Jumamosi ndiyo inaongoza kwa Dabi ya Kariakoo

Muktasari:

  • Ni mechi ya kisasi hivyo ndio unaweza kusema baada ya watani hao wa jadi kutarajiwa kukutana tayari kwa kumaliza msimu wa 2023/24 baada ya mzunguko wa kwanza Simba ikiwa nyumbani kukubali kichapo cha mabao 5-1.

Yanga inatarajia kuwa mwenyeji wa Simba mchezo ambao utakuwa ni mchezo wa 112 kwenye Ligi Kuu wikiendi hii tangu Jumatatu ya Juni 7, 1965. Yanga ilishinda bao 5-1 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza.

Ni mechi ya kisasi hivyo ndio unaweza kusema baada ya watani hao wa jadi kukutana tayari kwa kumaliza msimu wa 2023/24 baada ya mzunguko wa kwanza Simba ikiwa nyumbani kukubali kichapo hicho.

Miamba hawa wamekutana mara 12 ndani ya Aprili kuanzia mwaka 1965 lakini kati ya hizo sita zimekutana Jumapili huku Simba ikishinda mara mbili, sare tatu na ikipoteza mara moja.

Mechi inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa pande zote mbili inatarajiwa kupigwa Jumamosi swali ni je? Nani kuibuka mwamba na kuendelea kuandika rekodi ya kuwa kinara wa kumfunga mwenzake huku rekodi ikionyesha Yanga inaongoza.
Mwananchi linakuletea makala katika namba zikionyesha walivyokutana na matokeo waliyo yapata.


111

Kabla ya mchezo wa leo miamba hiyo ya soka Tanzania imekutana mara 111 na katika mechi hizo Yanga imekuwa kinara wa kushinda michezo mingi zaidi ya mtani wake Simba.

Yanga imeshinda mara 39 huku ikimuacha Simba kwenye michezo saba kwani mtani wake kashinda mara 32 tu na kwenye mechi hizo 111 sare ni 40.


118

Ni mabao waliyofunga Yanga kwenye mechi 111 walizokutana na Simba wamefunga mabao hayo huku wakiwaacha mbali watani zao ambao wao wametupia mabao 104 kambani.


40

Ni mechi ambayo watani hao wa jadi walikosa matokeo na kujikuta wanagawana pointi moja moja baada ya sare na suluhu kwenye mechi 111 walizocheza nyumbani na ugenini.


60

Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara nyingi zaidi (60) siku ya Jumamosi katika dabi 111 walizocheza, Jumatatu zimekutana mara tatu na Jumanne mara mbili.

Lakini, Jumatano timu hizo zimekutana mara saba, Alhamisi mara mbili, Ijumaa mara moja na Jumapili zimekutana mara 36 na hata mchezo uliopita Yanga akishinda mabao 5-1 mchezi ulipigwa pia siku ya Jumapili.

Katika michezo hiyo 36 ya Jumapili, Simba imeshinda michezo tisa, ikipoteza michezo saba na sare 19, kuonyesha kuwa ni siku ambayo imekuwa na bahati kwao kulinganisha na Yanga.

Hata hivyo, Yanga ndio timu ya kwanza kushinda mchezo wa Jumapili baada ya kuichapa Simba bao 1-0 Juni 18,1972 bao lililofungwa na Leonard Chitete.

Katika michezo 36 michezo minne ilichezwa nje ya Dar es Salaam, ambapo dabi ya kwanza ilipigwa Septemba 30, 2001 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 bao la Joseph Kaniki (Simba) na Sekilojo Chambua wa Yanga.

Dabi ya pili nje ya Dar es Salaam ilichezwa Aprili 17, 2005 na Simba kushinda 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro mabao ya Simba yakifungwa na Nurdin Msiga pamoja na Athumani Machupa huku lile la Yanga akifunga, Aaron Nyanda. Mchezo wa tatu ulichezwa Agosti 21, 2005 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Simba kushinda 2-0 mabao yakiwekwa kambani na Nico Nyagawa dakika ya 22 na 56.

Kipute cha mwisho cha dabi cha Ligi Kuu kuchezwa nje ya Dar es Salaam ilikuwa Julai 8, 2007 wakati timu hizo zikigawana alama baada ya sare ya bao 1-1 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu timu hizo kukutana Uwanja wa Taifa (Mkapa) ilikuwa Oktoba 26, 2008 na Simba kupoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Ben Mwalala dakika ya 15.

Katika michezo 35, Simba imekuwa mwenyeji michezo 21 wakati Yanga ikiwa mwenyeji michezo 15 na mchezo huu Simba ndio mwenyeji kwa mara nyingine.
Moja ya dabi inayokumbukwa zaidi ni pamoja na ile ya Jumapili ya Mei 6, 2012 Simba ikishinda 5-0 kwa mabao ya Emmanuel Okwi aliyefunga mawili, Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Felix Sunzu.

Wakati Yanga wakichapwa mabao 5-0 na mchezo kupigwa Jumapili watani wao Yanga na wao wamelipa kichapo hicho utofauti ukiwa ni mwaka na mwezi kwani wao pia waliitumia siku ya Jumapili Novemba 5 kuwafunga mabao 5-1.