Watoto wa mitaani wafunguka wanayoyapitia

Muktasari:

  • Watoto wanaoishi mitaani na kufanya kazi huko, wameiomba Serikali kuwapatia nyumba ya kuishi, elimu ya ujasiriamali na ufundi Ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Arusha. Dharau, lugha za matusi na vipigo vya mara kwa mara wakati mwingine bila kosa, ni baadhi ya madhila wanayokumbana nayo watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Ili kuondokana na hilo, wameiomba Serikali kuwakusanya pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali, mikopo ya vijana hasa wale waliosogea umri.

Wamesema lengo la kuhitaji kupatiwa mtaji ni waweze kujitegemea kimaisha, kuchangia pato la Serikali kupitia ulipaji wa kodi, lakini pia kupunguza wimbi kubwa la watoto wa mitaani na uhalifu.

Wameyasema hayo leo Aprili 19, 2024 jijini Arusha kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Mtaani yaliyoandaliwa na kituo cha kulelea watoto hao cha Amani Center kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii, usalama na dawa za kulevya.

Katika maadhimisho hayo, watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pia walialikwa ambapo Ayubu John amesema mazingira wanayoishi hayana kesho nzuri, kutokana na kutokuwa na uhakika wa kupata mahitaji muhimu kama chakula, mavazi, matibabu na malazi.

“Hakuna mtoto au kijana yoyote anayependa kuishi mtaani bali ni hali ya maisha ndio tunajikuta hapa, hivyo tunaomba jamii isituchukulie kwa mtizamo hasi kila wanapotuona katika maisha haya na kututupia matusi, lugha chafu na kutudharau kwani hata na sisi ni binadamu,” amesema.

Erick Isaya akisimulia moja ya mkasa wake, amesema huwa anabeba mizigo ya watu wanaokwenda masokoni kununua mahitaji mbalimbali na kuwasaidia hadi kituo cha magari, anakumbana na madhila mengi ikiwemo kudhulumiwa fedha, kusingiziwa kuiba na hata kushushiwa kipigo anapodai malipo yake ya kazi.

“Mimi nabeba  mizigo kutoka hapa soko kuu hadi kituo cha usafiri mtu anapoenda, na unaweza kabisa kupatana na mtu bei ni Sh2,000 au 5,000 kutokana na ukubwa wa mzigo lakini akifika kule anakupa hela anayotaka na ukidai anaweza kukuitia mwizi, au kukutukana kitendo ambacho kinaweza kukusababisha hasira na ukaamua kuzua vurugu,” amesema.

Amesema madhila hayo yanawaweka katika ushawishi wa kufanya uporaji, wizi au hata kupigana na wateja wanaowatumikisha na hawataki kuwalipa fedha waliyokubaliana.

“Ili kukabiliana na hili, Serikali ifanye mpango wa kuwarudisha watoto wenye familia zao, na wengine waliobaki wasajiliwe, wapewe nyumba ya pamoja ya kuishi, kwa ajili ya kupatiwa elimu ya ujasiriamali na mikopo ili tufanye biashara, tujitegemee kimaisha,” amesema Erick.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Amani Center kilichopo Arusha, Naomi Kimaro amesema wanaadhimisha siku hiyo kila mwaka kwa ajili ya kuwakumbusha wazazi na walezi wajibu wa kulea watoto wao vema ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani.

“Hakuna mtaa unazaa watoto ndugu zangu, hawa wote mnaowaona wanatoka kwenye familia na jamii zetu na ongezeko lao ni kuonyesha kuna mahali mimi na wewe tumeteleza kwenye wajibu wetu wa malezi. Siyo  kweli watoto wote hawa hawana wazazi au hata ndugu wa wazazi wao ndio maana tunakumbushana kila mwaka,” amesema Naomi.