Mechi sita kitanzi kigumu Mtibwa Sugar

Muktasari:

  • Michezo minne ambayo Mtibwa Sugar imebakiza ugenini ni dhidi ya JKT Tanzania, Simba, Mashujaa na Ihefu.

Takwimu mbaya ugenini msimu huu na ubora wa vikosi vya Yanga na Azam FC vinaifanya Mtibwa Sugar iwe na mechi sita za moto kati ya nane ilizobakiza msimu huu ili iweze kujinusuru na janga kushuka daraja linaloinyemelea.

Timu hiyo inayoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 17 ambazo ni sita pungufu ya zile za timu zilizopo nafasi ya 13 na 14 ambazo angalau haziwezi kushuka daraja moja kwa moja imebakiza mechi nne nyumbani huku pia ikiwa na michezo minne ambayo itacheza ugenini.

Mechi nne za ugenini ndizo zinaonekana mtihani mgumu kwa Mtibwa Sugar kutokana na historia ya kutofanya vizuri pindi inapokuwa ugenini kulinganisha na nyumbani msimu huu.

Katika mechi 11 ilizocheza ugenini kwenye Ligi Kuu hadi sasa, Mtibwa Sugar imevuna pointi sita tu huku ikipoteza 27 ambapo imepata ushindi mara moja, kutoka sare tatu na kupoteza mechi nane, ikifunga mabao tisa tu na yenyewe imeruhusu mabao 20.

Ni tofauti na uwanja wao wa nyumbani wa Manungu Complex ambao katika mechi 11 zilizochezwa hapo, wamevuna pointi 12, wakishinda mechi tatu, sare mbili na wamepoteza mechi sita huku wakifunga mabao 13 na kufungwa mabao 17.

Michezo minne ambayo Mtibwa Sugar imebakiza ugenini ni dhidi ya JKT Tanzania, Simba, Mashujaa na Ihefu.

Uwepo wa mechi nne za nyumbani ungeweza kuishusha presha Mtibwa Sugar lakini uwepo wa mechi mbili ngumu dhidi ya timu zinazoshika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi huku zikiwa na mwendelezo wa kufanya vizuri, Yanga na Azam FC hapana shaka unailazimisha Mtibwa Sugar kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inafanya vyema ili ijiokoe na balaa linaloinyemelea.

Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54, haijapoteza mechi 17 mfululizo za ligi msimu huu tangu ilipofungwa na Namungo FC, Oktoba 27 mwaka jana wakati Yanga ambayo ni kinara wa ligi hiyo kala ya mechi ya jana dhidi ya JKT Tanzania, ilikuwa imepoteza mechi mbili tu kati ya 22 ilizocheza hadi sasa na ilikuwa imeshinda michezo 19.

Mbali na mechi dhidi ya Yanga na Azam, michezo mingine miwili iliyobaki ya Mtibwa Sugar ni dhidi ya Tabora United na Namungo FC.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema kuwa bado wana matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zilizobakia.

"Nafasi tuliyopo sio nzuri lakini pengo la pointi kati yetu na walio juu yetu sio kubwa sana hivyo kama tutapambana na kufanya vizuri kwenye mechi zetu, tuna imani tutasogea na hatutobaki chini.

"Kipindi kama hiki presha inakuwa kubwa hivyo tunajitahidi kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili wawe na utulivu ambao utawafanya wasipoteza umakini kwenye mechi hizo," alisema Katwila.