Wawili mbaroni tuhuma za kuendesha mikopo ‘kausha damu’ Dodoma

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC), Theopista Mallya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo.
Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Dodoma kwa kuendesha mikopo ya kausha damu

Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia wafanyabiashara wawili kwa tuhuma za kuendesha mikopo ya ‘kausha damu’ bila kibali.

Wakopaji wanatakiwa kurejesha riba ya mkopo waliyochukua kati ya asilimia 20 hadi 40 huku riba iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni asilimia 3.5.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Mei 8, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC), Theopista Mallya wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Kamanda Theopista amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya polisi kufanya operesheni, misako na doria kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha Machi hadi Aprili 2024.

Amewataja waliokamatwa kwa tuhuma za mikopo hiyo ni Adrian Gervas, mfanyakazi wa Kampuni ya Logic Microcredit mali ya Merry Gervas anayeendesha biashara yake maeneo ya Chaduru A Kata ya Tambukareli jijini Dodoma.

Mwingine ni Fatma Ally, mfanyakazi wa Kampuni ya Brown Finance mali ya Pius Mushi ambaye anaendesha biashara yake maeneo ya Makole jirani na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dodoma.

"Watu hawa wamekuwa wakifanya biashara hii kinyume na sheria ambazo zimeweka viwango vya riba anayotakiwa kulipa mkopaji ambayo ni asilimia 3.5 lakini wafanyabiashara hawa wamekuwa wakiwalipisha wakopaji wao kiasi cha asilimia 20 hadi 40 kwa mwezi huku wakiwataka kuwa na majeresho ya kila siku," amesema Kamanda Theopista.

Amesema masharti hayo ya mkopo yamesababisha ugumu wa kulipa na kutengeneza mianya ya dhuluma kwa mali ambazo zinawekwa kama dhamana ya mikopo husika kitendo ambacho ni kinyume na matakwa ya sheria ya watoa huduma ndogo za fedha daraja la 2 ya mwaka 2018.

Kamanda huyo amesema dhamana ya mikopo hiyo zimekuwa ni vitu na mali mbalimbali ambavyo vinamilikiwa na mkopaji kama samani za ndani, vyeti vya shule kwa wanachuo, viwanja, nyumba, pikipiki na magari.

Aidha amesema bado wanawasiliana na BoT kuhusu wakopeshaji wanaotumia mitandao ya simu ili kujua kama wana leseni au la ili kama hawana waanze kuchukua hatua dhidi yao maana kuna wengine wana vibali lakini hawatoi mikopo kama masharti ya vibali yanavyotaka.

"Nawashauri wananchi wafanye kazi kwa bidii hakuna fedha za bure wajiepushe na hawa matapeli," amesema Theopista.

Polisi Dodoma wamewakamata watu hao kipindi ambacho kumekuwa na mjadala mkubwa wa masuala ya kausha damu na hivi karibuni uliibukia bungeni kwa wabunge kuitaka Serikali kuchukua hatua kwani imekuwa tatizo kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema wanamshikilia Asha Kimilo (17), mkazi wa Miyuji jijini Dodoma ambaye alikuwa anashirikiana na wahalifu wengine wawili wakiume kupita pikipiki.

Kamanda amesema Asha na wenzake wawili walikamatwa baada ya kupora pikipiki ambayo mwanamke huyo aliikodi na wakati wanakimbizwa waliitelekeza pikipiki hiyo na kukimbia huku Asha akikamatwa.

Kamanda Theopista amesema wanawashilikia watu 120 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya wizi, kukutwa na misokoto ya bhangi pamoja na kukamatwa na mali za wizi.