Zaidi ya Watanzania milioni moja wana matatizo ya macho

Muktasari:

  • Wakati Shirika la Christofeel Blinden Mission (CBM) likisaidia uboreshaji wa huduma za macho, Tanzania bado inakabiliwa na tatizo hilo ambapo inakadiriwa watu milioni 1.86 wanakabiliwa na changamoto ya kuona kwa viwango vya kati na juu.

Dodoma. Watanzania 620,000 wanakadiriwa kuwa na tatizo la kutoona huku watu wenye matatizo ya kuona kwa viwango vya kati na vya juu wakikadiriwa kuwa milioni 1.86.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe leo Ijumaa Machi 17, 2023 wakati wa uzinduzi wa miradi ya afya ya macho kwa ufadhili wa Shirika la Christofell Blinden Mission (CBM).

Amesema sababu za changamoto hiyo ni mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho unaorekebishika kwa miwani, shinikizo la macho na madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye macho.

“Zaidi ya asilimia 90 ya matatizo haya yanatibika au kuepukika,”amesema Dk Shekilaghe ambaye amewakilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa wizara hiyo, Ziada Sellah.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Dk Alex Makalla katika mwaka 2022 ni watu 8,805 tu waliofikiwa kwenye vituo vya tiba kati ya watu 205,000 waliotakiwa kuonwa kila mwaka kulingana na makadirio ya ukubwa wa matatizo ya macho.

Mkurugenzi wa CBM, Nesia Mahenge amesema shirika lake limetoa Sh1.47 bilioni kwa ajili ya kugharamikia mfumo wa huduma za macho na huduma jumuishi za macho mkoani Lindi.

“Ombi langu moja kwa Wizara ya Afya pamoja na hii miradi kutekelezeka kwa miaka mitatu tutamani sana kuundwa kwa kamati tendaji ambayo itakuwa na wajumbe kutoka ngazi za juu za wizara ambayo itakutana angalau mara mbili kwa mwaka kujadili mradi,” amesema.

Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Dk Bernadetha Shilio amesema kumekuwa na chanagmoto ya raslimali fedha kwa ajili ya uratibu na huduma za macho katika ngazi zote.

“Hii inachangia kuzorota kwa utekelezaji wa mikakati ya mpango na kutofikiwa kwa malengo tuliyoiwekea,” amesema Dk Shilio.