Bibi adaiwa kumfanyia ukatili mjukuu wake wa miaka minane

Mwonekano wa mwili wa mtoto Glory Felician (8) aliyekuwa akifanyiwa ukatili na bibi yake.

Muktasari:

  • Mtoto huyo ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, amekuwa akikatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni wembe sehemu mbalimbali za mwili wake na bibi yake huyo.

Moshi. Mtoto wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Himo, Glory Felician (8) ameokolewa na wanaharakati kufuatia vitendo vya ukatili anavyofanyiwa na bibi yake anayeishi naye katika mji mdogo wa Himo.

Mtoto huyo ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, amekuwa akikatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni wembe sehemu mbalimbali za mwili wake na bibi yake huyo.

Bibi huyo anadaiwa kutenda ukatili huo mwa mjukuu wake kwa nyakati tofauti ikiwamo pia kumnyima chakula na kumfungia ndani ya nyumba baada ya kurudi shule, akimtaka asitoke kwa kuhofia kwamba atawasimulia watu anavyonyanyaswa.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema bibi huyo alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi cha Himo.

“Ni kweli tukio hili lilitokea kwa bibi kumjeruhi sehemu za tumboni mtoto wa miaka minane aliyekuwa akiishi naye, tulimkamata na tayari tumefungua jalada la uchunguzi kwa hatua zaidi," amesema Kamanda Maigwa.

Mtoto asimulia

Akizungumza na Mwananchi Digital, mtoto huyo ambaye mwili wake umeharibiwa kwa kuchanwa sehemu mbalimbali ikiwemo tumboni na mikononi, amesema licha ya kumwomba bibi huyo asimfanyie ukatili huo, aliendelea kufanya hivyo.

“Bibi amekuwa akinifinya na wembe sehemu mbalimbali za mwili wangu, wakati mwingine nikitoka shule kutokana na maumivu ninayopitia napita polisi nawaeleza bibi anavyonifanyia, wakawa wananiambia bibi akizidi kunifinya niende niwaambie, nilienda nikamwambia bibi polisi watakukamata kama utaendelea kunifinya,” amesema.

Amesema inafika wakati usiku anashindwa kulala kutokana maumivu anayokuwa nayo.

Ameeleza kuwa  kutokana na majeraha kuuma wakati wa usiku alikuwa anajikanda mwenyewe ili apate usingizi.

Glory amesema bibi yake alikuwa hampi chakula, hali ambayo ilikuwa ikimlazimu kunywa uji shuleni mara tatu ili anaporudi nyumbani awe ameshiba.

“Bibi alikuwa hataki niende kwa majirani na wakati mwingine hanipi chakula, nilimwambia kama hunipi chakula bora niondoke kuliko kunitesa, akaniambia nile chakula tu cha shuleni, nikamwambia sawa nitakula tu, hivyo nikiwa shuleni nakunywa zangu uji hadi vikombe vitatu ili nishibe,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, ameomba bibi huyo akamatwe na achukuliwe hatua ili iwe ni fundisho na kuacha kutesa watoto.

Wanaharakati wafunguka

Akizungumzia namna walivyombaini mtoto huyo, Vicky Massawe ambaye ni mwanaharakati na Katibu wa kikundi cha Ushujaa wa Maendeleo na Ustawi Jamii Tanzania (Smaujata), halmashauri ya Moshi vijijini, amesema baada ya kupata taarifa za ukatili wa mtoto huyo walipambana hadi kufika eneo analoishi na kuchukua hatua.

“Baada ya kupata hii taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba kuna mtoto yupo hapa Himo anafanyiwa ukatili, tulifuatilia kujua huyu mtoto alipo, tulipewa ramani alipo na tulipofika tulimkuta akiwa katika hali mbaya, alikuwa na makovu mwili mzima.

“Tulimuuliza huyo bibi kwa nini alimfinya na kumjeruhi mtoto, akatuambia alimfinya kwa sababu mtoto anapenda kutoroka kwenda mtaani, lakini tulipozungumza na majirani walituambia huyu mtoto hajawahi kutoka nje ya geti na kwamba amekuwa akimfanyia ukatili,” amesema.

Amesema walimchukua mtoto huyo pamoja na bibi yake, wakaenda kituo cha polisi kwa ajili ya kupata RB ya matibabu ya mtoto na bibi yake aliwekwa ndani. Amesema kwa sasa mtoto yupo kituo cha watoto waliofanyiwa ukatili na  yatima mjini Moshi.