Yafahamu mambo 10 yanayosababisha matatizo ya macho

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Fabian Masaga (aliyevaa suti nyeusi) akifafanua jambo kwa umati wa wananchi waliojitokeza kupata huduma za matibabu ya macho katika hospitali hiyo leo kuadhimisha siku ya macho duniani. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

Wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) ya jijini Mwanza wametaja kuvaa miwani ya kusomea bila ushauri wala uthibitisho wa kitaalam na matumizi ya vipodozi vilivyoima muda wake kuwa miongoni mwa mambo 10 yanayochangia matatizo ya macho kwa watu wengi nchini.

Mwanza. Wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) ya jijini Mwanza wametaja kuvaa miwani ya kusomea bila ushauri wala uthibitisho wa kitaalam na matumizi ya vipodozi vilivyoima muda wake kuwa miongoni mwa mambo 10 yanayochangia matatizo ya macho kwa watu wengi nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Macho Duniani yaliyofanyika hospitaini hapo leo Oktoba 12, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Dk Fabian Massaga ametaja matumizi ya kompyuta bila tahadhari, uvutaji wa sigara na kutobadilisha mara kwa mara brashi za kusafishia uso kwa akina mama kuwa sababu nyingine zinazosababisha matatizo ya macho.

“Kutokula vyakula bora vinavyosaidia kurutubisha afya ya macho, kutofanya mazoezi na kutokuwa na utamaduni wa kupima macho mara kwa mara ni sababu nyingine inayosababisha matatizo ya macho,’’ amesema Dk Massaga

Mtaalam huyo ametaja mfumo wa maisha usiowapa watoto fursa ya kucheza ili kusaidia macho yao kuona mbali pia husababisha madhara kwa macho.

‘’Wazazi wawape fursa watoto wao kucheza nje kuwezesha macho yao kuona mbali badala ya kushinda ndani wakichezea simu na kutazama runinga,’’ ameshauri

Ulinzi wa macho

Dk Massaga amewashauri Watanzania kulinda afya ya macho yao kwa kuchukua tahahari wanapofanya shughuli zote za uzalishaji mali katika maeneo ya viwanda, migodini, kilimo na uvuvi.

Mafundi wa kuchomelea vyuma na wafanyakazi maofisini ambao shughuli zao zinahusisha matumizi ya komyuta nao wamtakiwa kuzingatia kanuni ya kulinda afya ya macho wawapo kazini.

"Wanaotumia Kompyuta wafuate kanuni ya 20 20 20 inayoelekeza kutazama umbali wa futi 20 kwa sekunde 20 kila baada ya kufanya kazi kwa dakika 20 mfululizo,’’ ameshauri Dk Massaga

Kuvaa miwani ya kukinga miale ya jua na kuvaa miwani ya kusomea baada ya vipimo na ushauri wa kitaalam ni sharti nyingine inayotajwa kuzingatiwa kulinda afya ya macho.

"Wanaotumia vipodozi wanapaswa kuangalia kwa makini muda wa matumizi na wakumbuke kubadilisha brashi za uso kila mara,’’ amesema

Kula mlo kamili wenye virutubisho vya macho, kufanya mazoezi na kutovuta sigara ni ushauri mwingine wa kitaalam unaosaidia kupunguza matatizo ya macho.

Kuacha kuvuta sigara ambayo utafiti umebainisha kuchangia magonjwa mbalimbali yakiwemo ya macho na kujenga utamaduni wa kupima afya ya macho mara kwa mara ni hatua nyingine inayoshauriwa kulinda afya ya macho.

Wagonjwa 2,500 kwa mwezi

Akitoa taarifa ya ukubwa wa tatizo la macho kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mkuu wa Idara ya Macho Hospitali ya Bugando, Dk Christopher Mwanansao amesema zaidi ya wagonjwa wa macho 2,500 hupokelewa na kutibiwa hospitalini hapo kila mwezi.

Kupitia maadhimisho ya Siku ya Macho duniani, hospitali hiyo imewafanyia upasuaji wa macho wagonjwa 32, miongoni mwao wakiwemo waliokuwa na tatizo la mtoto wa jicho.

‘’Tumetumia maadhimisho haya kutoa elimu kwa umma kuhusu afya ya macho, kumetoa ushauri, kupima presha ya macho na kutoa miwani kwa wenye uhitaji,’’ amesema Dk Mwanansao

Wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Bugando pia wametumia maadhimisho hayo kwa kuwatembelea wafanyakazi wa migodini na viwandani kutoa ushauri na kupima afya ya macho.

Suzana Steven, mkazi wa mjini Bariadi aliyefika hospitali hapo kupata huduma ya uchunguzi wa macho kutokana na tatizo la uoni hafifu ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kutoa huduma bila malipo kwa wananchi kuadhimisha siku ya afya ya macho akisema umetoa fursa kwa wasio na uwezo kiuchumi kupata huduma za kibingwa.

‘’Nashauri wataalam wa afya kutoka hospitali za rufaa kuwatembelea wananchi vijijini kuwafanyia vipimo, kutoa ushauri na tiba badala ya kusubiri hadi siku za maadhimisho,’’ amesema Suzana