Moto wateketeza nyumba Tabata, gari la Zimamoto lakwama kuifikia

Muktasari:

  • Wapangaji washindwa kuokoa chochote, msongamano unaotokana na ujenzi holela wa makazi wakwamisha gari la Zimamoto kufika eneo la tukio.

Dar es Salaam. Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika umeteketeza nyumba eneo la Tabata Kisiwani, Dar es Salaam.

Moto huo uliozuka leo Alhamisi Mei 2, 2024 saa moja usiku umeteketeza nyumba na mali zote zilizokuwamo ndani.

Wakati moto huo ukitokea imeelezwa wakazi wake ambao ni wapangaji hawakuwapo hivyo, jitihada za kuokoa mali kuwa changamoto kufanikiwa.

Licha ya jitihada za wananchi kuzima moto kwenye nyumba hiyo inayoelezwa ina wapangaji zaidi ya 10 hawakufanikiwa kuokoa chochote.

Mwananchi Digital imefika eneo la tukio na kukuta wananchi wakiendelea kuzima moto huo kwa kutumia maji kutoka kwenye mfereji.

Hata hivyo, madhara ya moto huo yangeweza kudhibitiwa iwapo gari la Jeshi la Zimamoto na Ukoaji lingefika ilipo nyumba hiyo, lakini hilo lilishindikana.

Hali hiyo ilijitokeza kutokana na kukosekana njia ya gari hilo kupita ikichangiwa na ujenzi holela usiozingatia mpangilio wa makazi.

Baadhi ya mashuhuda wameeleza moto huo ulizuka ghafla. Halima Mohamed, mpangaji kwenye nyumba hiyo amesema hakuna kitu alichoweza kuokoa.

Amesema ndani ya chumba chake kulikuwa na fedha ambazo hakutaja kiasi gani, nguo zake na za watoto wake pamoja na samani za ndani.

Mpangaji mwingine, Sebastian Mboga amesema wakati anatoka kazini akiwa anafungua mlango alihisi harufu na baadaye aliona moshi kutoka kwenye moja ya vyumba.

Amesema walijaribu kuvunja mlango waweze kuzima moto lakini ulikuwa umeshaenea kwenye vyumba vingine.

"Kama tungepata msaada mapema moto usengesambaa kwa kasi kiasi hiki lakini, kutokana na jiografia ya eneo hili moto ulituzidi," amesema.

Kijana aliyejitambulisha kwa jina la Ramadhani aliyeshiriki kuzima moto huo amesema baada ya kuanza kuwaka walitoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji baada ya kuzidiwa.