Umbali, hali duni vichocheo vya utoro shuleni

Korogwe. Mapema mwaka huu baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kutoka na kujikuta amefeli, hivyo kutakiwa kurudia darasa; Saum Balo (17) alikata tamaa ya kuendelea na masomo.

Saum, mwanafunzi wa sekondari ya Madago iliyopo Kata ya Madago, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni miongoni mwa wengi shuleni hapo kutoka vijiji vilivyo mbali, ambao wamepanga nyumba katika Kijiji cha Makuyuni ili kuwa jirani na shule.

Baada ya matokeo aliona anapoteza muda kuwa shuleni, hivyo alitamani atafute njia nyingine ya kupata ujuzi kwa haraka, akaazimia kuwa fundi wa kushona nguo.

Haikuwa rahisi kuwashawishi wazazi wake kwamba anaacha shule ili akajifunze ufundi, hivyo akatumia mwanya wa kuwa mbali na nyumbani kuondoka shuleni. Hata hivyo, aliishia kwenda kufanya kazi za ndani.

“Nilikaa wiki tatu sijaenda shuleni hakuna aliyefahamu, nyumbani walijua nipo shule kama kawaida. Ijumaa nilikuwa nakwenda nyumbani Mswaha nachukua fedha ya matumizi narudi Makuyuni,” anasimualia.

Saum anasema, “Baada ya kufanya hivyo kwa muda, nilipata wasiwasi itakuwaje wazazi wangu wakigundua siendi shuleni. Kuna jirani yangu nilipokuwa naishi, nikazungumza naye anisaidie kupata kazi.” Kwa msaada wake, anasema alipata kazi za ndani mkoani Kilimanjaro, hivyo alikwenda pasipo kuwajulisha wazazi na walimu wake. Siku chache baada ya kuanza kazi, anasema alitafutwa shuleni ndipo taarifa zikafika kwa wazazi wake.


Kauli za walimu

Makamu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Madago, Warioba Mwita-Mashauri anasema utoro wa binti huyo uliwashtua na kuwatia shaka.

Anasema waliwasiliana na mzazi wake, ambaye naye alishtushwa na taarifa hizo, kwa kuwa alijua mtoto yuko shuleni.

“Hapa hatuna hosteli, lakini tuna watoto wanaotoka vijiji vya mbali, wanatembea umbali wa kilomita takribani 20 kuifuata shule. Wengi wao wamepanga hapa kijijini, hivyo tuna changamoto kubwa ya ufuatiliaji,” anasema.

Mwalimu huyo anasema, “Huyu ni miongoni mwa watoto waliokuwa hapa kijijini tulipoona utoro wake umezidi tukaanza kufuatilia kwa mzazi, kumbe hata yeye hana taarifa na wakati tayari binti ameshaondoka kwenda kufanya kazi za ndani Moshi. Jitihada zilifanyika kuhakikisha anarudi.”

Mmoja wa walimu shuleni hapo, Justin Kimario anasema hawakuwa tayari kumuona Saum akikatiza masomo na kuishia kufanya kazi za ndani.

“Tuna changamoto kubwa ya watoto huku vijijini kushawishiwa kwenda kufanya kazi za ndani. Maeneo wanayokimbilia ni Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Zanzibar. Tumeamua kwa dhati kukabiliana na hili, maana tumegundua kuna watu wanawashawishi na hatuwezi kuruhusu hili liendelee,” anasema.

Kimario alisema, “Tuliwaeleza wazazi kwamba vyombo vya dola vitahusika ndipo jitihada zikafanyika hadi leo mwanafunzi yuko shuleni.”

Kwa ushirikiano wa wazazi, walimu na uongozi wa kijiji, Saum alirejea wilayani Korogwe na kujiunga na wenzake shuleni.

Wazazi na walimu walimjenga kisaikolojia hali iliyochangia kumrudisha kwenye mstari katika kipindi cha muda mfupi kama anavyothibitisha mwenyewe.

