katika hilo.

Kwa upande wake, mwalimu Bestina Mbuligwe amesema wamesherekea sikukuu ya wafanyakazi kama yatima kutokana na sintofahamu ya kukosa sare za walimu mkoa wa Songwe ambao ni wanachama wa (CWT), kitendo ambacho kimewafanya wazomewe na wenzao wa chama kipya cha Chakuhawata (Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania).

“Kwa kweli leo tumetia huruma hadi mkuu wa mkoa ametuita tukacheze mbele kutokana na kukosa sare. Kwa kweli viongozi wetu hawajatutendea haki watwambie shida nini,” amesema Mbuligwe.

Akizungumza kwa masharti ya kutoandika jina lake, mmoja wa viongozi wa CWT mkoani Songwe amesema moja ya sababu ya kutokuwa na sare, kwa mujibu wa viongozi kitaifa, ni tatizo la kusafirisha fulana hizo, jambo ambalo limewapa wakati mgumu kwenye viongozi wa ngazi ya mkoa hadi wilaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesikitishwa na kitendo cha walimu ambao ni wanachama wa CWT kushindwa kuvaa sare kulikosababishwa na viongozi wao kushindwa kuwatimizia takwa lao la kikatiba, na kuwafedhehesha kwenye sikukuu ya wafanyakazi.

“Kwa kweli CWT hamjawatendea haki walimu, mkumbuke hili suala lipo kwenye mkataba ambapo kila wakati wa Siku ya Wafanyakazi, wanatakiwa wanunuliwe sare,” amesema Chongolo.