NFRA kuanza tena kununua mahindi Songwe

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akijibu hoja mbalimbali za wananchi kwenye mkutano wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa uliofanyika mjini Vwawa mjini hapa, amesema Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), utaanza tena kununua mahindi baada ya kusitisha ununuzi huo tangu Septemba mwaka huu.

Songwe. Serikali imesema Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), utaanza tena kununua mahindi baada ya kusitisha ununuzi huo tangu mwezi Septemba mwaka huu, kutokana na kuwa na deni kubwa kwa wakulima mkoani hapa.

Kitendo cha kutangaza kuanza tena ununuzi, kumefikiwa baada NFRA kulipa sehemu kubwa ya deni (Sh26 bilioni), lililotokana mauzo ya nafaka, yaliyofanywa kati ya wakala huo na wakulima wa Mkoa wa Songwe.

Kauli hiyo inayotafsiriwa kama habari njema  kwa wakulima hao, imetolewa jana, Novemba 24, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati akijibu hoja mbalimbali za wananchi katika mkutano wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa uliofanyika mjini Vwawa.

Silinde amesema Mkoa wa Songwe pekee ulikuwa unadai zaidi ya Sh26 bilioni lakini deni hilo limelipwa na kusalia deni la zaidi ya Sh300 milioni.

“Nimepata maelekezo kutoka kwa waziri wangu, Hussein Bashe kuwa deni la mahindi lililosalia litalipwa Jumatano, Novemba 29 mwaka huu na kuhakikisha Serikali itaendelea kununua mahindi kutoka kwa wakulima,” amesema Silinde.

Awali Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila ameiomba Serikali kupitia NFRA, kuwalipa wakulima fedha zao ili waweze kurudi tena shambani kuzalisha.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema bei ya mbolea katika soko la dunia imepanda ambapo mfuko mmoja wa kilo 50 unauzwa zaidi ya Sh120, 000,  hata hivyo amebainisha kuwa Serikali inatoa Sh50, 000 kama ruzuku kwa mkulima, ili kupunguza gharama za uzalishaji.

“Niwatake wananchi msitoe mbolea hiyo nje ya nchi, kwani kufanya hivyo ni uhujumu uchumi, na jana nimewafokea watu wa Ileje kwa kuuza mbolea ya ruzuku nchi jirani ya Malawi, kwani kitendo hicho ni sawa na mauaji,” amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani hapa.