“Nakiri nilifanya makosa ila dhamira yangu ilikuwa nijifunze kitu kingine, sikuwa tayari kuendelea kuadhibiwa kwa kufeli maana nilijiona sitaelewa tena. Nashukuru wazazi na walimu wangu kwa kuniweka kwenye mstari. Wamezungumza nami vya kutosha kuhusu umuhimu wa shule,” anasema.

“Nimeelewa vyema kila nilichoambiwa, ndiyo sababu nimerejea shuleni na nafurahia uamuzi huu. Najiandaa kwa marudio ya mtihani na sifikirii tena kuacha shule, nitasoma hadi nimalize,” anasema Saum huku akibubujikwa machozi.

Si Saum pekee aliyepitia hali hii, wapo wengine walioamua kuacha masomo ili kutafuta njia nyingine zitakazowasaidia kuingiza kipato ndani ya muda mfupi, kwa kile wanachodai hali ngumu ya maisha.


Simulizi ya Paul

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika sekondari ya Mashewa katika halmashauri hiyo, William Paul aliacha shule na kwenda mgodini kutafuta kipato ili kuendesha maisha yake na ya familia.

“Nilipofaulu kidato cha kwanza hata shuleni nilichelewa kuripoti, sikuwa na vifaa vinavyohitajika, ilinichukua muda mrefu kupata sare, hatimaye nikaja shuleni hata hayo madaftari alinipatia mwalimu. Kwa kifupi nimetoka familia masikini,” anasema.

Paul anasema, “Kwa kuwa nyumbani kwetu ni mbali Kijiji cha Kwebamba, ilibidi nije kukaa kwa ndugu hapa jirani na shule. Hata hivyo, baada ya muda akaniambia niondoke maana watoto wake wanarudi hivyo nyumba haitatosha,” anasema.

Anasema aliishi maisha magumu na alipofika kidato cha tatu, wakati mwingine alishinda njaa akaona asiteseke, hivyo akarudi nyumbani na kujiunga na wachimbaji madini.

Anasema alijiunga na mgodi uliopo Kalalani akifanya shughuli zilizompatia angalau Sh5,000 kwa siku, fedha aliyotumia kusaidia familia yake.

Jitihada za walimu ziliwezesha Paul kurejea shuleni. Mwaka huu anatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne akiwa miongoni mwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani.


Takwimu za utoro

Kwa mwaka pekee, wanafunzi wa sekondari 690 wamekatisha masomo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa utoro sugu na ukosefu wa mahitaji.

Takwimu za Idara ya Elimu Sekondari kwa mwaka 2023 zinaonyesha wanafunzi 554 kati yao wasichana 255 na wavulana 299 wamekatisha masomo kwa sababu ya utoro sugu, huku wengine 122 wakiacha kwa sababu ya ukosefu wa mahitaji kutokana na hali duni ya maisha.

Hali ilikuwa vivyo hivyo mwaka 2022; wanafunzi 390 walikatisha masomo kutokana na utoro sugu, huku wengine 80 waliacha shule kwa sababu ya kukosa mahitaji.

Aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Halfan Magani alikiri kuwapo changamoto ya wanafunzi wanaoacha masomo kwa kushawishiwa kwenda kufanya shughuli nyingine kwa ajili ya kujitafutia kipato.

“Jamii za watu wengi ni masikini, kwa hiyo huangalia matokeo ya haraka. Mzazi haoni shida kumpeleka mtoto akafanye kazi za ndani ili apate mshahara wa Sh50,000. Anaona fedha hiyo ni kubwa, hivyo suala la shule linaweza lisiwe kipaumbele. Hata hivyo, tunaendelea kuielimisha jamii ione umuhimu wa elimu,” anasema Magani.

Kuhusu umbali, alisema huchangia wanafunzi kuacha shule, akitoa mfano kwamba wapo wanaotoka kata ya Kalalani wanaolazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule ya sekondari Kata ya Mashewa.


