Zena: MCL inaonesha kwa vitendo namna ya kuimarisha mshikamano

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Zena Ahmed  Said

Muktasari:

Baada ya MCL kuzindua Kampeni ya The Citizen Rising Woman Zanzibar, inaelezwa kuwa jambo hilo linakwenda kuongeza mshikamano wa Muungano badala ya kupeleka magazeti pekee

Unguja. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Zena Ahmed Said amesema Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL) imeanza kuonesha kwa vitendo namna ya kuimarisha mshikamano wa Muungano.

Zena ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 25, 2024 alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya The Citizen Rising Woman katika Hoteli ya Madnat, Unguja Zanzibar.

“Jambo hili linaongeza mshikamano wa Muungano badala ya kuwa mnaleta magazeti pekee," amesema Zena.

Katika hatua nyingine, Zena amesema mtoto wa kike ana nafasi ya kufika anapopataka endapo atajiwekea malengo yake yatakayoambatana na juhudi zake.

Zena amesema jambo kubwa la kuzingatia ni kuwa waadilifu na waonyeshe uwezo kwa kazi wanazopewa kuzifanya.

Amesema licha ya nafasi chache, zinatosha iwapo mtu akijitambua na kujiwekea malengo sahihi.

Katibu Mkuu Kiongozi Zena amesema jambo lingine linalotakiwa kuzingatiwa ni kujali muda wa kufanya kazi kwa wakati ili kuthibitisha uwezo wa mtu anapopewa nafasi.

Pia, amesema wanawake na watu wengine pia, wanatakiwa kujiamini na kuondoa hofu, pale wanapopatiwa nafasi ya kufanya kazi au kuongoza.

"Ipo tabia ya watu kuwa na hofu na kujiona hawana uwezo, lakini jiamini na ondoa hofu ukiamini unaweza kufanya kile unachokiamini mbele ya macho ya wengi," amesema katibu mkuu huyo kiongozi.

Amesema kuna changamoto kwa baadhi ya watendaji kushindwa kutoa taarifa za ukweli, wakidhani viongozi wakuu wataiona vipi.

"Tusiwe na hofu kupeleka taarifa za kweli kwa viongozi wetu, maana hiyo ndiyo njia ya kumfanya kiongozi wako aweze kufanya uamuzi sahihi, lakini ukimdanganya atashindwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya uamuzi na wewe utaonekana hufai," amesema Zena.

Pia, amesema sio watu wote wanapoteuliwa kwenye nafasi za uongozi wanakuwa na uelewa wa mambo hayo jambo kubwa ni kujifunza akijitolea mfano nafasi alizopitia lakini hakuwa na utaalamu tofauti na taaluma yake ya uhandisi.

Pia, amesema uaminifu ni jambo muhimu katika nafasi yoyote anayopewa mtu ikiwamo kutenda haki kwa usawa katika nafasi wanazopewa.

"Wakati mwingine tunapewa nafasi lakini tunawaumiza wengine, tunampa nafasi asiyestahili na kumuacha anayestahili jambo linaloumiza wengi," amesema Zena.

Amesema changamoto kubwa inayoikumba Zanzibar watendaji kuwa na muhali wa kuchukua hatua, "tekeleza majukumu yako kwa ukamilifu na jitathimini kwa unayoyafanya."