Ligi ya Mabingwa: Wakubwa wanapambana uwanjani

Arsenal itapaswa kujitafuta yenyewe kabla ya mambo hayatibuka na kujikuta wakipoteza nafasi za kubeba mataji mengi ndani ya wiki moja wakati usiku wa leo, Jumatano itakapokuwa Allianz Arena kukipiga na Bayern Munich kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wikiendi iliyopita, Arsenal ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Aston Villa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England na hivyo kuenguliwa kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England, ikiwapisha Manchester City na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kukwama kwenye mbio za kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu.

Usiku wa leo itakuwa na kazi ya kumalizana na Bayern ili kufahamu hatima yao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Emirates wiki moja iliyopita ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2. Arsenal inatafuta nafasi ya kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009.

Lakini, kwenye mechi hiyo kocha Mikel Arteta anaweza kukosa huduma ya mastaa wake kadhaa, huku akiwa na kazi ya kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji hao baada ya kipigo cha Aston Villa, Jumapili iliyopita.

Kwenye Ligi Kuu England kwa sasa Arsenal imeachwa pointi mbili na vinara Man City, lakini kwa usiku wa leo kasheshe linalowakabili ni kumenyana na Bayern, ambayo pia matumaini ya ubingwa kwao yamebaki kwenye mikikimikiki hiyo ya Ulaya baada ya Bayern Leverkusen kutwaa ubingwa wa Bundesliga.

Wasiwasi mkubwa kwa Arsenal ni kwamba huenda ikakosa huduma ya wakali wake kadhaa, Bukayo Saka, Martin Odegaard, Gabriel, Gabriel Jesus na Jurrien Timber kutokana na kuwa majeraha na kufanya mechi hiyo ya ugenini kuwa na uzito mkubwa kwao.

Ukiweka kando kipute hicho cha Allianz Arena, mechi nyingine ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye hatua ya robo fainali itakuwa huko Etihad, wakati mabingwa watetezi Manchester City watakapowakaribisha mabingwa wa kihistoria, Real Madrid. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Bernabeu, miamba hiyo ilifungana mabao 3-3 na sasa kusubiri kuona ni nani atapenya na kutinga hatua ya nne bora msimu huu.

Mchezo wa kwanza ulishuhudia mabao sita yakiingia wavuni na bado mashabiki wanaamini huu wa leo utakuwa na idadi kubwa ya mabao, huku kazi kubwa wakiachiwa mabeki wa Madrid kupambana na Erling Haaland wa Man City.

City inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa haijapoteza kwenye michezo 27 kwenye mashindano yote, kama itashinda leo itakuwa imecheza michezo 42 kwenye Uwanja wake wa Etihad bila kupoteza na kufikia rekodi ya mwaka 1921.

Hata hivyo, Madrid imefanikiwa kuvuka mara mbili tu kati ya 10 ambazo imecheza mchezo wa kwanza wa nusu fainali na kumaliza kwa sare na zote ilikuwa dhidi ya Manchester United mwaka 1999-00 na 2012-13