Watu 100, 000 kutibiwa bure magonjwa ya macho

Daktari wa magonjwa ya macho Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Noel Pastory (kulia) akimchunguza macho mmoja ya wananchi ambao wamejitokeza leo kupata vipimo na matibabu bure katika kliniki ambayo imeendeshwa na hospitali hiyo eneo la Kamanga jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

Fedha hizo zitasaidia kufanya vipimo, matibabu kwa wananchi, kukarabati miundombinu ya kutolea huduma ya macho, kutoa mafunzo, kuwajengea uwezo watoa huduma na kupeleka vifaa vya matibabu ya macho katika vituo na Hospitali 54 katika mikoa tisa ya Kanda ya Ziwa.

Mwanza. Sh3 bilioni zinatarajiwa kutumika kutoa matibabu kwa watu zaidi ya 100,000 wenye matatizo ya macho katika Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Tabora, Katavi na Geita.

Fedha hiyo pia itasaidia kukarabati miundombinu inayotumika kwenye matibabu ya macho katika vituo na Hospitali 54 kwenye mikoa hiyo, kutoa mafunzo kwa watoa huduma, vifaa vya matibabu na upasuaji wa maradhi hayo.

Fedha hizo zimetolewa kupitia 'Mradi wa Kuimarisha Huduma Bora Jumuishi za Afya ya Macho' unaotekelezwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ufadhiri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) wakishirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo linalolenga kusaidia watu wenye ulemavu duniani (CBM).

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 17, 2023 jijini Mwanza wakati wa kliniki ya vipimo na matibabu bila malipo kwa wananchi, Mkurugenzi Mkaazi Shirika la CBM Tanzania, Nesia Mahenge amesema mradi huo umeanzishwa mahsusi kusaidia wananchi baada ya kubaini mahitaji makubwa ya matibabu ya macho.

Amesema utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Novemba 2023 hadi Desemba 2025 na kuwanufaisha wananchi zaidi ya 100,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Kupitia mradi huu tumetoa Sh3 bilioni kwa hospitali ya Bugando ambayo ilileta maombi kutekeleza mradi wa afya ya macho baada ya kuona kuna mahitaji mengi kwenye eneo hili, kwahiyo tunategemea zaidi ya wakazi 100,000 kupata huduma hii na maelfu zaidi kupata elimu ya kujikinga na vitu vinavyohatarisha afya ya macho,” amesema Mahenge

Daktari bingwa wa Macho Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, James Shimba amesema tatizo la macho ndani ya jamii ni kubwa na watu wengi hawalizingatii ambapo hufika hospitalini wakiwa wameshaathirika zaidi nakuwata wananchi kufika mapema kupata matibabu pindi tu wanaposikia kuwashwa macho, kutokwa na tongotongo na uoni hafifu.

Amesema Bugando hupokea wagonjwa 100 na watoto 70 kila siku wenye matatizo mbalimbali ya macho ikiwemo mtoto wa jicho, mzio (allergy) na presha ya macho akiwataka wananchi wanapokuwa kwenye shughuli zao za kiuchumi kuzingatia usalama wa kazi kwa kuvaa vitu vya kulinda macho.

“Kuna shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazoweza kuhatarisha afya ya macho mfano waendesha pikipiki ambao hawavai kofia ngumu (helmet) wanaweza kuumiza macho watakapopata ajali, kuponda kokoto bila tahadhari pia ni hatari kwa sababu watu wengi wanakuja macho yametobolewa na kokoto, kuna wachomeleaji hawavai vitu vya kulinda macho kwahiyo wanahatarisha afya ya macho yao,” ameonya Dk Shimba

Naye, Benedicto Kato, ambaye ni mlemavu wa kusikia, ameiomba hospitali ya Bugando na Serikali wanapoandaa kliniki hizo na matibabu mengine kuwafikiria watu wenye ulemavu kwa kuweka wakalimani kwani wanapata changamoto wanapofika kupata huduma, huku akiomba huduma hiyo itanuliwe zaidi na kufika mbali kwa wananchi wengi ambao hawajanufaika.