VIDEO: Siri urais wa Samia

Rais Samia akizungumza katika Jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika Machi 8, 2024 katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam leo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema haikuwa rahisi kwake kupokea kijiti cha urais na ilimlazimu kutumia hekima kubwa kuwaondoa Watanzania hofu waliyokuwa nayo.

Samia aliapishwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke, Machi 19, 2021 akichukua nafasi ya hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huo.

Samia aliyekuwa makamu wa Rais, amesema hofu hiyo ilitokana na ukweli kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Taifa kupoteza kiongozi mkuu wa nchi akiwa madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na makamu wake, ambaye ni mwanamke.

Ametoboa siri hiyo na ujasiri wake wakati akifafanua kauli maarufu aliyoitoa wakati wa msiba wa Hayati Magufuli, kuwa   “aliyesimama hapa ni Rais, ni Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania,  ambaye maumbile yake ni mwanamke”  kwenye mahojiano maalumu yaliyoendeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu.

Mahojiano hayo yamefanyika leo Machi 8, 2024 kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo  Samia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la nne la jukwaa la The Citizen Rising Woman linaloandaliwa na MCL.

Rais Samia amesema alilazimika kutumia busara hiyo kuwatoa hofu Watanzania,  akijua kuna hofu iliyokuwapo ya baadhi ya  watu kutilia shaka kama angeweza kubeba jukumu hilo.

“Nilisema vile nikijua changamoto na wasiwasi uliopo mioyoni mwa watu, anaingia mwanamke kwa vishungi vyake, anasema kwa wepesi zaidi, anatazama kama hataki. Nikaona ngoja niwatoe watu kwenye hofu kwa kuwa nchi ina msiba ni lazima ivuke salama. Ule ulikuwa mtihani wangu wa kwanza.

“Hofu isingeacha kuwepo, kwa sababu hatujawahi kupoteza Rais akiwa madarakani, hofu ya pili ni nafasi hiyo kuchukuliwa na mwanamke. Labda ingekuwa mwanamke dume lakini niliingia nikiwa mwanamke hasa na niliyasema maneno yale nikiwa hata sina uhakika wa ninachokisema,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo amesema minong’ono iliyokuwepo wakati anaingia madarakani, ilimsukuma kutamka maneno hayo ambayo aliamini yangejenga imani ya Watanzania kwake.

“Kilichonisukuma kusema vile, tayari kulikuwa na minong'ono ataweza kweli huyu, hebu angalieni, kweli inawezekana, mwanamke kweli, lakini nikawaambia aliyesimama hapa ni Rais  mwenye maumbile  ya kike.  Urais hauna jinsi,  Rais ni Rais, mamlaka ni mamlaka,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.

LIVE: Rais Samia akishiriki kampeni ya ‘The Citizen Rising Woman’

Hata hivyo, Rais Samia amekiri kuwa mambo hayakuwa rahisi wakati anapokea kijiti cha kuongoza nchi kutoka kwa mtangulizi wake, hasa uendelevu wa miradi mikubwa ambayo alikuwa ameanzisha.

“Joto nililopata ni kwamba naenda kuwa mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, hiyo ni kazi pevu. Nilifikiri pia kuhusu miradi mikubwa ambayo ilikuwa imeshaanza. Niliwaza pia mapokezi yangu kama Rais wa kwanza mwanamke, nifanye nini ili wakubali kwamba ninaweza.

“Wakati naingia pia dunia ilikuwa kwenye janga la Uviko-19, uchumi unashuka, miradi inakutazama ilikuwa tanuru la moto, lakini nikasema kama nilishika kitabu ninachokiamini na kuapa nitafanya kazi hii basi Mungu atanionesha njia. Nilitumia mbinu za medani, namshukuru Mungu nimeweza,” alisema huku akitabasamu, kisha akahoji, si nimeweza, au siyo?

Kuhusu kama aliwahi kuwa na ndoto ya kushika nyadhifa za juu za uongozi kama makamu wa rais na urais, amesema: “Ndoto yangu ilikuwa kwenye ubunge au Baraza la Wawakilishi, hata nilipotangazwa uwaziri nilishangaa. Sikuwahi kuwa na ndoto ya kuwa makamu wa rais wala Rais. Mengine yaliyotokea yalitokea labda kwa sababu ilionekana naweza.”

Kupita mahojiano hayo, Rais Samia ametoa rai kwa wazazi kuwekeza kwa watoto wao bila kujali jinsi, kwa kile anachoamini binadamu yeyote akijengewa uwezo, anaweza kufanya makubwa.

“Tunapozaliwa wote tunakuja hali moja, hakuna anayekuja na nguo mkononi wala kitu kashika mkononi, wote tunazaliwa na hali moja na hapo ndiyo tunajulikana huyu mwanamke huyu mwanaume.

“Mwanadamu yoyote anayeumbwa na Mungu ana karama ambayo amempa, hivyo nataka niseme tusidharauliane. Kila mwanadamu akijengewa uwezo anaweza kufanya chochote kile, tuendeleze watoto wetu wa kike na wa kiume wote wanaweza kufanya maajabu katika nchi na ulimwengu huu,” amesema

Katika mahojiano hayo yaliyorushwa moja kwa moja na Mwananchi Digital, Rais Samia ameweka wazi kuwa utotoni alikuwa na ndoto ya kuwa mhudumu wa ndege,  lakini ilikatishwa na baba yake ambaye alimtaka kurithi kazi yake ya ualimu.

“Wakati nasoma shule ya msingi sikuwahi kuwaza nitakuwa nani ila nilipofika sekondari nikaanza kuvutiwa na kazi ya uhudumu wa ndege hasa nilipokuwa nawaona wafanyakazi wa Shirika la Ndege la DRC nikajikuta natamani kuwa kama wale.

“Baba yangu alikuwa mwalimu na alitamani mtoto wake mmoja arithi kazi yake, akanipangia mimi. Nilienda hadi chuo lakini nikatoroka na kurejea nyumbani, Nilikaa miezi mitatu ndipo nikapata kazi,” amesema Rais Samia aliyezaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.


Maana ya ukinizingua

Kuhusu kauli yake aliyoitoa kwa mawaziri wake ya: ‘Ukinizingua nitakuzingua’, amesema aliitoa kwa ajili ya kuongeza uchapakazi miongoni mwao, huku akibainisha wengi wao ni  vijana ambao anaweza kuwazaa.

Amesema wanaokwenda visivyo amekuwa akiwaweka kando kupitia taarifa kwa umma.

“Mimi ni mama, kwa bahati nzuri wengi niliowateua naweza kuwazaa na ndiyo maana nikapata uthubutu wa kuwaambia ‘ukinizingua tunazinguana’, amesema.