Ununuzi wa mazao sasa kidigitali 

Moja ya mashamba ya mpunga ambao ukivunwa unatarajiwa kwenda kuuzwa  NFRA.

Muktasari:

  • Serikali inalenga kumuwezesha mkulima kurahisisha uuzaji wa mazao yake sambamba na kufungua vituo vya ununuzi kwa mtindo wa kisasa zaidi.

Rukwa. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mkoani hapa, umesema utafungua vituo vya ununuzi wa mazao katika maeneo mbalimbali sambamba na kutumia mizani ya mifumo ya kidigitali kwenye  ununuzi.

Umesema lengo ni kutaka kuwarahisishia wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi na bila bugudha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 27, 2024 ofisini kwake mjini Sumbawanga, Meneja wa NFRA Mkoa wa Rukwa, Marwa Range amesema vituo vitakavyofunguliwa vitatumia mizani ya kidigitali kupima uzito wakati wa kununua nafaka kutoka kwa wakulima mkoani humo.

 "Tumepanga kununua zaidi ya tani 100,000 za  nafaka, wakulima walete mahindi yaliyokauka na yasiyo na unyevu, wafike ofisini ili kuepuka udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kwa sababu  sisi hatutumii madalali katika ununuzi wa nafaka,” amesema Range.

Amesema vituo vyote vitakavyofunguliwa vitatumia mizani hiyo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi ya ununuzi wa nafaka na kupunguza malalamiko.

“Wafanyabiashara wakubwa na wakulima wote hasa wadogo, wasisite kuleta nafaka zikiwa safi maana tumepanga kununua mahindi meupe na mpunga katika msimu huu wa ununuzi, hivyo  wahakikishe wanaleta nafaka hizo katika ubora unaotakiwa,” amesema Range.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mkakati huo wa NFRA, mkazi wa kijiji cha Kizi wilayani Nkasi, Daniel Mwanakusha amesema moja ya changamoto wanayokutana nayo pindi wanapopeleka kuuza nafaka ni pamoja na kuambiwa mahindi ni machafu na hivyo kujikuta wanatumia gharama kubwa kurudi nayo nyumbani.

“Ndiyo maana wakati mwingine huwa tunaamua kwenda kuuza sokoni, la kama wanatuhakikishia hakutakuwa na usumbufu huo tena, watatupata wengi,” amesema Mwakanusa.

Naye mkulima  kutoka katika kijiji cha Mtowisa Wilaya ya Sumbawanga vijijini,  Elizabeth Tengu ameuomba wakala huo kulipa fedha kwa wakati.

“Hatutarajii kukopwa, wakinunua tu watulipe maana ndiyo tunazitegemea hela hizo kwa mambo mbalimbali ya kifamilia,” amesema.

Hata hivyo, Meneja Range amewatoa hofu wakulima kuwa hakuna atakayekopwa. “Kila mkulima atalipwa kwa wakati, hatutarajii kumkopa mkulima yeyote,” amesema meneja huyo.

Amesema vituo vitakavyokuwa wazi kwa msimu huu wa ununuzi kwa Sumbawanga ni Mazwi, Kanondo na Laela.

Kwa  Wilaya ya Kalambo amesema ni pamoja na cha Mwimbi, Matai na Mkombo, pia amesema kuna vituo vitakavyohamishiwa Wilaya ya Sumbawanga vijijini ambavyo ni Kaengesa na Mtowisa huku Wilayani Nkasi ni Namanyere, Mtenga , Kasu na Ntalamila.