Wazazi waonywa kuwahusisha wanafunzi sherehe za harusi usiku

Afisa tarafa ya Sisimba jijini Mbeya, John Mboya (aliyesimama kulia) Akizungumza na wanafunzi na walimu alipofanya ziara katika Shule ya Sekondari Itagano kukagua hali ya taaluma shuleni hapo.

Muktasari:

  • Ziara ya ofisa tarafa ililenga kupitia na kukagua hali ya taaluma kwa shule zilizopo kata hiyo, ambapo ilibainika kuwapo utoro kwa wanafunzi huku mikesha na harusi za usiku zikitajwa kuchangia changamoto hiyo na kushusha kiwango ufaulu.

Mbeya. Wazazi na walezi wametakiwa kutowashirikisha watoto wao kwenye shughuli za kijamii hususani harusi na mikesha ya usiku ili kuondokana na utoro shuleni na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Akizungumza leo Septemba 27, wakati wa ziara yake katika shule ya sekondari Itagano, Ofisa Tarafa ya Sisimba jijini Mbeya, John Mboya amewataka wazazi na walezi kutowaruhusu wanafunzi kushiriki sherehe za usiku ambazo zinachangia utoro.

Amesema lazima wazazi na walezi wazingatie suala la elimu kwa watoto wao ili kuongeza kiwango cha ufaulu, akibainisha kuwa kumekuwapo na utoro kwa baadhi ya shule na kufanya ufaulu kushuka.

“Hivyo lazima kila mzazi na mlezi kumlinda na kumfuatilia mtoto wake kuhakikisha anafika shuleni, tuachane na kuwashirikisha kwenye shughuli za kijamii hususani harusi na mikesha mingine kwani hii inasababisha utoro na kushuka kwa taaluma,” amesema Mboya.

Mboya amemtaka mkuu wa shule hiyo, Ditrick Ng’imbi kukutana na wazazi na walezi wa wanafunzi ambao ni watoro shuleni hapo kuzungumza nao kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo na kuahidi ziara hiyo kuwa endelevu hadi kwa shule za msingi katika kata 15 anazoongoza jijini humo.

Kwa upande wake Ng’imbi amesema hata kabla ya maelekezo hayo wamekuwa wakikutana na kufanya vikao kadhaa na wazazi ili kuendelea kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi.

Amesema moja ya hatua walizofikia ni pamoja na kuazimia kila mzazi au mlezi atakayekutana na mwanafunzi akizurula barabarani ni kumpeleka shuleni, au katika ofisi ya mtendaji kwa kushirikiana na Askari wa Kata hiyo.

“Mara nyingi wanafunzi wanawapeleka shambani na kwenye harusi lakini kwa sababu Shule hii tuko na ukaribu sana na Afisa mtendaji tumeazimia na wazazi wote kila mmoja kuwachunga wanafunzi,” amesema.

“Yeyote anayekutwa anazurura akamatwe na kupalekwa shuleni au zilipo ofisi za mtendaji na hili tumeomba na askari wa kata watusaidie, kimsingi hapa shuleni utoro siyo mkubwa,” amesema Ng’imbi.

Mmoja wa wazazi Victoria Mwakipesile amesema jukumu la kumlinda mtoto linaanzia ngazi ya familia na kuomba kuwapo mkakati maalumu kwa viongozi kufanya ziara za kushtukiza shuleni ili kubaini mahudhurio ya wanafunzi.

“Tusimtupie lawama mwalimu hili la mwanafunzi ni jamii yote inahusika kwenye malezi, ukimuona mtoto analandalanda mitaani bila mpangilio ukanyamaza lazima atakuathiri, tushirikiane kutengeneza kizazi imara, viongozi wafanye ziara za kushtukiza,” amesema Victoria.