Waagizaji wa mafuta watoa angalizo kuhusu dola

Muktasari:

  • Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), kimesema hali inaweza kuzidi kuwa mbaya iwapo changamoto ya upatikanaji wa dola ya kimarekani haitatuliwa kwa haraka.

Dar es Salaam. Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), kimesema hali inaweza kuzidi kuwa mbaya iwapo changamoto ya upatikanaji wa dola haitatuliwa kwa haraka.

 “Tunaiomba Serikali iongeze nguvu kuhakikisha dola zinapatikana kwa kushirikisha benki za biashara, ili kuepuka changamoto hii kuleta athari kubwa,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Taomac, Salim Baabde, alipokuwa kwenye kikao na Waziri wa Nishati, Januari Makamba jana.

Kwa mujibu wa chama hicho, uhaba wa dola katika soko la fedha, umesababisha waagizaji kupunguza kiasi wanachoagiza ili kuepuka kushindwa kuulipia kwa wakati.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutafuta mwaarobani wa changamoto zake, waagizaji hao wamesema uhaba huo unaongeza gharama za uendeshaji wa biashara na kuathiri bei ya mafuta kwa mteja wa mwisho. 

“Biashara yetu inafanyika kwa kutumia dola ya Marekani, na pale inapotokea dola inakuwa adimu sokoni, huaathiri moja kwa moja bei ya uagizaji ambayo nayo inaathiri bei ya mafuta kwa mtumiaji wa mwisho,” amesema.

Makamba amesema Serikali inaelewa changamoto ambazo sekta inakabiliana nazo, na kwamba hatua madhubuti zimeendelea kuchukuliwa. Pia aliwashukuru kwa ushirikiano wa kuhakikisha nchi inapata mafuta muda wote.

Waziri Makamba pia alieleza kwamba mlango wake uko wazi wakati wote kwa ajili ya mashauriano. “Sisi hapa Wizarani filosofia yetu ni ile ya ‘open door,’ yeyote anakaribishwa kwa ajili ya mashauriano na majadiliano,” amesema.

Makamba alisisitiza umuhimu wa wadau ikiwemo Taomac kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika kwa ajili ya ustawi wa nchi na watu wake.