Yanga Arusha, Azam Mwanza nusu fainali Shirikisho

Muktasari:

  • Yanga imetwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho Tanzania mara tatu sawa na Simba huku Azam FC ikichukua taji hilo mara moja.

Droo ya uamuzi wa kiwanja kipi kitatumiwa na timu zipi katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB imechezeshwa leo ambapo timu za Ihefu, Yanga, Azam na Coastal Union zimejua mechi zao za nusu fainali zitachezwa wapi. Mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya mashindano hayo utachezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mei 18 ambao utazikutanisha Coastal Union kuanzia saa 9.30 alasiri. Kesho yake kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, Arusha, nusu fainali ya pili ya mashindano hayo itachezwa ikizikutanisha Ihefu na Yanga. Timu zitakazofanikiwa kuingia hatua ya fainali, zinatarajiwa kukutana katika Uwanja wa Kwaraa uliopo Babati, Juni 3 kusaka bingwa wa taji la mashindano hayo msimu huu. Mabingwa watetezi wa taji hilo, Yanga waliingia hatua ya fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United kwenye hatua ya robo fainali wakati Ihefu ilipenya baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Mashujaa ya Kigoma baada ya timu hizo kumaliza kwa matokeo ya sare tasa katika dakika 90 za mchezo. Coastal Union iliingia hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Geita Gold wakati huo Azam FC ikiingia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Namungo FC. Katika timu nne zilizoingia hatua ya fainali, Ihefu na Coastal Union bado hazijaonja ladha ya ubingwa wa mashindano hayo wakati Yanga na Azam kila moja imeshawahi kutwaa taji kwa nyakati tofauti. Wakati Ihefu na Coastal Union kila moja ikisaka taji la kwanza la mashindano hayo, Yanga yenyewe itakuwa inasaka ubingwa wa nne huku Azam ikipigania kutwaa taji hilo kwa mara ya pili.