Dabi yazigawa familia za mastaa

Presha ya dabi inazidi kupanda na kushuka huku saa zikiwa zinahesabiki kabla ya watani hao Simba na Yanga kushuka uwanjani saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikielezwa pambano hilo limewagawanya mastaa wa timu hiyo na baadhi ya wazazi wao kutokana na utani wa jadi.

Ipo hivi. Wakati mastaa wakipambana kujiweka freshi tayari kwa mchezo huo ambao kwa Simba itataka kulipa kisasi baada ya mechi iliyopita iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana kufungwa mabao 5-1 ikiwa wenyeji wa mchezo, huku Yanga ikitaka kuendeleza ilipoishia katika harakati za kuwania ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo, lakini baadhi ya mastaa wa timu hizo na wazazi wao wanatofautiana ushabiki na leo kazi itakuwepo.

Kuna mastaa wanaokipiga Simba na Yanga wazazi wao wana ushabiki tofauti na wao, hivyo kuibua presha mpya nje ya uwanja kutokana na namna kila mmoja anapambana kuomba timu ipate matokeo.

Kipa wa Simba, Aishi Manula licha ya kumtumikia Mnyama, lakini familia yake ni wanazi wa Yanga, swali ni je, wataungana na kipa huyo kuiombea dua Simba ipate matokeo au na wao watataka timu wanayoishabiki ishinde?

Ukiachana na Manula, kipa Hussein Abel, mama yake ni mnazi wa Yanga na amekiri kuiombea timu yake ishinde huku akitoa wazo la endapo mwanaye atakaa langoni basi dakika 90 ziishe kwa sare.

Kwa upande wa nahodha wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala', pia baba yake mzazi ni mnazi wa timu tofauti na inayomuingizia kipato mwanaye kwani anaishabikia Yanga.

Beki kitasa wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca' pia anakosa sapoti kutoka kwa mama yake kwani yeye ni shabiki wa Simba huku sapoti ikibaki kwa baba yake ambaye ni mwanachama wa Yanga.

Mama wa Bacca, Mwajina Makame amekiri asingependa Simba ipigwe tena 5-1 bali ishinde, lakini hofu yake kama mwanae anacheza ni bora Yanga ifungwe bao 1-0 au kuisha kwa sare ili kumweka salama mchezaji huyo, huku baba mtu, Abdallah Hamad amesema yeye ni shabiki damu wa Yanga na kuweka bayana kwa sasa anachokitamani ni kuona kikosi anachokishabikia kinaibuka kidedea kwa mara nyingine.

“Tunachotaka ni kuona Simba, inapigwa tena kama mchezo uliopita na sasa kiwe kipigo kikubwa zaidi. Hata kama wamekuja Zanzibar kujifungia, lakini bado tuna kikosi bora kuliko wao, hivyo kipigo kiko pale pale,” amesema baba wa Bacca.
Kiungo Jonas Mkude awali alikuwa anakipiga Simba na alikuwa timu moja na mama yake lakini baada ya kuamia kwa watani zake Yanga imekuwa tofauti kwani mama yake bado ni mnazi wa Simba.