Robo fainali Uefa... Mechi za wababe zinapigwa leo

London, England. Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali, inatarajiwa kuanza kuchezwa leo Jumanne ambapo kutakuwa na mechi mbili saa 4:00 usiku, ambazo ni Arsenal dhidi ya Bayern Munich itapigwa Uwanja wa Emirates, huku Real Madrid ikiwa mwenyeji wa Manchester City kunako Dimba la Santiago Bernabeu.


ARSENAL VS BAYERN
Ni mchezo ambao wengi wanasubiri kuona kama Arsenal italipa kisasi kwa Bayern baada ya kunyanyaswa mechi mbili za mwisho walizokutana kwenye michuano hiyo msimu wa 2016/17, ambapo ndiyo Arsenal ilikuwa mwisho kushiriki kabla ya kurejea tena msimu huu.

Matokeo ya jumla ya mabao 10-2 waliyopata Bayern dhidi ya Arsenal, ndiyo yanazungumzwa zaidi kipindi hiki kuelekea mchezo wa leo ambapo Arsenal inaonekana kuwa vizuri zaidi ya Bayern. Je, italipa kisasi au rekodi itawabeba Bayern?

Kuelekea mchezo huo, Bayern imepata nafuu baada ya baadhi ya wachezaji wake muhimu waliokuwa majeruhi kuanza mazoezi akiwemo Aleksandar Pavlovic, Kingsley Coman, Leroy Sane, Manuel Neuer na Noussair Mazraoui ambao wote hao walikosekana wikiendi walipochapwa 3-2 na Heidenheim kunako Bundesliga.

Neuer alikosekana katika mechi mbili zilizopita baada ya kusumbuliwa na maumivu ya misuli aliyoyapata wakati akifanya mazoezi na kikosi cha Timu ya Taifa ya Ujerumani. Wakati Neuer alipokosekana, Sven Ulreich alichukua nafasi yake golini.
Kurejea kwa Neuer, kunashusha presha kwa Bayern baada ya hapo awali, kumkosa kwa muda mrefu mwanzoni mwa msimu huu kutokana na majeraha.

Kwa upande wa Arsenal, wanaonekana kuwa kamili, huku mchezaji ambaye bado hajawa fiti moja kwa moja, ni Jurien Timber ambaye aliumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu dhidi ya Man City, mpaka leo hajacheza tena.

Fomu ya Arsenal katika mechi tano zilizopita, ndiyo inawapa jeuri zaidi vijana hao wa Mikel Arteta kwani katika michuano yote, wameshinda zote zikiwemo nne za Premier na moja ya UEFA dhidi ya FC Porto ilipoiondosha hatua ya 16 bora kwa penalti 4-2.

Bayern wao mechi tano zilizopita katika michuano yote, imeshinda tatu na kupoteza mbili ambazo zote ni za hivi karibuni ilipofungwa mfululizo ndani ya Bundesliga dhidi ya Heidenheim (3-2) ugenini na Borussia Dortmund (0-2) nyumbani.

Ukija kuangalia wawili hao walivyokutana katika mechi 12 za UEFA, Bayern ni wababe wakishinda 7, sare 2, huku Arsenal wakishinda 3.

Ubabe wa Bayern pia upo katika kufunga mabao wakiwa nayo 27, Arsenal 13. Bayern imeshinda mataji 6 ya UEFA, Arsenal haina kitu.


MADRID VS MAN CITY
Huu ni mchezo unaowakutanisha mabingwa watetezi, Man City dhidi ya mabingwa wa kihistoria, Real Madrid.
Rekodi zinaonesha kwamba, timu hizo zimekutana mara 10 katika michuano hii, Man City inaongoza kwa kushinda mechi nyingi (4) na kufunga mabao 17, huku ikibeba taji moja msimu uliopita lililokuwa likishikiliwa na Madrid.

Kwa upande wa Madrid, imeshinda mechi 3, imefunga mabao 14, ikishinda mataji 14 na ndiyo timu yenye mataji mengi ndani ya michuano hiyo.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mchezo wa nusu fainali msimu uliopita, Man City ikashinda kwa jumla ya mabao 5-1, baada ya mchezo wa kwanza pale Bernabeu kumalizika kwa sare ya 1-1, kule Etihad, Man City ikashinda 4-0. Ikaenda fainali kubeba kombe lao la kwanza la michuano hiyo.

Katika mchezo wao huo wa leo, kila upande unapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa, kwani kuna baadhi ya wachezaji wakionyeshwa kadi ya njano tu, basi watakosekana mchezo wa marudiano.

Man City inayonolewa na Pep Guardiola, beki wake Ruben Dias ndiye anapaswa kuwa muangalifu zaidi asionyeshwe kadi ya njano leo, lakini wapinzani wao Madrid wanaofundishwa na Carlo Ancelotti, wana wachezaji wengi walio kwenye hatari ambao ni Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, Aurelien Tchouameni na Vinicius Junior, atakayeonyeshwa kadi ya njano, imekula kwake.
 
MATOKEO ARSENAL VS BAYERN

Arsenal 1-5 Bayern
Bayern    5-1 Arsenal
Bayern    5-1 Arsenal
Arsenal    2-0 Bayern
Bayern    1-1 Arsenal
Arsenal    0-2 Bayern
Bayern    0-2 Arsenal
Arsenal    1-3 Bayern
Arsenal    1-0 Bayern
Bayern    3-1 Arsenal
Bayern    1-0 Arsenal
Arsenal    2-2 Bayern


MATOKEO MADRID VS MAN CITY

Man City 4-0 Madrid
Madrid     1-1 Man City
Madrid     3-1 Man City
Man City 4-3 Madrid
Man City 2-1 Madrid
Madrid     1-2 Man City
Madrid     1-0 Man City
Man City 0-0 Madrid
Man City 1-1 Madrid
Madrid     3-2 Man City