Polisi wamchunguza DED Mafia aliyetenguliwa na Rais Samia

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Kassim Ndumbo

Muktasari:

  • DED huyo anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi wa msaidizi wao wa kazi, huku taarifa zikieleza kuwa ameshaanza kuhojiwa na vyombo vya dola

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji linamchunguza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia (DED), Mkoa wa Pwani, Kassim Ndumbo kwa tuhuma za kufanya ngono na mfanyakazi wake wa ndani (jina limehifadhiwa) anayedaiwa kuwa na umri chini ya miaka 18.

Hatua hiyo imebainika saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa DED huyo usiku wa Aprili 18, 2024 akiwa Istanbul, Uturuki alikoenda kwa ziara ya kikazi.

Hata hivyo, taarifa ya kutenguliwa kwake iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus kwa vyombo vya habari haikueleza sababu za hatua hiyo.

Taarifa zilizoifikia Mwananchi zinadai kuwa Ndumbo anatuhumiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti huyo, jambo lililobainika  baada ya mkewe kugundua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Protas Mutayoba amelieleza Mwananchi kuwa wameanza kuchunguza suala hilo baada ya kufikishiwa.

“Si kwamba tulikuwa tunamchunguza, ndiyo tumeanza kumchunguza baada ya shauri hilo kuletwa polisi. Kikubwa ni kwamba anatuhumiwa kufanya vitendo vya ngono na mtu aliyekuwa ‘hausigeli’ wake. Tunataka tukamilishe uchunguzi wetu, tupate mashahidi na huyo binti kwa sababu hayupo Mafia. Inabidi tumpate ili tupate maelezo yake tukamilishe kila kitu.

“Kwa hiyo utaratibu wote tumeshauweka, litadhihirika tu ili twende nalo mbele, hatua za kisheria zichukue mkondo wake,” amesema.

Juhudi za kumpata Ndumbo ili kuzungumzia tuhuma hizo hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe haukujibiwa.

Hata hivyo, chanzo kimoja cha taarifa za tukio hilo kilieleza kuwa hiyo jana alikuwa Polisi anakohojiwa.


Uchunguzi zaidi

Mbali na Polisi, mmoja wa maofisa waandamizi wa Ofisi ya Rais-Tamisemi aliyeomba hifadhi ya jina lake alipoulizwa amesema: “Ni kweli tuhuma hizo za kutembea na dada wa kazi na sisi tumezisikia na uchunguzi wa vyombo vya dola unaendelea.”

Ofisa huyo ameongeza: “Lakini sijajua kama kutenguliwa kwake kumetokana na hizo tuhuma, labda mnaweza kuwasiliana na Polisi wanaweza kuwa na majibu zaidi.”

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema taarifa zilizopo ni kwamba Ndumbo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wake wa ndani kwa muda mrefu, hadi walipokuja kugunduliwa na mke wake.

“Kuna video iliyorekodiwa na picha za mnato zinawaonyesha jamaa akiwa chumbani na binti huyo. Inaonyesha ni mpango uliosukwa ili kuwanasa. Kwa hiyo si kwamba amembaka, ila walikuwa na uhusiano kwa muda mrefu,” kimeeleza chanzo chetu.

Ndumbo ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliteuliwa kuwa DED wa halmashauri hiyo Julai 31, 2021 na alikuwa atimize miaka mitatu Julai, 2024.

“Aliteuliwa akitokea Tanga na wote na mkewe ni walimu. Walipokuja hapa walikuwa na huyo hausigeli, kwa hiyo wako naye muda mrefu,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, binti huyo ameondolewa nyumbani hapo baada ya tukio hilo na kuwa Ndumbo ameshaitwa na kuhojiwa na vyombo tofauti, likiwamo Jeshi la Polisi.

 “Kabla ya kutenguliwa uteuzi wake, Serikali imeshachukua hatua. Kwa mfano, aliitwa kuhojiwa na Polisi na wamefanya upelelezi. Jana ilikuwa aende kwenye kikao cha ALAT (Jumuiya za Serikali za Mitaa) Taifa kinachofanyika Zanzibar, lakini alishindwa kuondoka,” kimesema chanzo hicho.

Mtoa taarifa mwingine anayeishi kisiwani Mafia na ambaye pia hakutaka kutajwa jina, amesema Ndumbo amekuwa kwenye vipindi virefu vya mahojiano na Jeshi la Polisi wilayani humo.

“Hata hapa ninapozungumza na wewe (saa nane mchana) yuko Polisi anahojiwa, lakini akimaliza anaenda nyumbani. Tatizo mtoto anayedaiwa kufanya naye mapenzi ana umri mdogo,” amedai.

Chanzo hicho kimesema hata “mkewe ameondoka hapa kisiwani tangu jana, kwa sababu ya tuhuma hizo.”