Uwazi ni msingi wa utawala bora

Uwazi katika sera za uongozi ni nyenzo muhimu ya utawala bora. Tumepitia awamu mbalimbali zilizokuwa zikinadi kaulimbiu tofauti japo zilikuwa na uficho katika baadhi ya mambo ndani ya uongozi wake. Tulipitia “Uhuru na Kazi” ya Mwalimu Nyerere, “Ruksa” ya Mzee Mwinyi, “Ukweli na Uwazi” ya Mheshimiwa Mkapa, “Maisha Bora kwa kila Mtanzania” ya Mheshimiwa Kikwete, “Hapa Kazi tu” ya JPM na sasa hii ya kwako “Kazi iendelee”.

Naweza kukiri kwamba usiri wa baadhi ya mambo si jambo baya kwenye uongozi, japo kuna baadhi ya mambo yanaweza kusababisha kuvunjika kwa imani ya wanaoongozwa. Hili linaweza kutokea pale ambapo wananchi watahisi viongozi wakitumia usiri ili kujinufaisha wenyewe na kuwanyima haki zao za msingi. Wananchi wanaamini kuwa na haki ya kujulishwa kila jambo kutoka kwa viongozi wao.
Hili ni jambo sahihi ingawaje kila uongozi una mitazamo tofauti juu yake.

Kwamba uongozi hauwezi kuachia mageuzi bora yatakayopiku sera anazozisimamia, yaani maono ya wengine yasiende tofauti na maono ya Serikali husika. Hii ina maana kwamba mtu mwenye njia bora zinazoweza kufanya vizuri kwenye uongozi wake, lakini kwa vile sera hizo zinatofautiana na dira ya uongozi uliopo, basi hawezi kuungwa mkono kirahisi.

Viongozi wengi wa siasa wanajisahau na kuamini kuwa wao ni viongozi wa imani. Ni ukweli kuwa uongozi ni imani kwa jinsi inavyoweza kuwavusha watu wengi katika wakati mmoja, lakini pia unaweza kuangamiza mamilioni ya roho za wasio na hatia kwa wakati huohuo. Lakini kitendo cha wanasiasa kuamini kwamba wanaweza kuingilia imani za watu kinawapa kiburi kinachoweza kuvuruga nia na malengo ya siasa.

Wapo wanaoamini mpaka leo kwamba Mwalimu Nyerere alimsusia nchi Ali Hassan Mwinyi baada ya shinikizo la mabepari wa Kimagharibi. Kwamba aliachia aidha kwa woga wa kuondoka vibaya au hasira ya kupoteza dira yake. Lakini wapo wanaoamini kwamba Mwalimu aliiona taswira ya maisha yajayo, na akaamua kuyapisha kistaaarabu. Kama wanaodhani hivyo watakuwa sawa, basi tutamwita Mwalimu kuwa Nabii wa kizazi chetu.

Nasema hivi kwa sababu kuna jambo la kihistoria lilitukia katika uelekeo wa uchaguzi wa mfumo utakaoinufaisha Tanzania. Wakati Tume ya Nyalali ilipofanya mchakato wa kujua njia bora ya kufuata kati ya utawala wa chama kimoja uliokuwepo au mpya wa vyana vingi.

Inasemekana Rais aliyekuwepo madarakani, Mwinyi alikwenda kujadiliana na Mwalimu baada ya matokeo yaliyotegemewa na wote: Mfumo wa chama kimoja.
Wawili hao wakakubaliana tofauti na Watanzania wote waliopiga kura za kuunga mkono mfumo wa chama kimoja. Na hata na wenzao waliopiga kura za kutaka mfumo wa vyama vingi japokuwa walibaki na imani ya kushindwa. Wazee hawa waliamua kuwapa ushindi wachache waliohusudu mfumo wa vyama vingi na kuachia Taifa lielekee kwenye demokrasia na soko huria, ambapo watu na taasisi binafsi walikamata nyundo zilizodhibiti ukiritimba wa Serikali.

Pamoja na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuingia na matatizo ya rushwa na uhujumu wa uchumi, tulijifunza jinsi viongozi wetu wanavyopaswa kuwa na subira.

Wanasema Mji wa Roma haukujengwa kwa siku moja, na hivi ndivyo mfumo huu mpya ulivyoingia kwa taratibu ukijitetea kuwa si mfumo wa maangamizi. Lakini ukweli ulidhihirika kwa baadhi ya viongozi kutaka kuuhodhi mfumo wa soko huria.

Lakini kubwa zaidi ni lile la viongozi hawa wakuu kuona kwamba huu ndio wakati ambao mabadiliko yalitakiwa kufanyika kabla ya watu kuondoa imani kwenye chama chao kimoja. Iwapo wangeruhusu watu wauchoke mfumo wa utawala waliouzoea (wa chama kimoja), wangeyadai mabadiliko kwenda kwenye mfumo mwingine kwa nguvu.

Hali kama hiyo imewahi kutukia kwenye nchi nyingi hapa Afrika na hata nje ya bara hili. Mara zote watu wanapodai mabadiliko kwa nguvu hukutana na pingamizi kutoka kwa wale wasiokubaliana na mabadiliko. Wataka mabadiliko huamini kwamba wanadai haki yao inayodhulumiwa, wakati wapinga mabadiliko wanaogopa kuadhibiwa baada ya kufanya madudu kwenye mamlaka zao.

Huu ni ubunifu wa kisiasa wa wazee hawa, ulioliingiza Taifa kwenye mabadiliko bila athari kubwa za kisiasa. Waliona jinsi dunia ilivyokuwa ikiondokana na ukiritimba katika baadhi ya mambo yaliyowezekana kuendeshwa na sekta binafsi. Walishuhudia maendeleo ya sekta hizo yakipiku ukiritimba wa Serikali zilizojaa rushwa na ufisadi uliofanywa na viongozi wasio na weledi.

Serikali yako imefanya makubwa katika uhuru wa kupashana habari, lakini yapo baadhi ya mambo yanayotakiwa kurekebishwa. Uhuru wa kutoa habari zisizo na vyanzo madhubuti udhibitiwe, lakini Serikali ijibu maswali ya wananchi na waandishi bila ubaguzi. Wanapotaka kujua viongozi wao wako wapi, wana hali gani na wanafanya nini, wasionekane kuwa wachochezi.

Sitaki kurudia taharuki mojamoja zilizowahi kujitengeneza baada ya ukali wa Serikali kwa wananchi wake.

Kama nilivyosema, usiri kwenye baadhi ya mambo si dhambi, lakini usiri kwenye haki za msingi sio jambo zuri.

Watu wabaya wanaweza kutumia nyufa ndogondogo kupenyeza taharuki ili kuondoa imani ya watu juu ya Serikali yao, na kuifanya nchi isiwe salama.