Wagonjwa 5,000 wa afya ya akili hutibiwa Bugando kila mwaka

Mkuu wa Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Catherine Magwiza akisisitiza jambo wakati wa kongamano maalum la kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za msingi jijini Mwanza namna ya kubaini na kuepuka tabia zinazochangia maradhi ya afya ya akili. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Baadhi ya viashiria na vishababishi vya tatizo la afya ya akili ni ulevi wa kupindukia, vitendo vya ukatili, mfumo wa maisha, hali ngumu kiuchumi na maisha pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Mwanza. Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya afya na magonjwa ya akili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ya jijini Mwanza imebainika kupokea na kuhudumia wastani wa wagonjwa 5,000 wanaosumbuliwa na tatizo la afya ya akili kila mwaka.

Hayo yamebainika kupitia taarifa ya Mkuu wa Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili Hospitali ya Bugando, Dk Catherine Magwiza wakati wa semina maalum kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za msingi za jijini Mwanza namna ya kutambua na kuepuka tabia zinazochangia tatizo la afya ya akili.

Dk Magwiza amesema watu 500 kati ya watu 5,000 wanaopokelewa na kutibiwa tatizo hilo hospitalini hufika wakiwa katika hatua inayohitaji huduma maalum wa kitabibu ikiwemo kulazwa kwa uangalizi.

Mtaalam huyo ametaja baadhi ya viashiria na vishababishi vya tatizo la afya ya akili kuwa ni ulevi wa kupindukia, vitendo vya ukatili, mfumo wa maisha, hali ngumu kiuchumi na maisha pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

"Kwa bahati mbaya, jamii bado ina uelewa mdogo kuhusu magonjwa ya afya ya akili ndiyo maana Bugando tumeona tutoe elimu kwa jamii kwa kuanza na kundi la watoto," amesema Dk Magwiza huku akishauri jamii kuwawahisha hospitali wote wenye dalili za magonjwa ya akili

Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Maenda Chambuko amewataka wazazi kuwaepusha watoto wao na tabia hatarishi zinazochangia uwepo wa watu wenye tatizo la afya ya akili ndani ya jamii.

"Visa na ugomvi miongozi mwa wazazi mbele ya watoto na vitendo vingine vya ukatili ni miongoni mwa mambo yanayochangia hofu na hatimaye tatizo la afya ya akili kwa watoto. Ni lazima wazazi na walezi tuwalinde watoto wetu,’’ amesema Chambuko

Mkazi wa Bugarika jijini Mwanza, Telesphory Musa ameiomba Serikali kuingiza elimu ya afya ya akili katika mtaala kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu kuwezesha jamii kutambua na kudhibiti viashiria vya magonjwa ya akili katika hatua za awali.

Amesema matukio ya kikatili ikiwemo vitendo vya mauaji na baadhi ya watu kujinyonga ni matokeo ya msongo wa mawazo ambayo ni dalili za za tatizo la afya ya akili.

"Ni vema tuanze kujenga jamii yenye watu wanaotambua na kumudu kukabiliana na matatizo ya afya ya akili kuanzia umri wa utoto hadi utu uzima. Hatuwezi kufanikisha hilo bila elimu kwa umma katika ngazi zote,’’ amesema Telesphory