Mama magugu yasihamishiwe kwenye tuta jipya ni hatari

Mtu yeyote anayepambana na maradhi hataki kuamini kuwa hayo ni maradhi yake, bali huyaona kama kitu kilichomvamia mwilini na hakina budi kuondolewa. Ndiyo maana hatumtakii nafuu katika “maradhi yake”, ila katika maradhi yanayomsibu. Madaktari wakifanya upasuaji huondoa ugonjwa na kuuzika. Hawaondoi jipu la usoni na kulipandikiza mguuni kwa sababu jipu si sehemu ya mwili wa binadamu.

Kiimani tunaona ni bora mtu apoteze kiungo chake kimoja kuliko kuangamia jumla. Vitabu vinafundisha ni heri mtu aukate mkono wake unaomshawishi kutenda dhambi, na si kuuachia umzamishe kwenye jehanamu ya moto. Tena kuna usemi uliochukuliwa vizuri na wapambanaji wetu: “Ni bora mmoja afe kwa ajili ya wengi”. Mwanajeshi akifa vitani katika ukombozi wa Taifa anatukuzwa, kwani amekufa kishujaa.

Mifano hii inatukumbusha kuishi kwa uzalendo. Tunaamini kwamba binadamu wote ni sawa, na kila mmoja anastahili heshima. Usawa ni haki ya msingi kibinadamu, kikatiba na hata kiimani. Hakuna aliyemzidi binadamu mwenzie hata kama ana mwili mkubwa, nguvu, akili au uwezo wa ziada. Pia, haki inatengua tofauti ya madaraja yanayoendekeza rangi, ukabila, udini, utaifa na itikadi.

Tanzania ni moja ya mataifa yanayozingatia haki kwa umakini mkubwa. Kila Mtanzania anayo haki ya kuchagua viongozi au kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa njia ya demokrasia. Pia, ana haki ya kupandishwa cheo pamoja na kuongezwa mshahara kazini kwake. Lakini yote hayo yanazingatia juhudi, maarifa na uzalendo wake kitaifa. Kiongozi asiye mzalendo atakuwa mbinafsi na mwenye kujali maslahi yake, si ya Taifa.

Mwalimu Nyerere alisema urafiki usiwe kigezo cha kulindana kwenye uongozi na utumishi wa umma. Aliasa kwamba hata kama ni rafiki yetu kiasi cha kutufanya tusifungue shampeni kabla hajafika, ni bora abaki kuwa rafiki. Ni hatari sana kumpa dhamana ya kuongoza watu kwa sababu ya urafiki tu. Ni lazima kiongozi aongozwe na Katiba na azingatie viapo vyake ili akikengeuka tupate kumshtaki.

Hapa nchini kumekuwa na kawaida ya kuendekeza urafiki usio na tija kwa baadhi ya viongozi. Wakati mwingine mazoea haya huja kwa kulinda maslahi ya chama au taasisi; kwamba tukimuumbua fulani tutaonekana na sisi ni “walewale”.

Inawezekana ubovu wa kiongozi huyo ulionekana tangu awali, lakini kwa jinsi alivyo na ushawishi kwa wananchi anaweza kuchukuliwa kama nyota kwenye chama au taasisi.

Lakini wakati mwingine mazoea hujenga tabia, na tabia huwa kama ngozi isiyoweza kuvuliwa kirahisi. Mtu huyo anaweza kuuficha ubovu wake katika muda fulani, lakini muda utakapojiri jeuri yake itajitokeza dhahiri atake asitake. Ndipo taasisi au chama kilichompa dhamana kitaanza kujitafakari namna ya kuondokana naye. Kumbuka ni mtu mwenye ushawishi kwa watu wengi.

Jambo la kusikitisha, kiongozi huyo atahamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine. Ama ni kwa sababu wanaombeba wanaficha ukweli kwamba walimkuza wakijua kwamba, huyo ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka, au kwa kumlipa fadhila baada ya kuwafanyia kazi ya kuwaingiza wananchi kwenye mkenge.

Tabia ya kumhamishia kiongozi asiyefaa eneo jingine ni sawa na kupalilia tuta, kisha kuyahamishia magugu kwenye tuta jingine. Hii inaleta kasoro kwenye tuta hilo lisiweze kumea mazao bora. Kiongozi mbovu ataingilia ufanisi wa kituo kipya anachohamishiwa na kuwarudisha nyuma wananchi wanaopambana kujikwamua. Na kwa kutumia uhusiano wake na wakubwa, ndio atauvuruga mkoa au kanda nzima.

Kim Il Sung aliwahi kusema: “Ukiwa na viongozi wenye maarifa, mnaweza kuyageuza hata mawe yakawa mavazi, lakini mkiwa na viongozi wabovu itakuwa kinyume chake; hata mkipewa chakula, mtakufa kwa njaa kwa sababu mtashindwa kupika”. Alikuwa na maana kwamba kiongozi mbovu huwa maangamizi kwenye Taifa.

Wapo viongozi wabovu wanaolalamikiwa kufisadi kwenye masuala ya ardhi. Waligawa maeneo ya wazi, wakajimilikisha maeneo ya raia kimabavu, wakauza maeneo yaliyohifadhiwa na Serikali kwa ajili ya huduma za jamii, lakini badala ya kuchukuliwa hatua, wamehamishiwa mikoa mingine pengine kwa sababu nilizozitaja pale mwanzo. Kwa mfano mkoani Mwanza kuna tuhuma za wabadhirifu kuhamishiwa Dar es Salaam na mikoa mingine.

Hasidi haachi kuhusudu mpaka siku ya kiama. Tusitegemee kiongozi huyu ajisafishe na kuwa muadilifu baada ya kuhamishwa. Jambo la hatari ni kwamba pengine kule alikopelekwa hakuna matatizo aliyoyafanya huko alikotokea, basi ni wazi atawavuruga na kuwarudisha nyuma kimaendeleo. Ndiyo maana nikasema kumhamishia kiongozi asiyefaa kwenye eneo jingine la kazi, ni sawa na kuhamishia magugu kwenda kwenye tuta lingine.

Zaidi ya kufanya madudu kwenye chaka jipya, kiongozi huyo atawashawishi wengine waadilifu kukengeuka. Pia, atakutana na wabovu wenzie waliokuwa hawana nafasi ya kuharibu. Wanasema “ndege wa rangi moja huruka pamoja” na “umoja ni nguvu”, hivyo kwa pamoja wataiendeleza dhambi yao na kuuathiri mkoa mzima.

Watu hawa wasionewe haya hata kidogo. Rafiki zetu Wachina waliondokana na umasikini baada ya kutekeleza sera ya kuwajibika bila kupepesa macho, sisi bado tunachekeleana kwa sababu za unafiki na maslahi ya kibinafsi. Kunguru hawa wasiachwe, waadabishwe wao pamoja na kunguru wenzao wanaowalinda!