“Tunalitambua hili na tunalifanyia kazi kwa kuwa tayari fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kujenga sekondari katika Kata ya Kalalani,” alisema.

Alisema pia wanatarajia kujenga hosteli katika sekondari ya Madago kuwawezesha wanafunzi kukaa mazingira ya shule.

“Kwa mwanafunzi kukaa bweni ni vigumu kuacha shule, hata kiwango chake darasani kitakuwa kizuri tofauti na yule anayetembea umbali mrefu kwenda shuleni na kurejea nyumbani,” anasema Magani.


Mwongozo wa elimu

Hatua zilizochukuliwa na walimu wa wanafunzi hawa zinaendana na maelekezo yanayotolewa katika mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali uliotolewa Februari 2022.

Lengo la jumla la mwongozo huo ni kutoa maelekezo yatakayowezesha urejeshwaji wa wanafunzi waliokatiza masomo ili wakamilishe mzunguko wa masomo yao katika mfumo rasmi.

Mwongozo pia unalenga kushirikisha wadau kuhusu wajibu wao katika kuwarejesha wanafunzi waliokatiza masomo, kuwezesha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wake.

Kundi hili linajumuisha wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu nyinginezo, zikiwamo umasikini, utoro, watoto kuwa walezi wa familia zao, ajira za utotoni, kuishi katika mazingira magumu, umbali kutoka nyumbani hadi shuleni, kuishi na mzazi au mlezi mmoja na kutowajibika kwa wazazi.

Mwongozo unamtaka mkuu wa shule kuhakikisha wanafunzi waliorejeshwa shuleni wanahudhuria na kujifunza kikamilifu na kuandaa mazingira wezeshi na rafiki kwa wanafunzi waliorejeshwa shuleni.

Unaelekeza pia kumsaidia mwanafunzi aliyekatiza masomo kuhamia shule nyingine ikiwa hayuko tayari kuendelea na masomo katika shule ya awali, na kuhakikisha wanafunzi wote wakiwamo wanaorejea shuleni baada ya kukatiza masomo wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za shule.

Akizungumzia hilo, Magani anasema ufuatiliaji unafanyika kuanzia ngazi ya halmashauri, kata hadi shuleni kuhakikisha wanafunzi waliorejea shuleni wanaendelea kubaki na kuwafuatilia wanaokwenda kinyume.

“Kila ngazi inachukua hatua yake halmashauri tunatimiza jukumu letu la ufuatiliaji kupitia idara zetu za msingi na sekondari, ukishuka kule kwenye kata tunao maofisa elimu kata ambao wanaangalia shule zote zilizo ndani ya kata, ufuatiliaji wao unakuwa wa karibu zaidi kwa kushirikiana na wakuu wa shule ndiyo maana nasema kwa upande wa ufuatiliaji kazi inafanyika,” anasema Magani.


Sera mpya ya elimu

Inawezekana wapo watoto wengi wenye mawazo kama ya Saum na Paul wanaoamini katika ujuzi nje ya mfumo rasmi wa elimu. Kuacha shule haitakuwa na ulazima kwa kuwa kupitia sera mpya ya elimu inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2024 kutakuwa na mkondo wa elimu ya amali.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika Septemba 7, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema licha ya kuwa kidato cha tano na sita kutakuwa na mkondo wa amali, zipo shule zitaimarishwa kwa ajili ya kutoa michepuo maalumu itakayowasaidia wanafunzi kubobea katika eneo husika.

“Rasimu ya sera inasema elimu ya lazima kwa kila mtoto ni miaka 10, elimu ya msingi miaka sita halafu miaka minne ni lazima uendelee na sekondari hadi kidato cha nne. Baada ya hapo kutakuwa na mikondo miwili, elimu ya kawaida na mafunzo ya amali ambayo yote itakuwa na michepuo mbalimbali,” alisema.

Alisema endapo pendekezo la wizara litapita, mwakani watarejesha mkondo wa amali katika ufundi, michezo na kilimo.